“Ikulu ni Kazi Tu Sikuja Kutafuta Mchumba”- Rais Magufuli
“Watanzania tumechezewa kwa miaka
50, sasa ni wakati wa kufanya kazi; lazima tuamke tukatae kuibiwa huku
tunakoimbiwa sasa kama kwamba tumerogwa” alisema Dkt. Magufuli mara baada ya kukabidhiwa ripoti hizo.
Aliwaambia viongozi na wananchi
waliokuwa wakifuatilia tukio hilo kupitia vituo vya televisheni, redio
na mitandao ya kijamii kuwa Ikulu ni sehemu ya kupita na yuko radhi
aonekane mwanasiasa mkorofi asiyependwa lakini lazima atatekeleza jukumu
lake la kutetea na kulinda rasilimali za taifa kwa manufaa watanzania
wote wa leo, kesho na mtondogoo.Alibainisha kuwa fedha zinazoibiwa kwa matrilioni zingetosha kubadili maisha ya watanzania wengi kwa kuwapatia huduma za jamii na hata kulipana mishahara mikubwa hivyo akiwa Rais hawezi kukubali hilo liendelee.
“Tuangalie maisha yetu yalivyo kila
mmoja amuangalie jirani yake anavyoishi maisha ya shida huku rasilimali
zote zikiibiwa na watu wakituacha katika umasikini,” alieleza Rais Magufuli na kuongeza kuwa wanyonyaji hao hawana huruma kabisa na watanzania.
Akionesha kuchukizwa na matokeo ya
ripoti hizo, Rais Mafuguli alisema kama baadhi iliyoelezwa kuwa udhaifu
huo unatokana na mfumo basi huo mfumo lazima ufumuliwe.
“Unaposaini mikataba ya aina hii na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inahusika basi kama ni mfumo tuufue ili
tufikie mahala maslahi yetu ya nchi yapewe kipaumbele” alisisitiza Rais Magufuli na kuongeza kuwa “Tukienda kwa utaratibu huu, tutakuwa watumwa milele”
Katika hotuba yake hiyo, Rais alisema
mambo mengine ni aibu kuyasema na kusisitiza kuwa yeye hataki baada ya
kumaliza muda wake kuwa miongoni mwa wale wanaotajwa kuwa “Nae alikuwepo hapa“Alisema yeye binafsi angependa kuona watanzania wanakuwa matajiri kutokana na rasilimali zao si kuwanufaisha watu wa nje na makuwadi wao wa ndani ambao aliwaeleza kuwa watu waliokosa uzalendo.
Alizipongeza ripoti hizo kuwa zimekidhi matarajio yake na kwamba zimempunguzia kazi ya kutafuta wataalamu wengine kuchunguza jambo hilo na kulipongeza Bunge kwa kutimiza wajibu wake huo vyema.
Katika mnasaba huo alimuagiza Waziri Mkuu kuwaita wataalamu wa sheria washirikiane na Bunge kukaa pamoja na kufanya marekebisho ya sheria.
“Tusiulizwe kwa nini tunabadili sheria hivi sasa kwani jibu ni wazi kuwa huu ndio wakati unaofaa kufanya hivyo,” alisisitiza Rais Magufuli.
Katika mkutano huo alivipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhabarisha wananchi na akatoa wito kwa vyombo hivyo kuendelea kuelimisha wananchi wajitambue na kuwa wazalendo
Post a Comment: