SERIKALI YATOA UFAFANUZI UJIO WA BOMBADIER
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya
Habari – MAELEZO, Bibi. Zamaradi Kawawa akisisitiza jambo wakati wa
mkutano wake na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusiana
na taarifa za kuzuiwa kwa ndege ya Serikali aina ya Bombadier ambayo
inatengenezwa nchini Canada. (Picha na: Idara ya Habari – MAELEZO)
Serikali
imethibitisha na kuwahakikishia Watanzania kuwa ujio wa ndege mpya ya
tatu aina ya Bombardier Q400-Dash 8 upo pale pale licha ya baadhi ya
wanasiasa wasio wazalendo kutumia kila njia kukwamisha ujio huo.
Kauli
ya kuthibitisha ujio wa ndege hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Bi. Zamaradi
Kawawa wakati akiongea na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam.
Alieleza
kuwa kuchelewa kwa ndege hiyo ambayo ilitakiwa kuwasili mwezi Julai
mwaka huu kumetokana na majadiliano yanayoendelea ambayo kimsingi
yamechangiwa na baadhi ya wanasiasa wasio wazalendo kushiriki kwao moja
kwa moja kuweka zuio mpaka pale majadiliano yatakapo kamilika.
“Kuna
baadhi ya Watanzania wenzetu wenye maslahi binafsi wanapiga vita ndege
hii kuletwa nchini lakini Serikali inawahakikishia wananchi kuwa ndege
itakuja na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi”, alisisitiza Zamaradi.
Alieleza
kuwa Serikali iliishapata fununu kuwa kuna kuna baadhi ya viongozi wa
chama cha siasa wana mpango wa kukwamisha juhudi za ujio wa ndege mpya
na kwamba bila hata chembe ya uzalendo, watu hao wamejidhihilisha
wenyewe hadharani kwamba wapo nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za
Serikali kwa maslahi yao binafsi.
“Serikali
imesikitishwa sana kwa hujuma zinazofanywa waziwazi na kwa ushabiki wa
hali ya juu na baadhi ya viongozi wa kisiasa kupingana na mwelekeo mzuri
wa Rais wa kuleta maendeleo”, alieleza Zamaradi.
Aidha
alisema kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za diplomasia na za
kisheria kwa wote wanaoshabikia na kutengeneza migogoro na hujuma
mbalimbali dhidi ya maendeleo ya nchi yetu.
Kwa
mujibu wa Zamaradi, kuna wanasiasa waliokwenda kufungua madai kwamba
Serikali ya Tanzania inadaiwa na kwamba ndege hiyo ishikiliwe hawana
uhalali wowote wa kufanya hivyo na ni vibaraka waliotumwa na wapiga dili
wasioitakia mema Tanzania.
Katika
siku za hivi karibuni kumeibuka baadhi ya wanasiasa Watanzania ambao
wamekuwa wakitoa kauli zenye lengo la kuhujumu maendeleo ya nchi ikiwemo
kushawishi wafadhili kuinyima misaada Tanzania lakini pamoja na
jitihada hizo, washirika wa maendeleo wameendelea kuongeza misaada kwa
Tanzania kutokana na kuridhishwa na hatua mbalimbali za Serikali katika
kupambana na rushwa na ufisadi na kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Post a Comment: