Jaji Mkuu, Polisi Watoa ONYO Mgomo wa Mawaikili Nchi Nzima
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa
Ibrahim Juma na Jeshi la Polisi nchini, wamelionya Baraza la Uongozi la
Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), kutoingilia vyombo vya
uchunguzi na upelelezi, vinavyochunguza tukio la mlipuko, uliotokea
kwenye ofisi za Kampuni ya Mawakili ya IMMMA usiku wa kuamkia juzi
jijini Dar es Salaam.
Profesa Juma jana alisema TLS hawana
haki ya kutoa agizo kwa mawakili, kutohudhuria mahakamani na kwenye
mabaraza mengine, kwa kuwa kila wakili ana mkataba binafsi na mteja
wake.
Profesa Juma alisema uhuru wa mahakama ni pamoja na kuheshimu mamlaka nyingine za nchi zinapokuwa zinafanya kazi zake.
Alisema kwa kuwa tukio la kulipuliwa
kwa ofisi za Mawakili wa Immma ni tukio la kihalifu, hivyo wanasheria
waiache Polisi na vyombo vingine vya upelelezi kufanya kazi yao.
“Kama kutatokea wateja
watakaolalamika kuwa mawakili wao hawakufika mahakamani siku ya Jumanne
na Jumatano, hatua za kisheria dhidi ya mawakili hao zitachukuliwa
ikiwemo kuwapeleka kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili,” alieleza Kaimu Jaji Mkuu.
Kwa upande wao, Jeshi la Polisi limesema liachwe liendelee na kazi ya uchunguzi, badala ya kulihusisha na tukio hilo.
Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu,
Kamishina Msaidizi Barnabas Mwakalukwa alisema Jeshi la Polisi ndicho
chombo chenye mamlaka ya kufanya uchunguzi na hivyo kama kuna mtu yeyote
mwenye taarifa yoyote kuhusu tukio hilo, anatakiwa kuzitoa polisi
badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Kauli hizo za Polisi na ya Kaimu Jaji
Mkuu, zimekuja baada ya Rais wa TLS, Tundu Lissu kuwaeleza waandishi wa
habari Dar es Salaam jana kuwa Baraza lao la Uongozi lina taarifa kuwa
kikundi cha watu wenye silaha za moto, wakiwa wamevalia sare za Jeshi la
Polisi, kiliwateka nyara walinzi binafsi wa Kampuni ya IMMMA na kuingia
ndani ya eneo la ofisi hizo.
Lissu alidai watu hao baada ya
kuingia ndani, walitega milipuko na madumu manne ya mafuta ya petroli
katika maeneo kadhaa ya jengo la ofisi hizo.
Alidai muda mfupi baadaye, milipuko
hiyo ililipuka na kusababisha uharibifu mkubwa wa jengo la ofisi za
IMMMA Advocates zilizoko Upanga pamoja na majengo jirani.
“Kama Lissu ana hizo taarifa
alitakiwa azilete polisi kwa kuwa ndicho chombo cha uchunguzi badala ya
kuzungumza na vyombo vya habari.
“Kazi ya polisi ni kufanya
uchunguzi wa kina na ndiyo maana Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu alisema
atatoa taarifa uchunguzi ukikamilika, hivyo watu wanapaswa kusubiri
taarifa kamili, nje ya hapo tunakuwa tunafanya kazi nje ya utawala wa
sheria,” alieleza Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mwakalukwa.
Mwakalukwa alivitaka vyombo vya
habari, kuwatafuta walinzi hao ambao Lissu alidai walitekwa na watu
wanaodhaniwa kuwa polisi ili waeleze tukio lilivyokuwa na ikibidi
walinzi hao kutoa taarifa za kutekwa kwao polisi.
Alisema jambo hilo siyo dogo, hivyo
watu waviache vyombo vya uchunguzi, viendelee na kazi yake kwani
uchunguzi pekee ndiyo utakaobaini chanzo na wahusika.
Ili kuonesha mshikamano, Baraza la
Uongozi la TLS limewataka mawakili wote ambao ni wanachama wao nchini,
wasuse kuhudhuria mahakamani na kwenye mabaraza ya aina zote kwa siku
mbili, kesho na keshokutwa.
Post a Comment: