Wednesday 29 November 2017

Waziri Majaliwa Atua Bandalini Ampa Agizo Hili IGP Sirro


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo Novemba 29, 2017 amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simo Sirro kuwakamata Bw. Bahman wa Kampuni ya NAS na Wakala wa Kampuni wa Wallmark Bw. Samwel kwa kutaka kutoa Bandarini magari makubwa 44 aina ya Semi Trailer bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.
 
Aidha, Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka viongozi wa juu serikalini.
 
“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia au Waziri Mkuu cha kuruhusu kutoa mzigo wake bila kufuata taratibu, akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema Waziri Mkuu.
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatano alipofanya ziara ya kushtukiza Bandarini baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka kutapeli kutoa magari hayo yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kutoka nchini Uturuki.
 
Hatua hiyo imekuja baada ya Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwamba amewasiliana ana Waziri Mkuu na wasipotekeleza agizo hilo watapata matatizo.

Post a Comment: