Agizo la DC wa Singida kwa wananchi kuhusu waharifu wa Kibiti, Pwani
Mkuu wa wilaya ya Singida, Elias
Tarimo, amewaagiza wakazi wa wilaya hiyo kuwafichua wageni wasioeleweka
kwa madai baadhi ya wauaji kutoka Kibiti mkoani Pwani, wameaanza
kukimbilia wilayani humo kwa lengo la kujificha.
Wilaya
ya Singida ina halmashauri ya wilaya ya Singida yenye makao yake makuu
ya muda katika kijiji cha Ilongero na halmashauri ya manispaa.
DC Tarimo ametoa agizo hilo juzi mbele ya kikao cha kawaida cha madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Singida.
Akilijengea
nguvu agizo lake hilo, alisema hivi karibuni jeshi la polisi liliuwa
mwanaume mmoja anayeaminika ametokea Kibiti, wakati wa majibizano ya
risasi kati yake na Polisi.
“Wakati
tunafanya operation ya kuwahamisha wavamizi haramu kwenye hifadhi ya
msitu wa Magori, raia wema walitupa taarifa kwamba nyumbani kwa wananchi
mmoja (jina tunalo), kuna mgeni ambaye wanamtilia shaka kwamba atakuwa
ni kutoka kikundi kinachouwa wananchi wasio na hati huko Kibiti,” alifafanua.
Akifafanua
zaidi, alisema baada ya taarifa hiyo, Polisi waliizingira nyumba hiyo
na mgeni huyo alipoombwa kujisalimisha na atoke nje, aligoma.
“Baada
ya kugoma, bomu la machozi lilipigwa ndani ya nyumba hiyo kitendo
kilichosababisha atokee dirishani huku akifyetua risasi. Risasi moja
ilipiga kifuani kwa polisi mmoja lakini alinusurika kufa, kutokana na
kuvaa kinga dhidi ya risasi. Ni chechetu ndizo zilizomjeruhi kwenye
shavu,” alifafanua zaidi.
Alisema
kutokana na tukio hilo,wakazi wa wilaya ya Singida wanapaswa kuwa
makini na ujio wo wote wa wageni wasioeleweka. Wakimtilia shaka mgeni
yoyote, watoe taarifa haraka kwa viongozi wao au kwenye kituo cha polisi
kilicho karibu.
“Tusiruhusu
wilaya yetu ikageuzwa kuwa kitovu cha uhalifu au maficho ya watu wenye
harufu ya vitendo vya ugaidi.Nasisitiza tulinde wilaya yetu, mkoa wetu
na nchi yetu kwa ujumla ili amani na utulivu uendelee kudumu,” alisema Tarimo.
Wakati huo huo, mkuu huyo wa wilaya,aliagiza mabango yote ya matangazo ya tiba asilia, yang’olewe na kuharibiwa.
Amesema
baadhi ya waganga wa madawa asili na wanajihusisha na vitendo vya ramli
chonganishi ambazo zina madhara makubwa ikiwemo kuchangia vifo.
“Kuna
tukio la kutisha limetokea katika halmashauri ya wilaya ya Singida hivi
karibuni. Hawa wapiga ramli chonganishi walienda kwenye mji moja na
kudai mtoto mdogo aliyekuwa mgonjwa si binadamu ni jini,” alisema na kuongeza.
“Baada
ya hapo akawashawishi wazazi wa mtoto huyo, wamchome moto. ili aweze
kubadilika na kuwa binadamu. Mtoto alichomwa moto na kuwa majivu na
kuacha vilio na simazi kwa familia.”
Na Nathaniel Limu, Singida
Post a Comment: