Serikali Kuajiri Maafisa Ugani Katika Kila Kata Nchini
Serikali imepanga kuongeza idadi ya Maafisa Ugani wenye ujuzi katika kila Kata na Kijiji ili kuleta mapinduzi ya kilimo Nchini.
Hayo yameelezwa
na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. William Ole Nasha wakati
akijibu swali lililohusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inafanya
mapinduzi ya kilimo kwa kuwa na wataalamu wa kutosha, leo Bungeni mjini
Dodoma.
Naibu Waziri huyo
amesema kuwa Serikali inatambua kuwa Sekta ya Kilimo ni muhimu na ndiyo
yenye kuajiri watanzania wengi hivyo mapinduzi ya kilimo yatachangiwa
na uwepo wa wataalam wa kutosha wenye taaluma na ujuzi stahiki ili
waweze kushauri matumizi ya teknolojia na kanuni bora za kilimo.
“Hadi kufikia
mwaka 2016/2017 Serikali imeajiri maafisa ugani 8,756 sawa na asilimia
43 ya mahitaji ya maafisa ugani 20,374 katika ngazi ya Kijiji, Kata na
Wilaya,” amefafanua Naibu Waziri Ole Nasha.
Aidha, Naibu
Waziri Ole Nasha aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha na
kuwezesha vituo vya kilimo na vituo vya Rasilimali za kilimo za kata
(WARCs) kwa ajili ya kufundishia teknolojia mbalimbali za kilimo.
Vilevile alisema
kuwa Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kuandaa miongozo
na mafunzo ya huduma za ugani, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa
kazi za Ugani na kuboresha usambazaji wa teknolojia za kilimo bora kwa
wakulima nchini.
Mbali na hayo Serikali inaendelea kusomesha vijana na kuwaajiri kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
Na Beatrice Lyimo- MAELEZO DODOMA
Post a Comment: