Saturday, 9 September 2017


                                                    Hussein Bashe.
MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kuiagiza Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kukaa na vyombo vya usalama ili kujadili hali ya usalama nchini ilivyo kwa sasa kufuatia kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Bashe aliyasema hayo jana bungeni Mjini Dodoma wakati akielezea tukio la kushambuliwa kwa Lissu.

“Mheshimiwa spika tukio hili lililotokea ni tukio la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu… hoja yangu ni kwamba, katika nchi yetu kumekuwa na matukio mbalimbali ambayo sisi kama wawakilishi wa wanachi tunahitaji kupewa taarifa.

“Ben Sanane alipotea hatujasikia kama wahusika wamekamatwa au la! Msanii ROMA Mkatoliki alitekwa naye hatujasikia chochote. Waziri Nape Nauye alitolewa bastola hadharani lakini hatukusikia mhusika huyo akifikishwa katika vyombo vya sheria wala kusikia kauli yoyote yenye matumaini."

“Jana (juzi), Tundu Lissu alipigwa risasi tena ndani ya majengo ya nyumba za mawaziri na viongozi, sisi tunawakilisha Watanzania milioni 50. Matukio haya yanaharibu taswira ya nchi ya Tanzania, nakuomba Spika, uiagize Kamati ya Ulinzi na Usalama ikutane na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kujadili hali hii ili tuweze kupata taarifa sahihi kuhusu kinachoendelea, kwa hali inavyoendelea hakuna mtu mwenye uhakika na maisha yake,” alisema Bashe.

Post a Comment: