Zitto Kabwe: Rais Magufuli Akiniteua Nitakataa!
Rais Magufuli (kulia) akisalimiana na Zitto Kabwe, kushoto ni Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa hatokubali endapo Rais Dkt Magufuli
atamteua kushika nafasi yoyote ya uongozi kwani hatakuwa na fursa ya
kukijenga chama chake ili kiwe tayari kushinda uchaguzi na kushika dola.
Zitto ambaye chama anachotoka tayari kimetoa viongozi wawili ambao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Elisha Mghwira alisema endapo atateuliwa, atamshukuru Rais na kukataa uteuzi huo.
Zitto Kabwe ambaye ni Mbunge wa Kigoma
Mjini aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na gazeti la Mwananchi
wakati akijibu swali kuhusu uteuzi wa viongozi wa chama chao ambao
mmoja alikuwa mshauri wa chama na mwingine alikuwa mwenyekiti wa chama
hicho kichanga Tanzania.
“Sitakubali uteuzi kwa sababu
jukumu langu na viongozi wengine wa ACT- Wazalendo ni kujenga chama ili
kupata ushawishi na kuungwa mkono na umma na hatimaye kushika dola,” alisema Zitto.
“Kukubali uteuzi utakaoniondoa na
kuniweka kando kwenye jukumu na malengo hayo ni kufifisha matumaini ya
maelfu ya wana-ACT Wazalendo,” aliongeza Zitto.
Akizungumzia sababu za chama kuridhia
uteuzi wa Prof. Mkumbo, Zitto alisema kwamba hapo hali ilikuwa ni
tofauti kwa sababu kabla na baada ya uteuzi wa Mkumbo, yeye ni mtumishi
wa umma, hivyo uteuzi wake haukushtua.
“Mama Anna Mghwira alikuwa ni
mwanasiasa kwa nafasi yake ya uenyekiti Taifa, ndio maana tulimuondoa
ili kumpa fursa kutumikia serikali.”
CHANZO: MWANANCHI
Post a Comment: