Thursday, 10 August 2017

 kiongozi wa chama - Act wazalendo Ndg Zitto Kabwe

Chama cha *ACT Wazalendo* kimeshtushwa na kauli (amri) ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu John Pombe Magufuli aliyoitoa hivi karibuni akiwa Mkoani Tanga ya kutaka Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mazingara, Kata ya Mkata, Wilayani Handeni , katika Mkoa wa Tanga ahamishwe katika kituo hicho mara moja,hakimu huyo liyefahamika kwa jina la Laizer ametakiwa kuhamishwa katika kituo hicho, kufuatia kutuhumiwa kupendelea wafugaji katika kesi za Wakulima dhidi ya Wafugaji.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Godwin Gondwe dhidi ya Hakimu huyo akimtuhumu kuwa kesi zote kati ya wakulima na wafugaji katika mahakama hiyo, wanaoshinda katika kesi hizo ni wafugaji, na kwamba anapendelea wafugaji.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Agosti 9, 2017 na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Katiba ACT, Thomas Msasa, amesema chama hicho kinalaani kauli hiyo, kwa madai kuwa inakiuka misingi ya Katiba ya nchi inayoipa Mahakama haki na uhuru wa kufanya kazi yake bila kuingiliwa na mihimili mingine.
“Kauli hii inakiuka Katiba ya nchi ya mwaka 1977, Ibara 107b ambayo inaipa mahakama haki na uhuru wa kufanya kazi yake bila ya kuingiliwa wala kubughudhiwa na mihimili mingine. Katiba inaainisha mgawanyo wa madaraka baina ya Serikali, Mahakama na Bunge,” amesema na kuongeza.

“Kitendo cha Ndugu Rais kutaka Hakimu wa Mahakama achukuliwe hatua kwa kuhamishwa ni kuingilia mhimili wa mahakama. Tunaamini kuwa hata kama tuhuma dhidi ya hakimu mhusika ni za kweli, basi lazima utaratibu wa hatua za kinidhamu kwa hakimu huyo zifuatwe kwa kuchunguzwa kwanza, kupata ushahidi na akikutwa na hatia achukuliwe hatua na mamlaka yake ya nidhamu ambayo ni Tume ya Utumishi wa Mahakama.”

Aidha, Msasa amevitaka vyama vya mawakili vya Tanganyika na Zanzanzibar na taasisi nyingine kupigania utawala wa Katiba na Sheria nchini kwa kuilaani kauli hiyo. Pia amesema ACT inamsihi Rais Magufuli kumchukulia hatua za kiutawala Gondwe kwa madai kuwa amemuingiza kwenye mgogoro wa Kikatiba usio wa lazima.

Post a Comment: