WAZIRI MKUU: APIGA MARUFUKU AJIRA ZA WATOTO

*Ahimiza elimu kwa mtoto wa kike, akemea mimba za utotoni
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora wawapeleke
watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya
tumbaku.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo (Jumapili, Agosti 13, 2017) wakati
akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa
wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo
maalum.
“Ninasisitiza
kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi
sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo kama vibarua kwenye mashamba
ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la kuondoa watoto
kwenye ajira,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kusisitiza viongozi
wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa
wanahitimu elimu ya sekondari.
“Kuna
tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo hili pia linahitaji usimamizi
ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao. Tuwalinde wanaposoma
elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa wamepevuka
na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” alisema.
Akihutubia
kwenye mikutano ya hadhara wakati wa ziara yake ya siku nne moani
Tabora, Waziri Mkuu aliwaasa vijana wa kiume wasithubutu kuwaoa mabinti
wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia kufungwa jela miaka 30.
Pia
aliwaasa wazazi wanaoamua kuwaoza mabinti zao ili wapate mahari, nao
pia wana hatari kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 endapo watabainika
kushirikiana na waoaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 14, 2017.
Post a Comment: