Sunday, 31 December 2017


Askofu Kakobe Umekosea sana kuigeuza nyumba ya Ibada takatifu na kuifanya kama Uwanja wa kuongelea mambo yahusuyo Siasa. Ni kweli  kila mtanzania  ana Uhuru wa kuongea na kutoa maoni yake lakini pia tufahamu wakati sahihi na mahala Sahihi pa kuwasilisha jambo fulani na wewe  kama Kiongozi na Mtumishi wa Mungu  tambua  MUKTADHA ama Ujumbe wako na Mazingira ya kuongelea jambo fulani, haikuwa mahala sahihi kuongelea mambo yahusuyo Siasa tena unayemlenga hayumo humo kanisani.

Kwa Uelewa wangu mdogo, kanisa kama eneo ama jengo ni mahala ambapo watu hukusanyika ili kupewa mahubiri/ mafunzo ya maneno matakatifu ya Mungu. Kanisani ni sehemu takatifu ya Kumwabudu Mungu, ni sehemu ya kuwaambia waumini waliokusanyika humo maovu yao ili  wayaache na kumrudia Mungu. Sasa huwezi kuacha kuhubiri habari za  Yesu Kristo ukaanza kuwahubiria  waumini habari za Siasa na wakati wamekuja kujifunza neno la Mungu. 

Tukumbuke  Kuna namna nzuri ya kuwasilisha ujumbe wako baada ya kumtambua vizuri uliyemkusudia kumpelekea huo Ujumbe wako. Mimi siwezi nikaanza kukusema wewe kakobe mtumishi wa Mungu kwa kupayuka tu na wakati natambua wewe ni nani katika Taifa hili na vivyo hivyo unatambua John Pombe Magufuli ni Kiongozi Mkuu wa Nchi katika Taifa hili kwa nini usingeomba appointment ya kuonana na Rais Magufuli na kumweleza ya moyoni. Hata vitabu vitakatifu pia vinazungumzia habari ya kuheshimu watawala halali wa Nchi, sasa kuheshimu ni pamoja na kumtambua mtawala halali wa Taifa lako ambaye amepata kibali kutoka kwa Mungu. Kama unataka kumkosoa basi yule si kama mimi ambaye unaweza kufanya ulivyofanya yule ni Mtawala na Kiongozi Mkuu wa Nchi mfuate umueleze na kumshauri vizuri. Muombe msamahama Rais Magufuli na waumini wako hata wao hukuwatendea haki.

Aidha Askofu Zacharia  Kakobe nikushauri kama umeamua kuwa mwana siasa fuata taratibu za Nchi kusajili Kanisa lako kuwa Chama Cha Siasa au Ubaki kuwa Mtumishi wa Mungu  na ufuate dhumuni hasa la Kanisa lako maana ulichokifanya ni kukiuka dhumuni la kuanzishwa kwake.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU WABARIKI NA KUWAHEKIMISHA VIONGOZI WETU WA DINI, MUNGU BARIKI RAIS WETU WA TANZANIA.

Robert PJN Kaseko
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha.
December 29, 2017.

Post a Comment: