SHAKA: “Jukumu la kuleta maendeleo Pemba ni la wote”
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) umesema kuwa Jukumu la kuleta maendeleo ya kiuchumi katika jamii
ni la kila mwananchi sio jukumu la serikali pekee.
UVCCM imesema kuwa jukumu la serikali ni kuwaonyesha wananchi fursa zilipo na namna bora ya kuzichanganua ikiwa ni pamoja na
kufanya kazi ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla
wake sambamba na kuwezeshwa kupata mikopo katika vikundi vyao vya
ujasiriamali.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu
Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Ndg Shaka Hamdu
Shaka leo Agosti 16, 2017 alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama
Cha Mapinduzi na jumuiya zake katika mkutano wa ndani uliofanyika katika
ukumbi wa Jamhuri Wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema kuwa vijana ni nguvu kazi ya
Taifa hivyo wanapaswa kutumia nguvu zao vizuri kwa kufanya kazi ili
kujikwamua kiuchumi katika familia zao badala ya kukaa maskani kujadili
mambo yasiyokuwa na tija kwao.
Aliongeza kuwa UVCCM inaunga mkono
vijana kukaa maskani kwa maslahi mapana ya mjadala wa Maendeleo
yatakayopelekea kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujiunga katika
vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.
Shaka alisema kuwa Kila mwananchi kwa
nafasi yake anatakiwa kuwajibika kwa nafasi aliyonayo ndani ya chama ama
serikali kwani wananchi wanataka maendeleo ya uchumi wao sio ahadi hewa
za majukwaani.
Aidha, alisema kuwa Serikali ya Chama
Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe Dkt John Pombe Magufuli ipo pamoja na watanzania wote ambao ni
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ama wale ambao sio wanachama wa vyama
vya siasa kwani mchakato wa maendeleo hauangalii itikadi za vyama vya
siasa.
Alisema wananchi wanatakiwa kutumia
Tunu ya amani, umoja na mshikamano uliopo nchini kufanya shughuli za
maendeleo na kujiepusha na maneno ambayo yataleta chokochoko za kuondoa
mshikamano katika jamii.
Shaka alisema kuwa vijana wanatakiwa
kujiajiri katika ujasiriamali kwa kuchukua hatua za makusudi
za kujiajiri kwani kusubiri ajira za serikali zitawachelewesha na
pengine kufikia hatua ya uzee pasina kuajiriwa kutokana na uchache wa
ajira serikalini na wingi wa vijana.
Kaimu Katibu Mkuu wa umoja wa Vijana
UVCCM ameanza ziara ya kikazi jana Agosti 15, 2017 visiwani Pemba ikiwa
ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi ya
mwaka 2015-2020.
Post a Comment: