Prof. Makame Mbarawa awashukia wafanyabiashara JK AIRPORT
Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa Mwezi mmoja kwa
wafanyabiashara wanaotoa huduma katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kulipa kodi ya Majengo kama mikataba yao
inavyolekeza.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo leo
wakati alipokutana na wafanyabiashara hao ili kujadili changamoto
mbalimbali zilizopo na jinsi ya kuzitatua ili kuendelea kutoa huduma
bora katika uwanja huo.
“Kulipa kodi za majengo hapa ni
suala la lazima, hivyo ifikapo Septemba mwishoni nataka kuona
wafanyabiaashara wote mmeshalipa kodi ya pango, makusanyo haya ni muhimu
kwetu ili tuendelee na hatua nyingine za uboreshaji wa viwanja vya
ndege na huduma nyinginezo,” alisisitiza Profesa Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ameutaka uongozi
wa Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Kuhakikisha mikataba
yote ya upangishaji wa majengo inapitiwa upya na kufanyiwa marekebisho
ili thamani ya fedha iendane na wakati huu.
Profesa Mbarawa amewahimiza
wafanyabiashara hao kubadilika na kuendana na mabadiliko ya Sayansi na
Teknolojia ili kuweza akuendana na ushindani wa kibiashara uliopo ndani
na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea
kujenga mazingira mazuri kwa wafanyabiashara nchini ili waweze kufanya
biashara zao ili kujiingizia kipato binafsi na kukuza pato la Taifa.
Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa
amekagua sehemu ya kuingilia abiria katika uwanja huo ambapo amesema
Serikali itaweka mpango maalum wa muda mfupi kwa wasafiri wanaoenda nje
kutotumia muda mrefu katika ujazaji wa fomu wakiwa uwanjani hapo.
“Kwa kushirikiana na taasisi zote
zinazotoa huduma katika uwanja huu tutaweka mpango maalum utakaowezesha
wasafiri kuhudumiwa kwa haraka na kwa muda mfupi, Msafiri yoyote
anataka huduma za haraka ili waweze kuwahi na sisi tutahakikisho
tunakidhi mahitaji ya wateja,” alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande Kaimu MKurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi amesema
Mamlaka imeshapitia mikataba yote ya wafanyabiashara kiwanjani hapo na
hatua inayofata ni kufatilia madeni yote ili kuboresha huduma katika
kiwanja hicho.
Bw. Msangi ameongeza kuwa kwa yale madeni ambayo hayataweza kulipwa kwa wakati taratibu za kisheria zitafuatwa.
Post a Comment: