SERIKALI YATANGAZA KIAMA KWA WANAOHUSIKA NA HUMAN TRAFFIC (BIASHARA YA WATU)

BALOZI DK AUGUSTINE MAHIGA
SERIKALI imepata majina ya baadhi ya wahusika wa mtandao wa kimataifa
unaohusika kusafirisha na kuuza nje ya nchi wasichana wa Kitanzania wa miaka
kati ya 16 na 24, kwa kisingizio cha kuwatafutia ajira.
Aidha, imesema tayari mawasiliano na serikali za
nchi wanakopelekwa wasichana hao yamefanyika kuhakikisha wanakamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu wanachokifanya ni biashara haramu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Augustine Mahiga alieleza Bunge jana akiwasilisha Makadirio
ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Balozi Mahiga aliweka wazi kuwa katika orodha wamo
Watanzania wanaoishi nchini na wengine nje ya Tanzania wanaoshirikiana na wageni.
Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, kufanikiwa kupata majina hayo kumetokana na
ushirikiano kutoka kwa Jumuiya za Watanzania waishio nchini Thailand na India
pamoja na waathirika wa biashara hiyo haramu.
“Kwa hapa nyumbani uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana
na balozi za nchi ambazo wasichana wetu wanapelekwa ili kubaini watu wote walio
sehemu ya mtandao huo, hususan wanaowezesha upatikanaji wa vibali vya kusafiria
kwenye balozi hizo ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria,”
alisema Balozi Mahiga.
Alisema tayari serikali imeziomba balozi hizo ziwe
makini zaidi kudhibiti uombaji wa vibali vya kusafiria kwa shughuli mbalimbali
na kuwataka wahusika kuthibitisha uwezo wa kifedha walionao kufanya utalii,
kufanya shughuli au kuishi kwenye nchi wanazokwenda ili kuudhibiti mtandao huo.
Alisema, wanamtandao hao wanaojihusisha zaidi
kuuza watu ili washiriki ukahaba, huwanyang’anya, kushikilia pasipoti za
wasichana wanaowarubuni na kuwadai Dola za Marekani 5,000 hadi 6,000, baada ya
kuwafikisha wanakowapeleka, jambo linalokuwa gumu kutekelezwa na wasichana hao
kwa kukosa fedha, hivyo kujikuta wakikubali kufanya biashara ya ukahaba.
“Ninatoa mwito kwa Watanzania wote tuwe makini
pale tunapopata fursa za kazi nje ya nchi. Ni muhimu kuzingatia na kujiridhisha
kuhusu masuala ya msingi yanayohusu ajira za nje ikiwa ni pamoja na kuwepo
mkataba rasmi wa ajira unaotambuliwa na mamlaka husika zilizopo nchini na za
nchi ambayo mtu anataka kwenda,” alisema.
Alitoa rai pia kwa Watanzania wanaokwenda nje
kufanya kazi kujisajili kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania uliopo katika nchi
hizo na kutokubali kuweka hati za kusafiria rehani. Balozi Mahiga aliwataka
wananchi waelewe kuwa ahadi nyingi za ajira kwa nchi za Thailand, Malaysia na
China zinatolewa na watu wasio waaminifu wanaoshiriki katika mtandao wa
biashara haramu ya watu.
Aidha, alisema bado kuna Watanzania kadhaa
wanatumikia vifungo na adhabu ya kifo katika magereza ya nchi mbalimbali
duniani baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa
za kulevya. Alitaja nchi waliko na idadi yao kwenye mabano kuwa ni Brazil (41),
China (266), Iran (68), Thailand (14) na Umoja wa Falme za Kiarabu (3).
Post a Comment: