HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO,
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU
WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO,
MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA
UPINZANI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA
TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17
Inatolewa chini ya
Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
_________________________
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Mwanafalsafa Baron Montesquieu aliwahi kuandika ifuatavyo kuhusu mgawanyo wa madaraka “Pale ambapo madaraka ya Bunge na ya
Serikali kuu yanakuwa yamehodhiwa na mtu mmoja, au katika chombo hicho hicho
cha hukumu, hakutakuwa na uhuru, kwa sababu hofu itazuka, utawala huo huo au
bunge litatunga sheria kandamizi na kuzitekeleza kwa mfumo kandamizi. Pia
hakutakuwa na uhuru endapo madaraka ya Mahakama, Bunge na Serikali
hayatatenganishwa. Pale ambapo madaraka
ya Serikali kuu yanapokuwa yamefungamanishwa na Bunge, uhai wa Bunge na Uhuru
wake unakuwa katika hatari kubwa ya kudhibitiwa kiholela: kwa kuwa Jaji
hawezi kuwa mtunga sheria. Pale ambapo Serikali kuu imefungamanishwa na
mahakama, basi Jaji anaweza kuwa na tabia ya mabavu na ukandamizaji. Inakuwa
mbaya zaidi, pale ambapo mtu huyo huyo au chombo hicho hicho, iwe ni wateule wa
Serikali au watu wengine wanapotumia hayo madaraka ya kutunga sheria,
kutekeleza maazimio ya umma na kutoa hukumu za jinai au tofauti za watu”
Mheshimiwa Spika, Kwa
mujibu wa mada iliyowasilishwa na Profesa P.J. Kabudi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam juu ya “Mafundisho ya Mgawanyo
wa Madaraka na jinsi yanavyotumiwa Tanzania” (Doctrine of Separation of Powers
and its Application in Tanzania: Success, Challenges and Prospects) ni
kwamba; hakuna mgawanyo dhahiri wa
madaraka baina ya mihilimili mikuu ya dola na kwamba bado Tanzania ina
‘hang-over’ ya ulevi wa siasa za chama kimoja . Sehemu ya Mada hiyo inasomeka
hivi: nanukuu; “Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 bado
inatumika mpaka leo pamoja na kuwa marekebisho yalikuwa mfano wa Ustawishaji wa
mfumo wa chama kimoja nchini Tanzania. Katiba pia iliendelea kustawisha dhana
ya Ukuu wa Chama kushika hatamu. Ibara ya 3 na 10 zilibainisha kuwa CCM ndio
chama pekee cha Siasa Tanzania na kuwa shughuli zote za Serikali ilibidi
zifuate sera na miongozo ya chama. Hii ilimaanisha kuwa Bunge na Mahakama
vilitakiwa kufuata maelekezo ya chama katika kutenda majukumu yao. Zaidi ya
yote, kama ilivyokuwa kwa Katiba ya Mpito, ibara ya 63(4) ya Katiba ililifanya
Bunge kuwa kamati maalumu ya Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa. Ilikuwa ni jambo
la kawaida pale ambapo bajeti ya wizara imekwama basi wabunge waliahirisha
mkutano na Bunge lilikaa kama kamati ya Chama ili kujadili hilo suala. Mara tu
uamuzi unapofikiwa basi Bunge linarejea na bajeti inapitishwa bila kuwa na upinzani mkubwa”
Katiba ya mwaka 1977 imerekebishwa mara kadhaa. Marekebisho makubwa zaidi yalikuwa ni yale ya tano, ambayo yaliingiza Haki za Binadamu katika Katiba, na marekebisho ya nane yaliyofanyika mwaka 1992 yaliyorejesha tena Mfumo wa Vyama Vingi Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maudhui ya nukuu ya mwanafasafa wa kale wa Sayansi ya Siasa Montesquieu, mada ya Profesa Paramagamba John Kabudi, na tabia isiyokubalika ya Serikali kuendelea kushawishi Mahakama na kulidhibiti Bunge kwa hila mbalimbali ni kwamba, Tanzania sasa iko katika hatari kubwa ya kuingia katika mfumo wa Dola la Kidikteta na tayari dalili zote za utawala wa namna hiyo zimeanza kuonekana.
Mheshimiwa Spika, vitendo vya hivi karibuni vya Serikali hii kukanyaga uhuru wa vyombo vya habari kwa kufuta kabisa usajili wa baadhi ya vyombo vya habari, kupiga marufuku urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya mijadala ya Bunge kupitia televisheni ya Taifa, kuingiza polisi ndani ya ukumbi wa Bunge na kuwapiga na kuwadhalilishwa wabunge; kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni sehemu tu ya tabia za utawala wa kidikteta.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakemea kwa nguvu zote ukandamizaji wa demokrasia na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Serikali ya Tanzania dhidi ya watu wake. Aidha, tunataka Jumuiya ya Kimataifa ijue na dunia ijue kwamba sasa Tanzania hakuna utawala wa kidemokrasia tena – kinachofanyika ni utekelezaji wa amri za Rais – yaani Presidential decrees.
Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni ya Kambi Rasmi
ya Upinzani kuhusu bajeti ya Serikali ya 2016/17, napenda kuweka rekodi sawa
kuhusu upotoshaji unaofanywa na Wabunge wa CCM kwamba Wabunge wa Upinzani
wanaisaini mahudhurio bungeni na kuchukua posho bila kufanya kazi. Napenda mkumbuke
kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikisisitiza kufutwa kwa posho
za vikao kwa maana ya “Sitting allowance”,
lakini serikali imekuwa ikipata kigugumizi, hivyo basi Kambi Rasmi inasema kama
kweli Serikali ya Rais John Pombe Magufuli inania thabiti ya kubana matumizi ya
Serikali basi inoneshe uthabiti huo kwa kuifuta posho ya vikao na fedha hizo
zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo hususani kuwapatia
Watanzania maji safi na salama. Hata hivyo, tunashauri, wale wanaokaa bungeni
bila kuchangia hata kwa maandishi na kuchukua posho, wafuatiliwe na wakatwe mishahara yao, kwa kuwa hawajafanya
kazi na hansard itumike kuwabaini.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada kuongeza mapato, Serikali
katika bajeti hii imekusudia kukata kodi ya asilimia 5 kwenye kiinua mgongo cha
wabunge. Kambi Rasmi ya Upinzani haina tatizo na pendekezo hilo, ila inaitaka
Serikali kwenda mbali zaidi kwa kuifanyia marekebisho sheria ya mafao ya
viongozi wa kisiasa ambayo kwa sasa imewapa misamaha ya kodi ya viinua mgongo
viongozi wakuu wa kisiasa kama Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Spika, Naibu Spika, Wakuu wa
Mikoa na Wakuu wa Wilaya ili sasa na wao walipe kodi hiyo. Hata hivyo, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaikumbusha Serikali kwamba kiinua mgongo cha
wabunge hutolewa mwisho wa uhai wa bunge husika, hivyo haioni mantiki ya kutoa
pendekezo hili sasa kwa kuwa halina impact kwa bajeti ya 2016/17.
2. HALI YA UCHUMI
Mheshimiwa
Spika, tunaposema hali ya uchumi
tunaangalia uchumi kwa ukubwa wake (Macro economy) katika nchi, mataifa
yanayotuzunguka na kwa dunia nzima, na ni kwa vipi sera zetu za uchumi
zinavyoathirika na uchumi wa dunia, na ni kwa jinsi gani watunga sera
wanatakiwa kuwa na mikakati itakayoweza kukabiliana na sera za wale
tunaotengamana nao kibiashara.
Mheshimiwa
Spika, Na katika hili ni lazima tuangalie ni jinsi gani
uchumi mdogo (micro-economy) ambao ndio nguzo kuu ya nchi kwa maana unaowafanya
wananchi waweze kuishi, au sera za uchumi zinazoendesha biashara ndogo ndogo
kati ya kampuni na kampuni, na zinaangalia jinsi biashara zinavyoweza
kufanikiwa kwa kiwango cha juu na aidha, namna gani maamuzi ya biashara
yanatakiwa kufanywa ili biashara ziweze kufanikiwa, kwa maana nyingine ni
kushughulika na “supply and demand”, jinsi ya kufikisha uchumi kwenye
mifuko ya watu mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, kukua
au kutokukua kwa uchumi kutaonekana na jinsi
pato la taifa litakavyokua ambalo ni matokeo ya shughuli za uzalishaji
na utoaji wa huduma katika mzunguko mzima wa uchumi. Katika makadirio
yaliyokuwa yametolewa na serikali katika mpango wa maendeleo awamu ya kwanza
kwenye ukuaji wa uchumi ilitarajiwa kuwa ukuaji wa pato la taifa lifikie
asilimia 8. Hii iliwekwa kutokana na ukweli kuwa kwa mwaka 2011 GDP ilikuwa
7.9%, 2013 GDP ikawa 7.3% na miaka miwili mfululizo GDP ikawa 7.0% na matarajio
kwa mwaka 2016 ni 7.2%.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi hicho ukuaji wa baadhi ya sekta za uzalishaji pamoja na shughuli za utoaji wa huduma
ulikuwa kama ifuatavyo; Mawasiliano (14.9%),
Huduma za fedha na Bima (10.4%), Ujenzi (10.3%), Kilimo - kwa maana ya mazao, ufugaji,misitu na uvuvi (3.1%) kwa
kulinganisha na 3.4% mwaka 2014. Sekta hii licha ukuaji wake kuwa mdogo kwa
kulinganisha na mwaka wa nyuma lakini mchango wake katika Pato la Taifa
uliongezeka na kuwa 31.4% kulinganisha na 28.9% kwa mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa takwimu za Serikali, inaonesha kuwa kiwango cha riba za amana za muda
maalum kiliongezeka kutoka wastani wa asilimia 9.02 Januari, 2015 hadi asilimia
9.08 Januari, 2016, kiwango cha riba za amana kwa mwaka kiliongezeka hadi
11.01% kutoka 10.66% 2015. Riba za mikopo kiliongezeka kutoka 15.75% Jan. 2015
hadi asilimia 16.28 Jan.2016, wastani wa riba za amana za mwaka na riba za
mikopo za mwaka iliongezeka kutoka wastani wa 3.14% Jan.2015 na kufikia 3.33%
Jan.2016 Kambi Rasmi ya Upinzani inasema riba hizi zingeweza kuongezeka kama
Serikali isingekuwa inafanya biashara kubwa na mabenki na hivyo kupelekea
mabenki kushindwa kuhamasisha wananchi kufanyabiashara nayo.
2.1 USIMAMIZI WA
TAASISI NDOGO-NDOGO ZA FEDHA
Mheshimiwa Spika, Kambi
rasmi ya Upinzani inapenda kusisitiza tena kwa
Serikali kuleta muswada wa sheria ambao utaanzisha mamlaka ambayo itatoa
kisheria muundo wa kudhibiti na kusimamia taasisi ndogondogo za fedha nchini
ambazo kwa sasa zimekuwa zikisimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na
taasisi nyingine za kifedha kama mabenki. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona haja
ya kuwa na mamlaka huru iliyo chini ya Benki Kuu ya Tanzania ya kusimamia taasisi ndogondogo kama ambavyo
Benki Kuu ya Tanzania imeruhusu uanzishwaji wa mamlaka za kusimamia mifuko ya
hifadhi za jamii, bima na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, kuundwa
kwa chombo chenye mamlaka ya kusimamia
taasisi ndogondogo za fedha ni lazima kwa kuwa kwa sasa hakuna mrandamo wa
viashiria kwa mabenki na taasisi ndogondogo za fedha. Kutokana na utofauti wa
muundo wa mabenki na taasisi ndogondogo za fedha, inakua ni vigumu kudhibiti
riba na utoaji wa vigezo vya kifedha katika kuhudumia wananchi na kutoa mikopo
yenye unafuu.
Mheshimiwa Spika, hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani ni kuwepo na chombo chenye mamlaka
tofauti na Benki kuu ya Tanzania itakayosimamia na kuratibu taasisi ndogo ndogo
za fedha na kuziwezesha katika kutoa mikopo kwa wananchi hasa walio katika
sekta isiyo rasmi. Hivi sasa kumekuwapo na taasisi ndogondogo za kifedha ambazo
zinawapa fursa wananchi kujiunga katika vikundi vidogo vidogo na kuwapa elimu
ya ujasiriamali kisha kuwasaidia katika suala la mikopo ambayo utakaoweza
kuwapa fursa watanzania waliopo katika sekta isiyo rasmi kama wamachinga, mama
lishe, mafundi uashi na wajenzi, mafundi magari na seremala ambao chombo hicho kingeweza
kusimamia ukusanyaji wa fedha kutoka
katika makundi haya na kuweza kuwekeza kwa ajili ya kusaidia kutoa mitaji pale
inapohitajika.
Mheshimiwa Spika, hili ni suala zuri ambalo linalenga kuboresha maisha ya wananchi wa
vijijini na maeneo mbalimbali ya mijini. Pia, zipo Saccoss (vyama vya kuweka na
kukopa) na benki jamii (vicoba) ambazo zimekuwa na wanachama wengi wanaoendelea
kujiunga ili kujikwamua kiuchumi. Lakini kumekuwa na mapungufu kwa kuwa taasisi
ndodondogo za fedha zimeendelea kutumia masharti sawa na zile za mabenki ambazo
zimekuwa ni mzigo kwa mlengwa ambaye ndiye analipa riba kubwa kutokana na
masharti mazito yenye kulingana na vigezo vya kutoa mikopo kwa mabenki chini ya
Benki kuu ya Tanzania. Kwa mfano, taasisi za fedha chini ya Benki Kuu bado
zimeendelea kumtaka mtu awe na dhamana ya mali isiyohamishika na zile wanazojidhamini
kwa vikundi. Je, itawezekanaje kwa Mwananchi mwenye hali duni kuwa na dhamana
ya mali isiyohamishika?
Mheshimiwa Spika, kuwepo
kwa chombo chenye mamlaka pia itasaidia kuwa na Credit Reference Bureau
itakayokuwa na taarifa za wakopaji kutoka taasisi ndogondogo za fedha tofauti
na itakayosimamia wadaiwa wa mabenki na taarifa hizi zitasaidia udhibiti wa
wateja wa taasisi hizi kuchukua zaidi ya mkopo mmoja kwenye taasisi tofauti
tofauti ambapo hali hii husababishwa na uchelewashaji wa mikopo unaotolewa na
taasisi hizi pamoja na uhafifu wa mikopo katika kumsaidia mlengwa.
3. MPANGO WA TAIFA WA
MAENDELEO 2016/17
3.1.
Ugharamiaji
wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
2016/2017
Mheshimiwa
Spika, moja ya sifa kubwa ya Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano uliomaliza muda wake (2011/12 – 2015/16) ni kuweka
msingi wa kibajeti ulioitaka Serikali kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya
ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mpango ulisema hivi: nanukuu,
“kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya
uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35
ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya
maendeleo kila mwaka” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na uhalisia kwamba Mpango
huo haukutungiwa sheria ya utekelezaji; Serikali ilijificha katika kichaka cha
udhaifu huo; na matokeo yake kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango
huo, Serikali haikuwahi hata mara moja kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya
ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuna wakati mwingine
haikutenga hata senti moja. Kwa mfano katika mwaka wa fedha 2012/13 Serikali
haikutenga fedha yoyote kutoka katika mapato yake ya ndani kugharamia miradi ya
maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na Serikali kugoma kutoa
asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo, miradi
mingi ya maendeleo haikukamilika hadi mwisho wa muda wa utekelezaji wa Mpango.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na aibu ambayo Serikali
iliipata kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango huo kwa kushindwa
kutekeleza utaratibu iliyojiwekea yenyewe
wa kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya ndani kugharamia mpango wa
Maendeleo; safari hii Serikali imefuta utaratibu huo katika Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21).
Mheshimiwa
Spika, tafsiri rahisi ya uamuzi wa
Serikali hii ya CCM inayojinasibu kwa kauli ya “hapa kazi tu” kufuta msingi wa kibajeti wa kugharamia mpango wa
maendeleo kwa kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani ni hofu ya kushindwa
kutekeleza commitment hiyo kama ambavyo ilishindwa kufanya hivyo katika Mpango
uliomaliza muda wake lakini pia ni kukwepa kuwajibika au kuwajibishwa na Bunge
kwa hofu hiyo hiyo ya kushindwa kutekeleza. Kwa hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inadhani ni bora Serikali hii ikakubali uhalisia kwamba imetawaliwa na hofu tu na sio kazi tu
kwa kuwa inakimbia kivuli chake yenyewe.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa ibara ya 63(3)(c) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza kwamba: “Kwa
madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake, Bunge laweza; kujadili na
kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa
katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria
ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo; hivyo basi, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleta Muswada wa Sheria ya Utekelezaji
wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaopendekezwa kabla ya kupitishwa na Bunge.
Aidha; Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Muswada huo uitake Serikali
kutenga asilimia 40 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, suala la kutuga sheria ya kutekeleza
Mpango huu sio ushauri wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – ni takwa la
kikatiba. Ikiwa Serikali hii itapuuzia
jambo hili basi ijulikane na iingie kwenye rekodi kwamba Serikali imevunja
Katiba ya Nchi.
Mheshimiwa
Spika imebidi sasa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni ichukue jukumu la kusimamia misingi ya Katiba ili Serikali hii
isiendelee na tabia yake ya kuwa na ndimi mbili katika jambo moja. Nasema hivi
kwa sababu; Serikali hii imekuwa na historia ya kulidanganya bunge, na kwa kuwa
wanajivunia wingi wa wabunge CCM basi mambo yamekuwa yakipitishwa kiholela bila
kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria za Nchi na hata Kanuni za Bunge. Kwa
mfano; Serikali imesema katika Mpango wake wa Maendelo wa 2016/17 kwamba
imetenga shilingi trilioni 11.82 sawa
na asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo;
lakini ukisoma kitabu cha Matumizi ya Fedha za Maendeleo (Public Expenditure
Estimates Development Votes) VOLUME IV, fedha zilizotengwa ni shilingi trilioni 10.511.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inapokuwa na tarakimu
tofauti katika suala nyeti kama hili la Bajeti ya Serikali, tunapata mashaka
makubwa sana na weledi wa watendaji wa Serikali akiwemo kiongozi wao mkuu. Katika hali kama hiyo, ni lazima kuwa
na sheria itakayotoa mwongozo kwa Serikali juu ya utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo ambao unatumia fedha za umma.
3.2.
Mpango
wa Taifa wa Maendeleo na Agenda 2030 ya
Dunia ya Maendeleo Endelevu
Mheshimiwa Spika, tarehe
25 Septemba, 2015 Dunia iliingia mkataba wa kutekeleza malengo 17 ya agenda
2030 ya kuibadilisha Dunia na kuwa mahali salama zaidi pa kuishi kwa kuweka
malengo ya kuwa na maendeleo endelevu. Malengo hayo ni kama ifutavyo:
Lengo Na. 1. Kuondoa umasikini wa aina zote
Lengo Na. 2. Kuwa na kilimo endelevu, Kuondoa njaa na kuwa
na uhakika wa
chakula na lishe bora kwa watanzania wote.
Lengo Na. 3.
Kuhakikisha kuwa jamii ya rika zote inakuwa na afya bora.
Lengo Na. 4. Kuhakikisha fursa ya elimu bora na iliyo shirikishi
kwa watanzania wote.
Lengo Na. 5. Kutoa
usawa kwa jinsia zote na kuwawezesha akina mama na wasichana wote.
Lengo Na. 6.
Kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa watanzania wote.
Lengo Na.7. Kuwa na
uhakika wa upatikanaji wa nishati endelevu na ya kisasa kwa wote.
Lengo Na. 8. Kukuza ajira endelevu na zenye staha na
ukuaji wa uchumi shirikishi.
Lengo Na. 9.
Kujenga miundombinu bora na shirikishi ili viwanda viwe endelevu kwa kupokea mabadiliko
yoyote.
Lengo Na. 10.
Kupunguza tofauti za ndani na baina ya mataifa kwa walionacho na wasio nacho.
Lengo Na. 11.
Kufanya miji yetu na makazi shirikishi, endelevu na salama.
Lengo Na. 12.
Kuhakikisha uzalishaji endelevu utakaoendana na matumizi.
Lengo Na. 13.
Kuchukua hatua za haraka kukabiliana na
mabadiliko ya tabia nchi.
Lengo Na.14.
Kutunza na matumizi endelevu kwa maendeleo ya rasilimali za baharini.
Lengo Na.15.
Kulinda na kuwa na matumizi endelevu ya ‘terrestrial ecosystem’, kutunza
misitu na kupambana na ukame na kurudisha uhalisia wa ardhi.
Lengo Na.16. Kuwa na taasisi imara ili kuwa na haki na
amani,
Lengo Na.17.
Kuimarisha ushiriki wa pamoja katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo
endelevu.
Mheshimiwa
Spika, Kwa kuwa Tanzania
ni sehemu ya dunia, na kwa kuwa Tanzania haiwezi kusimama peke yake na
kufanikiwa katika kufikia malengo yake ya maendeleo kama haishirikiani na
mataifa mengine, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza
Bunge hili imetekeleza kwa kiwango gani agenda ya Dunia ya 2030 kuhusu malengo
ya maendeleo endelevu?
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa malengo
yote 17 ya maendeleo endelevu ya dunia ni muhimu kwa nchi yetu, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kutoa mchanganuo wa kina wa jinsi kila lengo
lilivyotekelezwa na kiwango cha utekelezaji (asilimia) kwa kila lengo. Aidha, tunaitaka
Serikali kutoa majibu ya ziada na ya kipekee ya namna ilivyotekeleza lengo la
16 la Kuwa na Taasisi imara ili kuwa na Haki na Amani.
Mheshimiwa Spika, Tumeweka msisitizo katika lengo hili kwa kuwa haki inaleta
amani na amani ni tunda la Maendeleo. Kwa hali ilivyo sasa hapa nchini, kuna
dalili zote kwamba taasisi zetu haziko imara jambo ambalo linafifisha jitihda
za kuwa na haki na amani katika nchi yetu. Kama taasisi zetu hasa za kutoa haki
zingekuwa imara ni dhahiri Zanzibar kusingekuwa na hitajio la uchaguzi wa
marudio. Jambo hilo linatia mashaka kama Tanzania tutaweza kukidhi malengo
endelevu ya maendeleo kama Agenda 2030 ya Dunia inavyohitaji.
4. UCHUMI WA VIWANDA
Mheshimiwa Spika, kwa
nchi yoyote Duniani ambayo uchumi wake unaendelea kukua ni dhahiri kuwa sekta
ya viwanda inakua kwa kasi inayoridhisha
na sekta hiyo ina uhusiano wa moja kwa moja na sekta zinazotoa malighafi
kwa sekta ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, Kuwa
na uchumi wa kipato cha kati kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda ni lazima kama
nchi iwe na malengo ambayo yako wazi kuhusu aina ya sekta zitakazowekezwa ili
iwe chachu ya kututoa hapa tulipokwama kwa kipindi chote. Ili malengo yawe wazi
ni lazima kuangalia mazingira yetu ya ndani na mazingira ya nje ambayo kwa njia
moja au nyingine yana uhusiano wa moja kwa moja na uzalishaji wa viwandani.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaposema malengo yaende sambamba na mkakati mzuri wa
utekelezaji, ni kwamba utakapo chagua viwanda viwe katika sekta kama: bidhaa za
kilimo, mifugo, uvuvi, madini, kemikali, misitu na/au huduma; nk. Ni lazima ujenzi
wa viwanda kufuatana na sekta tajwa hapo juu uhitaji upembuzi yakinifu wa hali
ya juu hadi kufikia maamuzi ya wapi viwanda hivyo vijengwe kwa kulingana na
kiwango cha rasilimali zilizopo na kiwanda kitakachojengwa ni kwa muda gani
kitaweza kurudisha mtaji na ajira kiasi gani zitazalishwa. Na pia kuangalia
nchi za jirani zina kiwanda kama hicho na uwezo wake wa kuzalisha bidhaa na ubora
wa bidhaa zake ukoje (uhimili wa ushindani wa bidhaa). Je, aina ya teknolojia
itakayotumika kuzalisha bidhaa itaweza kutumiwa na wananchi wetu (rasilimali
watu ya hapa hapa ndani ya nchi) au kitakuwa tegemezi kwa wataalamu wa nje?.
Mheshimiwa Spika, Mojawapo
ya malengo ni kuhakikisha yanakidhi mahitaji ya ndani kwa bidhaa
zinazozalishwa, kuwa soko la malighafi ya bidhaa za kilimo, mifugo, uvuvi,
misitu na madini kwa kuwa nguzo kuu ya mnyororo wa thamani, kwa kuubadili mfumo
wa uchumi ambao ulikuwa tegemezi kwa sekta za kilimo, madini na huduma na kuwa
uchumi tegemezi kwa sekta ya viwanda. Pia kuwezesha bidhaa zinazozalishwa kuwa
shindani katika soko la Afrika ya Mashariki na soko la nchi za Kusini mwa
Afrika[1].
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inasema ili kuwa kweli nchi yenye uchumi wa viwanda na hivyo
kupelekea kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati, tuna hitaji mkakati mzuri na
utekelezaji wake wa kutufikisha huko na sio matamanio na mahubiri tu, kama
yanavyotolewa na viongozi wetu.Viwanda siyo tu vinakuza uchumi kwa kuongezea
bidhaa thamani bali pia vinatengeneza ajira nyingi kwa haraka na kwa sekta
nyingine.
Mheshimiwa
Spika, Kwa kuwa mwaka huu
wa bajeti 2016/17 ni mwaka wa kwanza kwa awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo
wa 2025, japokuwa ni mwendelezo wa awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo,
hivyo basi ni muhimu kuangalia uwekezaji ambao tayari umefanyika katika sekta
nzima ya uzalishaji.
Mheshimiwa
Spika, Serikali kwa
kushirikiana na Serikali ya China wameanzisha kituo cha Biashara kwa ajili ya
bidhaa toka China (Kurasini Logistic Center) ambapo hadi sasa Tanzania
imekwishatoa shilingi 65,279,464,100/-ambazo ni sawa na
Asilimia 72% ya fedha zilizotakiwa
kutolewa na Serikali kwa ajili ya fidia kwa wakazi wa kurasini.
Mheshimiwa
Spika, dhana nzima ya
uwekezaji wa pamoja katika kuanzisha Kituo hiki, kwamba bidhaa mbalimbali toka
China zitakuwa zinaletwa hapo na wafanyabiashara wa nchi za Afrika ya mashariki
na zile za Kusini mwa Afrika badala ya kwenda China kufuata bidhaa, basi
watakuwa wanapata bidhaa zote Dar es Salaam. Kambi Rasmi ya Upinzani
inasema kwamba uwekezaji uliokwishafanywa
na unaoendelea kufanywa katika kuanzisha kituo hicho ni dhahiri kwamba
unapingana na dhana nzima ya awamu ya pili ya Mpango wa maendeleo wa 2025 kuwa
ni kuifanya nchi kuwa na uchumi wa viwanda.
4.1.
SEKTA
YA NYUMBA NA UKUAJI WA UCHUMI
Mheshimiwa Spika,
itakumbukwa kuwa mwaka 2011, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe.
Freeman Mbowe (Mb) akiwasilisha Bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu
bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alipendekeza kuwa pamoja na mambo mengine kuna
ulazima kama taifa kuwa na mamlaka udhibiti wa sekta ya nyumba (Real Estate
Regulatory Authority) itakayokuwa na jukumu la kusimamia sekta ya nyumba nchini
hasa majengo makubwa ili kuwa chanzo cha mapato ya serikali.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na pendekezo hilo kutolewa wakati huo serikali wakati wa bajeti ya
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imependekeza mwaka ujao wa fedha
2016/2017 imeahidi kuleta Bungeni muswada wa sheria ambayo itasimamia sekta ya
nyumba nchini. Ni msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa pendekezo
hili limechelewa sana. Kama serikali ingelitekeleza jambo hili mapema, serikali
ingelipata chanzo cha mapato.
Mheshimiwa Spika,
majirani zetu wa Kenya ndani ya jumuiya ya Afrika ya Mashariki, sekta ya nyumba
imechangia pato la taifa kwa 10.6% sekta hiyo ikiwa ya nne katika kuchangia
katika uchumi wa nchi hiyo. Aidha athari
za kuanguka kwa bei ya mafuta duniani haijaathiri uchumi wa Dubai kwa sababu ya
kuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya nyumba.
Mheshimiwa Spika,
tamwimu zinaonesha kuwa Tanzania kuna uhitaji wa nyumba 200,000 kila mwaka na
uhaba wa nyumba milioni 3. Hii ni kutokana na ongezeko la kasi la idadi ya watu
nchini pamoja na uhitaji wa nyumba zenye hadhi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona
kuwa serikali haijawa na mkakati madhubuti wa kuhakikisha tunatumia fursa ya
sekta ya makazi kukuza uchumi wa nchi yetu kama ambavyo mataifa mengine
yamepiga hatua kubwa kwa kutumia fursa
hiyo.
4.2 KODI YA MAJENGO (PROPERTY TAX)
Mheshimiwa Spika, kwa
miaka mingi kodi ya majengo ilikuwa ikikusanywa na halmashauri, lakini kwa sasa
serikali imeamua kodi hiyo ikusanywe na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kupelekwa
Hazina. Agizo hili litaathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri zetu
nchini kwa kuwa kodi ya majengo ilikuwa chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri
hasa za Miji, Manispaa na Majiji.
Mheshimiwa Spika, ieleweke
kuwa kama fedha zitakusanywa na Hazina na kama utaratibu wa kutoa fedha hizo
kwenda Halmashauri utaendelea kama ilivyo sasa ambapo fedha za maendeleo kutoka
Serikali Kuu zinachelewa kupelekwa kwenye Halmashauri basi tusitegemee kuwa
fedha za kodi ya majengo zitanuifaisha tena Halmashauri zetu.
Dhana
hii ni kutokana na ukweli halisi ambao upo kwenye kodi ya ardhi ambayo ilikuwa
inakusanywa na Halmashauri na kuwasilishwa Wizara ya Ardhi ilionyesha wazi kuwa
ikishafika wizarani ilikuwa vigumu sana kurejeshwa kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Hii
ni kutokana na sababu kuwa serikali mara nyingi imekuwa ikipeleka fedha
Halmashuri katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha. Ni rai ya Kambi Rasmi ya
Upinzani kuwa serikali itafikiria upya uamuzi huu ambao utapunguza sana mapato
ya Halmashauri zetu na kuzifanya kushindwa kutoa huduma kwa wananchi wake.
4.3
SEKTA
YA UTALII
Mheshimiwa Spika, sekta
ya utalii ni sekta ambayo inachangia fedha za kigeni katika sekta nzima ya
uchumi (foreign exchange earner), kwa
kuwa na watalii milioni moja wanaochangia asilimia 17.7 ya pato la Taifa (GDP).
Kwa mujibu wa takwimu za nchi nzuri duniani[2]
ni kwamba; Tanzania ni namba 8 kati ya mataifa 20 yenye vivutio vizuri na vingi
Duniani kwa ajili ya watalii. Lakini kuwa na vivutio vingi sio sababu ya kuwa
na watalii wengi, ila sababu kubwa ni jinsi gani unajitangaza na unawavutia
vipi watalii? Takwimu zinaonesha kuwa Ufaransa ndiyo nchi inayoongoza kuwa na
watalii milioni 83.77 kwa mwaka wakati katika zile nchi 20 haimo. Afrika ya
Kusini inapokea watalii 9,616,964[3]
kwa mwaka, lakini katika orodha inachukua namba 1, Kenya ambayo ilikuwa
imefikisha watalii milioni 1.7 kabla ya tishio la ugaidi, sasa inatarajia
watalii milioni 1.6, Uganda inapokea watalii 1,266,000 kwa mwaka, Zimbabwe inapokea
watalii 1,905,000 na Msumbiji 1,661,000[4]
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kama tutaweza kuongeza idadi ya watalii hata
kufikia milioni 5 kwa mwaka ni dhahiri uchumi wa Tanzania unaweza kuendeshwa na
sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, Ili
Tanzania iweze kupata watalii milioni 5 kwa mwaka, Kambi Rasmi ya Upinzani
inashauri kwamba Serikali iimarishe kwanza usafiri wa anga. Hali ilivyo sasa, watalii wanapata tabu sana
kufika Tanzania kutokana na gharama kubwa inayosababishwa na kutokuwepo usafiri
wa uhakika wa ndege. Tunashauri kwamba Serikali iweke mkakati mahususi wa kuwashawishi
marafiki zetu wa China ili shirika lao la ndege lianzishe safari za kuja
Tanzania, na vile vile mashirika ya ndege toka Marekani kuwa na safari za
Tanzania kila wiki. Pili, tozo katika
viwanja vyetu vya ndege zipunguzwe ili kuvutia watalii. Tatu huduma
zinazotolewa kwa watalii huko mbugani ziboreshwe na kuwa na kiwango cha
kimataifa ili kuwavutia watalii zaidi.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na misimamo ya Serikali isiyokuwa ya kibiashara ni kwamba utalii kuwa
na faida sana inategemea na idadi ya watalii wanaoingia, hivyo kama Serikali
itakubali kuwa kipindi kisichokuwa cha msimu wa utalii ni vyema bei zikashuka
ili idadi ya watalii na siku za kukaa nchini iongezeke. Kambi Rasmi ya Upinzani
inasema kuja kwa watalii kuna wanufaisha watu wengi sana mbali ya Serikali kupata mgawo
wake, ni muda mwafaka sasa Serikali kuwa-“flexible”
ili kuwa kibiashara zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Tunaitaka Serikali kutumia mfano wa jirani zetu Kenya, ambapo Rais Uhuru Kenyatta amefuta tozo za
kutua kwa ndege zote za kukodi zitakazokuwa zinaleta watalii nchini Kenya[5].
5. VITUO VYA KUUZA
UTALII WA TANZANIA NJE
Mheshimiwa Spika,
Bodi ya Utalii imekuwa ikitumia fedha nyingi
kwa muda mfupi wakati wa maonyesho mbalimbali ya utalii yanayofanyika
nje ya nchi. Ili kuwe na ujio endelevu
wa watalii nchini, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali iweke
vituo vya utangazaji wa utalii wetu katika balozi zetu katika nchi za Marekani,
Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia,Uchina, Japani, Canada na nchi za Scandinavia na kuwe na watumishi maalumu
watakaoajiriwa katika vituo hivyo kwa kazi maalum ya kuhakikisha kuwa
wanatangaza vivutio vyetu na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja hapa nchini.
Mkakati huo ukifanikiwa ni dhahiri kwa mwaka mmoja tunaweza kupokea watalii
zaidi ya milioni tano.
Mheshimiwa Spika,
fursa hii si kila mtu anaweza kuiona, hivyo ni muda muafaka kuwashawishi
wachina wawekeze katika hoteli za kitalii, badala ya wawekezaji hao kushindana
na watanzania katika maduka ya vifaa vya ujenzi pekee. Kwa njia hii tutaweza kuvuta soko la watalii
wengi toka China.
6.0 SERIKALI YA HAPA KAZI TU, IMELETA BAJETI HEWA BUNGENI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ni wajibu wa Bunge kupanga na kuidhinisha mapato na matumizi ya serikali kila mwaka wa fedha .Hii ni kwa mujibu wa ibara ya 137(1)’Rais atatoa maagizo kwa watu wanaohusika kwamba watengeneze na kuwasilisha kwenye Bunge katika kila mwaka wa fedha wa Serikali, makadirio ya ‘Mapato na Matumizi’ ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha mwaka wa fedha unaofuata’
Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2016/17 serikali imewasilisha bajeti hewa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, ninasema kuwa serikali hii imeleta bajeti hewa hapa Bungeni na nitathibitisha maoni yangu haya kama ifuatavyo;
1. Kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato ya serikali katika mwaka huu wa fedha volume 1 ‘Financial Statements and Revenue estimates’ for the year 1st July ,2016 to 30th June 2017 kilicholetwa hapa Bungeni kinaonyesha kuwa mapato yote ya serikali yaani mapato ya kodi , yasiyokuwa ya kodi ,mikopo na misaada ya kibajeti itakuwa jumla ya shilingi Trilioni 22.063.
Mheshimiwa Spika, upatikananji wa mapato hayo ni kama ifuatavyo;
i. Mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali ni shilingi Trilioni 17.797
ii. Mapato yasiyokuwa ya kodi ni shilingi Bilioni 665.664
iii. Mikopo na misaada ya kibajeti ni shilingi Trilioni 3.600
Mheshimiwa Spika, ni muhimu Waheshimiwa Wabunge wakatambua kwamba Serikali hii haijaonyesha chanzo kingine kipya cha mapato ambacho hakijathibitishwa na au kupitishwa na Bunge hili kwa mujibu wa katiba na ijulikane pia kuwa Bunge halipitishi kitabu cha hotuba ya waziri bali hupitisha mafungu yaliyopo kwenye vitabu vya bajeti ya serikali.
2. Kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya kawaida ,volume II Estimates of Public Expenditure Consolidated Fund Services for the year 1st July ,2016 to 30th June, 2017 na kitabu cha Maendeleo, Volume IV Public Expenditure Estimates Development Votes (part A) kama vilivyowasilishwa Bungeni , tayari bunge limeshaidhinisha matumizi ya jumla ya shilingi Trilioni 23.847
Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:
i. Fedha za Matumizi ya Kawaida (Volume II) shilingi 13,336,042,030,510
ii. Fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo (Volume IV) shilingi 10,511,945,288,575
3. Ukichukua kitabu cha Mapato ya Serikali (Revenue Book Volume I) utaona kuwa
jumla ya mapato yote ya serikali ni shilingi Trilioni 22.063 , ila serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi Trilioni 23.847 ambacho ni kiasi
tofauti na Mapato ambayo serikali imepanga kukusanya na tofauti yake ni kuwa
kuna nakisi ya shilingi Trilioni 1.783
jambo ambalo linaifanya bajeti hii kukosa uhalali kwani nakisi hii ni kubwa
sana.
4. Kwa mujibu wa maelezo ya waziri wa fedha
‘Mapendekezo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kwenye
mkutano wa wabunge wote katika ukumbi wa JNICC’ mnamo tarehe 06 Aprili, 2016
pamoja na maelezo ya hotuba yake aliyoyatoa hapa Bungeni uk. 91 ameendelea
kulidanganya Bunge na Dunia kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali ina bajeti
ya kiasi cha shilingi Trilioni 29.539
5. Hotuba ya waziri wa fedha katika ukurasa wa 92
‘Mfumo wa Bajeti wa Mwaka 2016/17’ inaonyesha kuwa kiasi cha shilingi trilioni
7.475 ni mikopo ya ndani yenye masharti ya kibiashara. Fedha hizi kwenye kitabu
cha mapato hazipo na pia hazionekani zitakopwa kutoka Benki gani kama ambavyo
mikopo ya nje yote imeonyeshwa kwenye kitabu cha mapato na hata kwenye kitabu
cha miradi ya maendeleo hazionekani kwenye kutekeleza mradi wowote ule na hivyo
ni sahihi kusema kuwa ni fedha hewa , maana hazina hata kasma yake na Bunge
hili tunapitisha kasma .
6. Hotuba ya waziri wa fedha uk.58 anasema kuwa moja
ya chanzo chake cha mapato ni pamoja na kurekebisha sheria ya Kodi ya Mapato
SURA 332 (i)’kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo
kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano.’
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu ya kina kuhusu mambo
yafuatayo;
i.
Bunge linapitisha takwimu zipi hasa? Ni kitabu cha hotuba ya waziri au
ni vitabu vya mapato na matumizi pamoja na kile cha Miradi ya maendeleo?
ii.
Fedha ambazo waziri kwenye hotuba yake anasema kuwa ni mikopo ya ndani
ya masharti ya kibiashara, zinakopwa ili kugharimia miradi ipi? Kwani tayari kitabu cha
miradi ya maendeleo VOLUME IV kimeshataja miradi yote na kiasi cha fedha ambazo
kila mradi utatumia.Hii miradi inayosemwa kuwa fedha itakopwa kwa ajili ya
miradi ya maendeleo ni miradi ipi hiyo? Mbona haijapitishwa na bunge au ni
miradi hewa?
iii.
Waziri wa fedha anaposema kuwa fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi
Trilioni 17.719 na hapo hapo anasema
kuwa tunakwenda kulipa deni la taifa kiasi cha shilingi trillion 8, mbona hizi fedha hazipo kwenye kitabu ambacho kinapitishwa
na Bunge? Kitabu cha matumizi ya kawaida VOLUME IV?
iv.
Kwa kuwa CAG anakagua kasma zilizopo kwenye vitabu yaani VOLUME IV na VOLUME
II, katika bajeti hii atakagua kasma ipi?maana fedha za kulipia deni la taifa
hazipo kwenye kitabu cha VOLUME II na hata mikopo yenye masharti ya kibiashara
inayosemwa itakopwa haipo kwenye Revenue Book
v.
Huu mkanganyiko wa vitabu vya serikali moja imesababishwa na nini au
kuna mikopo na miradi hewa? Ni kwanini kitabu cha mapato (revenue book)
kinaonyesha mapato madogo kuliko kiwango cha matumizi?
vi.
Kuingiza malipo ya kiinua mgongo cha wabunge ambacho kinatakiwa kulipwa
mwaka 2020 kwa mujibu wa sheria na kuwa chanzo cha mapato katika mwaka huu wa
fedha 2016/17 hiki si chanzo hewa? Nasema hivi kwa kuwa, kila mwaka tutakuwa
tukipitisha bajeti na hiki kilipaswa kuwa chanzo ifikapo mwaka 2020 ambapo ndio
kiinua mgongo hiki kinalipwa na ndio kingekuwa chanzo cha mapato au serikali
imepanga kulipa kiinua mgongo hicho kila mwaka wa fedha?
Mwisho Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, tunaitaka serikali iwasilishe Vitabu vyenye
kumbukumbu na takwimu sahihi kabla ya kulitaka Bunge hili kujadili bajeti hii
na kuamua kuipitisha au kuikataa, la sivyo Bunge litakuwa halitimizi wajibu
wake kikamilifu kwa mujibu wa katiba ya Nchi yetu.
7. WIZARA YA FEDHA NA JUKUMU LA UTEKELEZAJI MPANGO WA KWANZA WA TAIFA WA
MIAKA MITANO 2011/12-2015/16
Mheshimiwa Spika, Mpango huu ni wa kwanza kati ya
mipango mitatu ya miaka mitano mitano inayotumika kama chombo katika dhamira ya kuongeza
kasi ya utekelezaji wa Mpango wa
Taifa wa maendeleo wa miaka ishirini na mitano (Tanzania Development vision(TDV)-2025).
Malengo yakiwa ni Tanzania iwe ya kipato cha kati ifikapo 2025 ambayo pamoja na
mambo mengine litakuwa taifa lenye:
i)
Kiwango cha juu cha mapinduzi ya viwanda
ii)
Ushindani na hali nzuri/bora ya maisha kwa wananchi wake
iii)
Utawala wa sheria
iv)
Jamii ya wasomi waliobobea
Vipaumbele vya msingi (Core Priorities) katika
mpango huo ni :
i)
Miundombinu / Infrastructure
ii)
Viwanda / industry
iii)
Maendeleo ya rasilimali watu /human capital development
iv)
Nishati
Mheshimiwa Spika, tuangalie mafanikio ya wizara ya fedha katika utekelezaji wa jukumu
lake la kusimamia utekelezaji wa mpango wa miaka mitano 2011/12- 2015/16.
1)
Reli- mpango ulipanga kukarabati KM
2,707 ya reli ya kati, imefanikiwa
kukarabati km 150 tu za Reli
2)
Barabara – Kujenga na kukarabati km 5,204 za barabara. Zimejengwa
km 2,775
3)
Nishati- Ongeza uzalishaji wa umeme kufikia 2,780 MW. Sasa hivi tunazalisha MW 1,461
4)
Kilimo - Ukuaji wa mwaka
kwa 6%, ukuaji kwa sasa 3.2% (ukuaji huu ni wa kipindi chote toka
tupate uhuru….).Kiwango cha umwagiliaji
toka 345,690 – 1,000,000.
Matarajio yalikuwa ni kuongeza eneo jipya la umwagiliaji lenye ukubwa wa hekari
645,690. Mafanikio ni nyongeza
ya hekari 115,656 tu!
5)
Maendeleo ya viwanda na uzalishaji – kukua kwa 11%.
Mafanikio ni ukuaji wa 6.6%
6)
Elimu - Nyongeza kada ya wasomi wa kiwango cha juu toka
2.7% mpaka 4.3% ifikapo 2015. Idadi
imepungua mpaka 2.5%. Halikadhalika
kuongeza kada ya wasomi wa kiwango cha kati toka 13.6% mpaka 17.8% ifikapo 2015.Imeongezeka kwa 1% tu
kufikia 2015.
Mheshimiwa Spika, Hakuna ubishi kwamba tukiwa tunaelekea katika mpango wa pili wa miaka
mitano, wizara ya fedha imeshindwa kutekeleza wajibu huu kikamilifu, hali hii
inatia mashaka ufanisi wa utekelezaji wa mpango wa pili, wakati mpango wa
kwanza umeisha kwa kusuasua!
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze
Bunge hili tukufu, Ni kwa namna gani serikali imejipanga kuweza kufidia ombwe
hili!ili miaka tisa ijayo Tanzania liwe Taifa lenye mapinduzi ya viwanda ya
hali ya juu, hali bora ya maisha kwa wananchi wake, utawala bora na Taifa lenye wasomi waliobobea (Rejea taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma
na Maendeleo ya jamii)ambayo
ilitamka bayana kwamba hali ya
elimu nchini ni hatari kwa usalama wa
Taifa. Ninukuu maneno ya kamati ‘Taifa letu limejenga mfumo wa elimu ambayo
haikidhi DIRA na Mahitaji ya Nchi’.[6]
7.1
UPATIKANAJI FEDHA KUTOKA HAZINA
a) Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi: Hadi
kufikia Machi 2016 ,wizara ilikuwa imepokea shilingi 660,333,375,957/- kati ya shilingi 816,080,198,000 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo . Kati ya fedha zote zilizopokelewa kwa ajili ya matumizi ya Wizara, mishahara
ilikuwa 52%, matumizi mengineyo ilikuwa 47% na kwa upande wa bajeti ya
maendeleo ni 1% tu.[7]
b) Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa: kwa
miradi ya maendeleo iliidhinishiwa shilingi bilioni 232.1. Mpaka Februari, 2016
Wizara ilipokea shilingi bilioni 40 tu,
sawa na asilimia 17.2 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.
c) Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto: Bajeti ya maendeleo iliyotengwa 2015/16 ni bilioni 440.6, mpaka mwezi machi ikiwa ni
robo ya tatu ya mwaka hakuna fungu hata moja ambalo wizara hiyo ilikuwa imepata
zilizoidhinishwa na Bunge kwa angalau
50%. Halikadhalika Fungu 52 – Idara kuu Afya hadi kufikia tarehe 31 March 2016 kiasi cha fedha
kilichopokelewa ni 31% tu ya Bajeti ,
halikadhalika fungu 53 kwa Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii jinsia na watoto.
d) Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi: Katika kipindi cha mwaka 2015/16 wizara ilitengewa jumla ya shilingi
213,079,803,000/- kati ya fedha hizo 32,713,073,000 ilikuwa ni fedha za maendeleo. Hadi kufikia Machi 2016 ,
fedha za maendeleo zilizokuwa zimepatikana ni
bilioni 5.1 ambazo ni sawa na
15.9% tu ya bajeti iliyoidhinishwa na
Bunge.
Mheshimiwa Spika, ikubukwe kwamba; Mpango wa kwanza wa miaka mitano (FYDP 1) uliweka
malengo ya kibajeti katika sekta ya
kilimo (miaka mitatu ya mwanzo) ya shillingi za kitanzania Bilioni 2,710.65 (Trillion 2.7). (ambayo
ingewezesha kilimo kukua toka 3.2% ya sasa mpaka 6%). Fedha iliyokuja kutolewa kwa kipindi chote
hicho ni shilingi 250.12 billioni sawa na 9.23% ya mahitaji.
e) Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi: Wizara iliidhinishiwa shilingi 511,525,227,000
kwa ajili ya matumizi ya kawaida . Hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka, yaani
Machi 2016 Wizara ilikuwa imepokea kiasi
cha shilingi 316,402,868 ,828.00 sawa na 68%. Kuhusu bajeti ya maendeleo,
wizara imepokea jumla ya shilingi 360,922,754,359.61 sawa na 61.9% ya fedha
iliyoidhinishwa 582,670,597,884.49. Bodi
ya mkopo ambayo ni sehemu muhimu sana ya
wizara hii kupitia fungu 46 iliidhinishiwa
shilingi 418,300,000,000 kwa ajili
ya Mradi Namba PT 4340 uliojulikana kama Higher Education Students
Loans ambao ni mradi wa kutoa
Mikopo. Hadi kufikia tarehe 15 Machi ,2016
Bodi ilikuwa imepokea jumla ya shilingi bilioni 245 sawa na asilimia 55.9% tu ya
bajeti iliyoidhinishwa na Bunge . Fedha hizo zingetolewa zote kwa 100% wanafunzi wengi zaidi wangepata
mikopo.
f) Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano: Wizara hii ni miongoni mwa wizara (chache sana)
zilizopata fedha zilizopangwa katika
bajeti na zaidi, hususan katika sekta ya ujenzi (barabara). Katika mwaka wa
fedha 2015/16. Sekta hii ilitengewa shilingi
883,832,338,500/- kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi ya maendeleo . Kati ya
hizo, fedha za ndani kutoka mfuko mkuu wa hazina wa serikali ni shilingi
191,619,568,500 na shilingi
85,572,770,000 zilikuwa fedha za
nje. Kwa upande wa fedha za mfuko wa barabara zilitengwa shilingi
606,640,000,000. Hadi Aprili, 2016 fedha zilizotolewa ni shilingi 1.080,804,942,594. Kati ya fedha
hizo shilingi 607,350,007,730 ni fedha za ndani kutoka mfuko mkuu wa
hazina/serikali (Ongezeko la shilingi
415,730,439,230) ,shilingi 149,502,934,864 ni fedha za nje na shilingi
323,952,000,000 ni fedha za mfuko
wa barabara. Sehemu kubwa ya fedha za ndani
zilizotolewa imetumika kulipa
madeni ya Makandarasi na wahandisi
washauri wa miradi ya barabara.[8]
Mheshimiwa Spika, Licha ya mabilioni yanayotumika kujenga barabara na kulipa madeni yenye
riba kubwa sana kutokana na serikali kuchelewa
kulipa madeni ya barabara, wakati
kamati ikikagua miradi mbali mbali ya barabara
nchini imebaini kuwepo kwa changamoto ya kuharibika
kwa barabara mapema mara baada ya
barabara kujengwa![9]
Licha ya visingizio vilivyotolewa vya uharibifu huo, sababu hizo hazina mashiko
/msingi wa kuhalalisha upotevu huo wa mabilioni ya fedha. Barabara zote hizi
lazima zifanyiwe ukaguzi wa kitaalam ili kujiridhisha na thamani ya fedha na
kazi iliyofanywa. Hii inatokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu sana (tokea
kipindi ambacho Rais alikuwa waziri wa miundombinu) Wizara hii imekuwa
ikihusishwa na uchakachuaji katika ujenzi wa barabara.
g) Wizara ya Nishati na Madini: Wizara hii nayo ilipata fedha kuliko kiasi
kilichotengwa kwenye bajeti.Katika mwaka wa fedha 2015/16. Wizara
iliidhinishiwa na Bunge Jumla ya Shilingi bilioni 642.12. Kati ya fedha
hizo shilingi bilioni 502.30 sawa na 78%
ya bajeti yote ilikuwa kwa miradi ya maendeleo na shlingi 139.82 sawa na 22%
zikiwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida .Hata hivyo bajeti
iliongezeka kutoka bilioni
642.12 mpaka bilioni 762.12 (Nyongeza ya
bilioni 120.12)
Mheshimiwa Spika, Licha ya nyongeza hiyo, miradi ya REA
inayogharimiwa na fedha za Mfuko wa Nishati Vijijini
ambao vyanzo vyake vya mapato ni
pamoja na tozo ya shilingi 100
katika kila lita ya mafuta ya
petrol na Dizeli; na shilingi 150 katika kila lita ya mafuta ya taa bado inasua sua. Hii inatokana na fedha ambazo
wananchi wanatozwa katika mafuta tajwa hapo juu kwa makusudi ya kupeleka huduma
ya UMEME vijijini kutumika kwa matumizi mengine yasiyokusudiwa! Licha ya fedha
hizo kuwa zimewekewa wigo kisheria (Ring Fenced). Takwimu zinaonyesha kwamba tangu tozo hizi zilipoanza kukusanywa Julai 2013 mpaka Machi 2016, fedha
zilizopatikana toka kwenye tozo ya
petrol na Dizeli ni shilingi bilioni 493.8,
Mafuta ya taa shilingi bilioni 448.5 na shilingi bilioni 45.4 kutoka kwenye ‘Custom Processing Fee’. Licha ya makusanyo ya shilingi bilioni 987.7 (tozo ya
petrol na dizeli) kiasi kilichopelekwa kwenye umeme vijijini mpaka mwezi April 2016 ni shilingi bilioni 366.95 tu sawa na 37.15%
ya makusanyo yote. Katika mazingira kama haya, kamwe serikali ya CCM haiwezi
kujitapa imetekeleza wajibu wake kikamilifu. Kwa lugha nyepesi imewaibia
mamilioni ya wananchi wanaoishi vijijini
ambao mfuko huu uliundwa mahususi kwa ajili ya kusogeza huduma za umeme kwao.
Ikumbukwe hii fedha sio ya hisani bali ni fedha ya nyongeza iliyoongezwa kwa
kila lita inayonunuliwa na wananchi kwenye mafuta ya taa, petrol au dizeli.
h) Wizara ya Maliasili na Utalii: Katika mwaka wa fedha 2015/16 wizara ya maliasili na utalii iliidhinishiwa jumla ya shilingi 66,313,757,000 kwa ajili ya
matumizi ya kawaida . Kati ya fedha hizo
shilingi 45,235,955,000 zilikuwa
ni kwa ajili ya matumizi mishahara na shilingi 21,077,802,000 kwa
ajili ya matumizi mengineyo. Mpaka Machi
2016, wizara ilipokea 43,487,894,012.34
sawa na 65.5% ya bajeti iliyoidhinishwa ambapo 32,714,043,166.18 ikiwa ni
mishahara na 10,773,850,856 ni kwa matumizi mengineyo. Fedha iliyoidhinishwa
kwa miradi ya maendeleo ni 7,709,150,000/= . Fedha zilizotolewa ni bilioni 1 na
yenyewe ni fedha ya NJE sawa na asilimia 12.9 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kutokana
na hali hiyo katika miradi 10 ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa hakuna hata
mradi mmoja uliotekelezwa kwa ufanisi.[10]
i) Wizara ya Viwanda na Biashara: Katika mwaka 2015/16 Wizara ilitengewa jumla ya shilingi 87,470,349,000 ambapo 52,082,968,000
zilikuwa ni matumizi ya kawaida (mishahara na matumizi mengineyo) na shilingi 35,387,381,000/- za matumizi ya maendeleo (shilingi
26,588,200,000 ni fedha za ndani na
shilingi 8,799,181,000 ni fedha za
nje). Mpaka mwezi Machi 2016 Wizara
ilipokea 29,752,487,320/- sawa na 34% ya fedha iliyotengwa. Kati ya fedha hiyo
fedha za maendeleo zilizotolewa ni 1,602,111,662 tu ambayo ni fedha za nje! Kwa
lugha nyingine fedha za ndani za maendeleo zilizotoka ni 0%, na fedha ya nje
iliyotoka ni 18% tu! [11]
j) Wizara ya Fedha na Mipango
Mheshimiwa Spika, Wizara hii, licha umuhimu wake mkubwa
katika uchumi wa Tanzania katika mwaka wa fedha 2015/16, pamoja na
mafungu yake nane (8) iliidhinishwa kutumia jumla ya shilingi
7,326,769,737,771. Kati ya fedha hizo shilingi 72,659,909,000 kwa ajili ya
Mishahara (PE) Shilingi 7,218,508,850,128 kwa ajili ya Matumizi mengineyo (kati
ya hizo shilingi 6,381,430,000,000 ni
kwa ajili ya deni la Taifa). Kwa upande wa fedha za maendeleo fedha
zilizoidhinishwa ni shilingi 1,022,924,905,000 ambapo fedha za ndani zilikuwa
shilingi 651,541,992,000/- na fedha za nje 371,382,913,000. Mpaka mwezi machi 2016 wizara ilipokea fedha
za maendeleo shilingi 25,908,256,142,
sawa na 3% tu ya fedha zote
zilizoidhinishwa!
8. MWENENDO WA MAPATO YA NDANI NA MKANGANYIKO WA TAARIFA ZA SERIKALI YA
HAPA KAZI TU
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka huu wa fedha, na hususan miezi ya karibuni mwenendo wa
mapato umekuwa sio wa kuridhisha sana! Kodi ya ushuru wa forodha haikufikia
lengo na kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda hali inazidi kuwa mbaya! Idadi ya
meli zilizohudumiwa Januari - Aprili 2015 (TPA- Kontena) zilikuwa 41 ukilinganisha na
meli 16 tu zilizohudumiwa Januari- Aprili 2016. Pungufu ya meli 25, badiliko la -61%. Halikadhalika kwa
Meli ya Mzigo Mchanganyiko ‘General
Cargo’ meli zilizohudumiwa Jan- April
2015 zilikuwa 53 ukilinganisha na meli
zilizohudumiwa Jan – April 2016 ambazo
ni 33 tu. Pungufu ya meli 20 sawa na badiliko la -37%
Mheshimiwa Spika, Maelezo ya waziri wa fedha na
Mipango kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2015/16
kwa kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016 na mwelekeo hadi juni 2016[12]
anaeleza sababu za upungufu kuwa ni ;
i)
kupungua kwa uingizaji wa
mizigo kutoka nje kutokana na hofu ya wafanya biashara katika kipindi cha
uchaguzi
ii)
Udanganyifu uliokuwa unafanywa na wafanyabiashara kwa kukwepa kodi ya ushuru wa forodha kwa
bidhaa zinazopitia bandarini
iii)
kushuka kwa bei ya bidhaa
katika soko la dunia
iv)
Na kwa upande wa kodi ya ongezeko la thamani upungufu umetokana na marejesho ya VAT (VAT
inputs) kuwa kubwa kutokana na uwekezaji katika viwanda vya sementi
pamoja na kupungua kwa mahitaji.
v)
Halikadhalika tatizo la
kutoa/kuomba risiti za kielekroniki katika huduma mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Wakati wizara ya fedha ikitoa visingizio tajwa hapo juu, Mamlaka ya
usimamizi wa Bandari Tanzania katika maelezo yake ya Takwimu za uingizaji
mizigo katika Bandari ya Dar es salaam
kwa kipindi cha 2013-2015 na kipindi cha Jan- April 2016 inaeleza sababu
zilizopelekea kupungua kwa shehena ya mizigo kuwa ni:
i)
Kudorora kwa uchumi wa china
(Hii imeleta madhara katika bandari nyingi duniani)
ii)
Hofu ya wateja kutokana na kuanzishwa kwa sheria ya VAT katika huduma
zinazotolewa na mawakala kwenye mizigo
ya nchi jirani (VAT on Transit GOODS) ambayo ni kinyume na sheria za
kimataifa
iii)
Tatizo la Single customs
Territory. Mizigo inayopatikana kwa mfumo wa single customs territory
unatozwa kodi kwa asilimia 100%, baadhi ya wafanyabiashara wanaona
kupitisha mizigo Tanzania ni gharama kubwa.
iv)
Kushuka kwa bei ya shaba
duniani kumesababisha migodi mingi nchini Zambia na DRC kufungwa na hata ile
inayofanya kazi uzalishaji umepungua.
v)
Tozo la barabara (Road tolls) USD 16 kwa KM
100 hapa Tanzania ulikilinganisha na USD 8 kwa kila KM 100 zinazotozwa
kwa nchi nyingine kwa magari yenye ekseli zaidi ya mbili.
vi)
Muda mfupi (Short grace
period) kwa mzigo wa mafuta wa nchi jirani. Tanzania ni siku 30 mzigo unatakiwa
uwe umesafirishwa kabla ya kuwa localised tofauti na nchi nyingine ambazo zinawapa siku 60
hadi 70.
vii)
Kuongezeka kwa Tozo kutokana na “Government Chemical Agencies”
kutoza USD 1.00 kwa Tani badala ya USD 100 kwa “ Bill of Lading” kwa
bidhaa ambazo wanazikagua kama vile
mbolea hivyo kuongezeka kutoka wastani
wa USD 500 hadi USD 20,000 au Zaidi
kutokana na ukubwa wa mzigo.
viii)
Mfumo wa TANCIS wa TRA kutoruhusu kugawanywa kwa “Bill of Landing”
ili kuruhusu kutoa mizigo ambayo haina tatizo panapokuwa na tatizo la mzigo mmoja badala ya mzigo wote kuzuiwa na kusababisha gharama za tozo
za hifadhi kwa mteja ambazo sio
lazima.
Mheshimiwa spika, Ni aibu kubwa, kwa vyombo viwili vya serikali kuzungumza lugha tofauti
katika suala moja! Hiki ni kiashiria kwamba ama serikali hii haifanyi kazi kama
timu…ama waziri wa fedha amedhamiria kulipotosha Bunge kwa kutoa sababu nyepesi
huku zile za msingi akiziweka kibindoni (sijui kwa manufaa ya nani). Kambi
rasmi ya upinzani inaitaka Serikali ya CCM na Magufuli kutambua kwamba Tanzania
sio kisiwa na kwamba Bandari ya Dar es salaam inakabiliwa na ushindani kutoka
kwenye bandari za Mombasa (Kenya), Beira,Nacala na Maputo (Msumbiji) , Durban
(Afrika ya Kusini ), Walvis Bay (Namibia) na Lobito (Angola) kama kuna vikwazo
vyoyote vinavyoikwamisha bandari yetu na nchi kushindana katika soko la
ushindani vikwazo husika lazima vishughulikiwe mara moja. Na wizara ya fedha
iliyopewa jukumu kubwa la kusimamia uchumi wa Tanzania haiwezi kukwepa jukumu
hili.
9. UNUNUZI WA NDEGE ZA ATCL KUNA HARUFU YA UFISADI!
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa kitabu cha fedha za Maendeleo Volume IV Part A fungu 62
kasma 4294 zimetengwa jumla ya
shilingi Bilioni 500 fedha za ndani
kwa ajili ya kununua ndege za abiria kwa ajili ya shirika la Ndege la ATCL.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya waziri wa ujenzi ,uchukuzi na mawasiliano
kifungu cha 185 alisema kuwa, nanukuu ‘kazi
inayoendelea ni kukamilisha taratibu za ununuzi wa ndege mbili mwaka
2016.Wizara kwa kushirikiana na ATCL na wadau wengine imekwishaainisha ndege
zinazofaa kununuliwa baada ya kukutana na wawakilishi wa viwanda vya ndege vya
Boeing ya Marekani, Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya
Canada. Ndege mbili za awali zinazotarajiwa kununuliwa zitakuwa na uwezo wa
kubeba abiria 78 kila moja.Ndege ya tatu na ya nne zitakazonunuliwa katika
mwaka wa fedha 2016/2017 zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 155’
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango ni kwamba; serikali
imeamua kununua ndege kutoka kiwanda cha Bombadier
ya Canada na hii ni kutokana na ushauri ambao wizara ilipokea kutoka kwa
wataalam wake .Aidha tuna taarifa kuwa ndege mbili za mwanzo ambazo
zitanunuliwa sio mpya bali ni ndege ambazo tayari zilishatumika (kuukuu) kama taarifa hizi ni za kweli , Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa kwa Bunge hili sababu za kina
zilizopelekea serikali kwenda kununua ndege chakavu kinyume cha sheria ya manunuzi
ya mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti wetu kama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
tuliamua kutafuta taarifa za kina na za uhakika juu ya Bei za ndege mpya kwenye
Viwanda ambavyo serikali ilisema kuwa iliwasiliana nao na kufanya nao mazungumzo
yaani Viwanda vya ndege vya Boeing
ya Marekani, Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya Canada na na kukuta bei za
ndege mpya kuwa kama ifuatavyo;
Kiwanda cha Bombardier.
Aina ya Ndege
|
Idadi ya Viti
|
Bei (Januari 2015) Mil USD
|
Q 400
|
90
|
31.3
|
CRJ 700
|
70
|
41.0
|
CRJ 900
|
76-90
|
46.0
|
CRJ 1000
|
100
|
49.0
|
CS 100
|
100-133
|
71.8
|
CS 300
|
160
|
82.0
|
Kiwanda cha Air Bus
Aina ya Ndege
|
Idadi ya Viti
|
Bei (January 2015) Milioni USD
|
A 320
|
100-240
|
97.0
|
A 318
|
|
74.3
|
A 340
|
260-400
|
284.6
|
A 350
|
270-350
|
351.9
|
Kiwanda Cha Boeing
Aina ya Ndege
|
Idadi ya Viti
|
Bei (January 2015) Milioni USD
|
737-700
|
85-215
|
80.6
|
747-8
|
467
|
379.1
|
767-300 ER
|
181-375
|
197.1
|
787-8
|
250-290
|
224.6
|
Mheshimiwa Spika, kwa bei hizo hapo juu Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni tunataka kujua ni kwanini Serikali imeamua
kununua ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 78 wakati fedha zilizopitishwa na
Bunge hili ni Bilioni 500 ambazo zingetosha kununua ndege mpya kubwa na za kubeba
abiria wengi zaidi na hivyo kuwa na ufanisi na hata uwezo mkubwa wa kwenda
safari za mbali.Au ndio yaleyale ya kutumia Mawakala ambao wanajiwekea asilimia
kama ilivyokuwa huko nyuma katika ununuzi wa ndege ya Rais ?
Aidha kwa mujibu wa waziri wa Fedha alipokuwa
anawasilisha mpango wa maendeleo hapa Bungeni alisema kuwa serikali imeamua
kununua ndege mbili aina ya Q 400 mbili na CS 300 Moja.
Kutokana na uamuzi huo ni kuwa ndege aina ya Q400
mwaka jana ilikuwa dola milioni 31.3 na ndege aina ya CS 300 ilikuwa dola
milioni 82.0
Hivyo basi kimahesabu ni kuwa ndege 2 aina ya
Q400 na ndege 1 aina ya CS 300 ni jumla
yake itakuwa shilingi Bilioni 318.120
(usd1= 2,200) na hivyo kufanya kiasi cha shilingi Bilioni 181.880 kikisalia .
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua ni kwanini tulitenga
kiwango hicho cha fedha (500bilioni) wakati bei halisi za ndege zinajulikana?
Hizi fedha zinazosalia baada ya manunuzi ya ndege hizo zitatumika kufanya
shughuli gani ? Je kuna Wakala katika ununuzi huu wa ndege ambaye atapata
Kamisheni, na kama yupo ni kiasi gani ?
9.1 Hakuna fedha za kuendesha ATCL
Mheshimiwa Spika, pamoja na serikali kutenga fedha kwa ajili ya kununua ndege mbili,
jambo la kushangaza ni kuwa hakuna fedha za uendeshaji ambazo zimetengwa na
serikali kwa ajili ya shirika letu la ndege ATCL .Hata kwenye mashirika ya
serikali ambayo yatapata ruzuku kwa mujibu wa kitabu cha Volume II ‘Public
Expenditure’ kifungu 62 kasma 2006 kifungu 270846 ATCL zimetengwa shilingi bilioni 3.221 kwa ajili ya mishahara.
Fedha kwa ajili ya uendeshaji ‘other charges’ hakuna hata senti moja
iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua baada ya serikali kununua ndege
hizo mbili shirika litapata wapi fedha kwa ajili ya undeshaji na hasa
ikizingatiwa kuwa shirika mpaka sasa ni mufilisi ? Serikali haikuona umuhimu wa
kulipatia shirika hili ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa shirika, mtaji wa
kuanzia utatoka wapi?
9.2
UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA MWL.JK NYERERE PHASE
II
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere awamu ya
pili uko katika hatihati ya kusimama kutokana na Serikali kutokutii makubaliano
ya mikataba ambayo waliingia na Kampuni ya Ujenzi ya BAM International ya
Uholanzi. Hii ni baada ya wizara ya fedha kuamua kukiuka masharti ya mkataba
baina ya TAA na BAM International kuwa fedha za kutekeleza mradi zitatolewa na
HSBC kwa awamu zote mbili yaani phase 1&2 na badala yake wizara ya fedha
imeamua kwenda kutafuta Mkopo Mpya nje ya makubaliano ya mkataba baina ya BAM
na TAA wa Octoba 2015.
Mheshimiwa Spika, jambo hili la wizara ya fedha kuingilia na kuanza kutafuta mkopo
sehemu nyingine nje ya makubaliano ya awali linahatarisha ukamilikaji wa ujenzi
wa uwanja huu na hata mkandarasi ametishia kusimamisha ujenzi kama fedha za
ziada hazitaongezwa kwa ajili ya mradi huu.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua ni sababu gani zimeipelekea wizara
ya fedha kwenda kutafuta mkopo mwingine kutoka taasisi nyingine nje ya
makubaliano ya awali ya kimkataba? Nani ananufaika na utaratibu huu wa kutafuta
mkopo mpya badala ya kukamilisha taratibu zilizokuwepo? Je, Kitendo cha kuanza
kutafuta mkopo upya kitachelewesha ukamilikaji wa mradi huu kwa kiwango gani?
Nani atalipia hasara itokanayo na kuchelewa kutekelezwa kwa mradi huu?
9.3
UJENZI WA
KIWANJA CHA NDEGE CHATO
Mheshimiwa Spika, ukisoma Mpango wa Maendeleo wa Taifa
katika eneo la usafiri wa Anga moja ya kipaumbele cha mpango katika uk.76
sehemu (x) ni ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Chato. Mradi huu unahusisha
ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege Chato kwa ajili ya huduma za usafiri wa anga kwa
mwaka huu wa fedha 2016/2017 mpango wa maendeleo umetenga kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kuanza kufanyika
kwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua kama paliwahi kufanyika
kwa utafiti wa kina na majibu ya utafiti huo kuonyesha kuwa ujenzi wa kiwanja
cha ndege Chato ndio kipaumbele cha
taifa kwa sasa na kuwa mradi huu umelenga malengo mapana ya taifa ya kukuza
uchumi wa taifa letu. Kwanini fedha hizi zisingeongezwa kwenye kuimarisha
viwanja vilivyopo kwa sasa na hasa ikitiliwa maanani kuwa serikali ndio kwanza
inawaza kununua ndege tatu kwa shirika letu la Ndege.
10 .PRESIDENTIAL DELIVERY BUREAU-BRN
Mheshimiwa Spika, kitengo hiki ambacho kilianzishwa kwa mbwembwe nyingi na serikali ya
awamu ya nne na hata Bunge hili kushawishiwa kuwa ndio njia pekee ya kuongeza
ufanisi serikalini chini ya kauli mbiu ya Matokeo Makubwa Sasa! kimeshindwa
kabisa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Itakumbukwa kuwa wakati kitengo hiki
kinaanzishwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tulipinga uanzishwaji wa kitengo
hiki kwani kilikuwa ni kwa ajili ya ulaji tu.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha wameamua kimya kimya kukivunja
kitengo hiki kwa kutotenga hata senti moja kwa ajili ya mishahara na marupurupu
mengine kwa ajili ya wafanyakazi wa Kitengo hiki (VOTE 6) na badala yake
zimetengwa kiasi cha shilingi 397,278,000
kwa ajili ya kulipia kodi ya pango , (kasma
220700-rental expenses ).
Aidha, ukiangalia bajeti ya mwaka wa fedha
ulioisha 2015/2016 kifungu hiki kilitengewa kiasi cha shilingi 602,800,000 kwa ajili ya kodi hiyo
hiyo.
Mheshimiwa Spika, ukisoma katika kitabu cha Maendeleo - Volume IV utaona kuwa fungu 06 President’s Delivery Bureau
zimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 27,218,829,000
ambazo zote ni fedha kutoka nje (DFID & UNDP) na maelezo yake ni kuwa ni
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya matokeo makubwa sasa ambayo kimsingi
haijaainishwa kwa ufasaha kwenye randama na vitabu vya bajeti.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata maelezo ya kina juu ya mambo
yafuatayo;
i.
Waliokuwa watumishi wa kitengo hiki wamehamishwa, wamefukuzwa au
wamesimamishwa kazi? Mbona hakuna fedha za mishahara na marupurupu mengine kwa
kitengo hiki?
ii.
Ni sababu zipi zimepelekea kitengo hiki kutokupatiwa fedha za uendeshaji
mwaka huu wa fedha?
iii.
Ni nani ataenda kusimamia fedha za Maendeleo takribani bilioni 27
ambazo zimetengwa kama kitengo hakina wafanyakazi? Au ndio kusema kwamba DFID
&UNDP itakuwa ikisimamia fedha zake moja kwa moja?
iv.
Tangu kuanzishwa kwa kitengo hiki kimetumia kiasi gani cha fedha na
ufanisi wake umekuwa upi?
v.
Fedha za malipo ya pango/kodi ni kwanini mwaka huu imepungua kwa zaidi
ya aslimia 48 kulinganisha na ya mwaka jana? Nani watakaa kwenye jengo hilo
wakati hakuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya mishahara yao?
11 . MILLENIUM CHALLENGE
CORPORATION (MCC)
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya Wizara ya Fedha na Mipango kifungu 1007 katika
mwaka wa fedha 2016/17 idara wameomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 500 kama bajeti yake ya
matumizi ya kawaida. Kati ya fedha
hizo kiasi cha shilingi milioni 60
(kasma 210300) zinaombwa kwa ajili ya kuwalipa posho ya majukumu kwa watumishi
12 wa MCA-T Compact II watakaofanya kazi ya uchambuzi wa miradi inayohitaji
ufadhili wa MCC. Aidha kiasi cha shilingi milioni
280 (kasma 220700) ni kwa ajili ya kulipia pango la ofisi.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa Bodi ya wakurugenzi ya MCC mnamo tarehe 28,Machi 2016
ilisimamisha kutoa fedha kwa Tanzania katika mradi wa MCA-T Compact II zaidi ya shilingi trilioni moja (USD. 472,824,825)
ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya umeme nchini kutokana na serikali hii
ya CCM kupitisha sheria mbaya na kandamizi ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crime
Act), Sheria ya Taifa ya Takwimu na kuminywa kwa Demokrasia Nchini hasa kufutwa
kwa matokeo halali ya Uchaguzi wa Zanzibar
ya Octoba 25,2016.
Mheshimiwa Spika, baada ya Marekani kusimamisha utoaji wa fedha kwa ajili ya mradi huu,
bodi ya wakurugenzi ya MCC ilimuandikia rasmi barua Rais wa Jamhuri ya Muungano
ya Tanzania Mhe.John Magufuli tarehe 31 Machi,2016 na kumjulisha rasmi juu ya
uamuzi wake .Pamoja na Rais kujulishwa kwa barua Kambi rasmi ya Upinzani ina
taarifa kuwa mpaka tarehe 11/05/2016 barua hiyo ya Bodi ya MCC ilikuwa
haijapatiwa majibu na Ikulu .
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupatiwa majibu ya kina juu ya mambo
yafuatayo;
i.
Ni kwanini serikali inaomba fedha kwa ajili ya kulipa watumishi ambao
watachambua miradi ya MCC ambayo haipo?
ii.
Ni lini serikali itaijibu barua ya bodi ya MCC? Kwanini imechukua muda
mrefu kiasi hicho kutoa majibu kwa barua yao? Hasa ikizingatiwa kuwa katikati
ya mwezi Juni Bodi ya MCC itakaa pamoja na mambo mengine itatoa uamuzi wa
mwisho juu ya jambo hili.
iii.
Hivi kulipia kiasi cha shilingi milioni
280 cha kodi ya ofisi kwa mwaka ambayo ina watumishi 12 ni kiwango sahihi?
Kinaendana na dhana ya kubana matumizi?
12 . WATUMISHI HEWA SERIKALINI
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 01 Mei, 2016 wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mei
mosi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Magufuli alilitangazia
taifa kuwa jumla ya watumishi hewa walikuwa wamefikia 10,295 na alisema kuwa
kati ya watumishi hao hewa 8,373 wanatoka TAMISEMI na watumishi 1,922 wanatoka
Serikali Kuu. Aidha, aliendelea kusema kuwa watumishi hao hewa walikuwa
wakiligharimu taifa shilingi Bilioni
11.6 kwa mwezi sawa na shilingi Bilioni
139 kwa mwaka na kwa miaka 5 ni shilingi Bilioni 695.
Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni nyingi sana kwa nchi maskini kama hii ya kwetu kupotea
kwa sababu tu ya uzembe na kukosekana kwa usimamizi ulio makini na dhabiti
katika kusimamia rasilimali za taifa letu.Jambo hili halikubaliki hata kidogo
katika ulimwengu wa sasa na teknolojia ilikofikia ya watumishi kupokea
mishahara kupitia Benki.
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, kupitia hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni katika Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa umma; ilitoa suluhisho la kuweza kushughulikia
ufisadi huu wa watumishi hewa ambao unalelewa na mfumo.
Aidha, leo tunataka kujua hatua ambazo
zimechukuliwa dhidi ya Maafisa maduhuli, wakuu wa idara na vitengo pamoja na
wahasibu ambao ndio wanaondaa na kupitisha orodha ya watumishi ambao
wanastahili kulipwa kila mwezi ‘pay roll’. Hawa ndio wanaoandaa orodha, mbona
mpaka leo bado wapo kazini?
13 . WIZARA YA FEDHA, BENKI YA STANBIC NA SAKATA LA MKOPO WA DOLA MILIONI 600-UTAKATISHAJI
FEDHA HARAMU
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13 serikali ya Tanzania iliomba mkopo wa dola millioni 600
kwa malengo ya kugharamia mpango wa Taifa wa miaka mitano. Mkopo huu uluzihusisha
benki zenye mahusiano ya kibiashara stanbic (Tanzania) na Standard Bank PLC
(kwa sasa inafahamika kama ICBC Standard Bank PLC) (Standard Bank) ya Uingereza.
Standard Bank ilihusishwa kutokana na ukweli kwamba aina ya mkopo ambao
serikali ilikuwa inautaka Benki ya Stanbic Tanzania ilikuwa haitoi hiyo huduma
ya aina hiyo.
Mheshimiwa Spika, Inasemekana kwamba mchakato huo ulihusisha udanganyifu wa ada ya mkopo,
taarifa zinaonyesha kwamba ada halali
iliyotakiwa kulipwa ni 1.4 % ya mkopo wote, hata hivyo ada iliyokuja kulipwa ni 2.4% ya mkopo wote.
Kutokana na udanganyifu huo, kuna kesi inayoendelea mahakamani
ikiwahusisha aliyekuwa kamishna Mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania, ndugu
Harry Kitilya (na mwenyekiti wa bodi ya EGMA, inayohusishwa katika sakata hili),
aliyekuwa Mkuu wa idara ya ushirikiano na uwekezaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, Shose Sinare
pamoja na aliyekuwa mwanasheria Benki ya Stanbic Tanzania, Bwana Sioi Solomon SUMARI.
Mheshimiwa Spika, Sio dhamira ya Kambi Rasmi ya Upinzani kujadili wahusika tajwa hapo juu
kwa kuwa tunatambua, kanuni zetu za Bunge zinatuzuia kujadili suala ambalo liko
Mahakamani, lakini kwa kuwa leo ni siku ya kujadili Bajeti ya Serikali ni
wajibu wetu kama kambi kuhoji nini kilichopelekea udanganyifu huo na kwa
kiwango gani Serikali hii ilitekeleza wajibu wake kikamilifu ili kuepusha
makosa kama hayo kujirudia hasa ukizingatia kwamba katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2016/17, serikali inatarajia kukopa mikopo ya
kibiashara ya aina hii ili kufidia ombwe la bajeti yenye thamani ya
shilingi trillion 7.4. Na wahusika wakuu katika mchakato mzima ndio hao
wahusika!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inazo nyaraka mbali mbali, moja wapo ikiwa ni
barua toka TAKUKURU (TAASISI YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA) kwenda kwa mwanasheria mkuu wa serikali, Mhe. George
M. Masaju yenye kumbukumbu namba CACE255/362/01/104 ya tarehe 20/01/2016. Barua
husika imeambatanishwa na barua kwenda kwa Kitengo cha kimataifa cha makosa ya
jinai (International Criminal Unit) kikiomba msaada wa uchunguzi wa wahusika
katika sakata husika, huku ikirejea vifungu vya sheria vilivyovunjwa!
Mheshimiwa Spika, Barua husika ina ainisha mambo yafuatayo:
1.
Imewataja majina ya watu wanaochunguzwa kwa kukiuka:
a) vifungu
22,23,31,32 na 34(1)sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa (The Prevention and Combating
of Corruption Act 2007.
b) Vifungu 333, 335 na 337 vya sheria ya kanuni za adhabu (The Penal Code
(Cap 16 R.E 2002).
c)
Vifungu 12,13 vya sheria ya
kuzuia utakatishani wa fedha haramu ( Anti- Money Laundering 2006 (R.E 2012)
Watuhumiwa
wakiwa Stanbic Bank,Harry Msamire
Kitilya (Aliyekuwa Kamishna Mkuu TRA), Peter Anandi Nyabuti, Bashir Awale,
Shose Sinare, Sioi Solomon Sumari, Dr
Servacius Likwelile (Katibu Mkuu Wizara
ya Fedha), Alfred Paul Misana, Bedason Shalanda, Ramadhan Kijjah na Ngosha Said
Magonya
2.
Mpaka mwezi Februari 2012 makubaliano ya ada ya mkopo kwa benki zote
mbili ( Standard na Stanbic ) ilikuwa 1.4%
ya Mkopo wote
3.
Mchakato ulisuasua sana /ulikwama mpaka mwezi septemba 2012 pale ambapo
Stanbic ‘iliongeza’ ada mpaka 2.4% .
4.
Nyongeza hiyo ya 1% angelipwa
‘local partner’ na kwamba mgao huo ulikuwa na malengo ya kumshawishi ndugu Harry Kitilya na pengine ‘maafisa wengine wa serikali ya Tanzania’ili wawape upendeleo wa
kuchukua mkopo toka benki tajwa hapo juu.
5.
Mara tu baada ya nyongeza ya 1%,
mchakato ulikwenda kwa kasi ya ajabu. Mwezi Novemba 2012 barua ya ‘mandate and
fee’ ilisainiwa kati ya standard bank, Stanbic Bank na Wizara ya fedha .
6.
Makubaliano husika hayakuelezea chochote kuhusiana na ‘local patner’ au ‘mtu wa tatu’ zaidi
ya kuainisha ada ya ujumla ya 2.4% iliyoogezwa kiaina toka 1.4%
7.
Pamoja na yote, utaratibu uliopangwa na pande zote tatu (Stanbic/Standard na wizara ya fedha)uliruhusu fedha ya UMMA (MKOPO wa
kibiashara) kuingizwa kwenye akaunti binafsi
ya ‘local partner’ badala ya fedha
husika kuingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Serikali ya Tanzania.
8. Pamoja na kwamba kulikuwa na viashiria vyote vya hatari ya rushwa na udanganyifu,hakuna afisa yeyote
ya serikali (wizara ya fedha) ,wala timu ya benki ya standard bank aliyeonekana
kujali,wala kuhoji chochote na wala hawakutaka kuchunguza au kuhoji uhalali wa
huyo ‘third party’ au ‘local partner’ ambaye sio sehemu ya mkataba /makubaliano
kuingiziwa 1% ya fedha ya Mkopo
9.
Baada ya fedha husika kuingizwa kwenye akaunti ya ‘Local Partner’ mwezi
Machi 2013. Kiasi kikubwa cha fedha kilianza kuondolewa haraka haraka na ndugu
Fratern Mboya. Ikumbukwe akaunti hii ilifunguliwa mahsusi mwezi mmoja kabla
(February 2013)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iliambie Bunge hili tukufu;
i)
Ni vigezo gani vilivyotumika
kuwachuja watuhumiwa kutoka 11 mpaka 3?
ii)
Ni kwa vigezo gani wizara ya
fedha iliruhusu fedha za Umma kuingia katika akaunti binafsi huku ikifahamu
(kama ilivyoainishwa kwenye barua) anayeingiziwa fedha hajatajwa/hayuko kwenye
mkataba baina ya serikali na benki tajwa hapo juu?
iii)
Ni kwa kiwango gani wizara ya
fedha inadhani, ilitekeleza wajibu wake ipasavyo katika mchakato mzima? Kama
ndio kwa nini? Kama sio ni hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya maafisa wa
serikali (Wizara ya Fedha) waliopewa dhamana kusimamia mchakato mzima?
iv)
Barua ya TAKUKURU inamtaja
bwana Franten Mboya kuhusika na utoaji wa mabulungutu ya fedha kwa kipindi cha
siku 10 mfululizo, na kiasi kilichobaki kuhamishiwa kwenye akaunti nyingine ya
‘local partner’. Japokuwa Kambi Rasmi haijui hayo ‘mabulungutu’ yalienda kwa
nani?. Kwa nini ndugu huyu sio miongoni mwa washtakiwa? Kwa nini wameshtakiwa
watatu tu?
v)
Ni kwa nini mpaka sasa
Dr. Servacus Likwelile , Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
ndugu Paul Misana kamishna wa wizara
ya fedha hawajafunguliwa
mashtaka na wanaendelea kuitumikia
serikali hii inayojinasibu kwa kutumbua
majipu? Mbona hii sheria sio msumeno tena? Inang’ata upande mmoja tu?
13.2 Uwezo Mdogo wa Benki Kuu Kufanya Ujasusi wa Miamala ya Fedha na
Kuchukua Hatua Stahiki
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatilia mashaka uwezo na dhamira ya kitengo cha
Financial Intelligence Unit (FIU) cha Benki Kuu kufanya ujasusi wa Miamala ya
fedha katika kuzuia utakatishaji wa fedha haramu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kitengo cha Financial
Intelligence Unit (FIU) kina mamlaka ya kiutawala pekee na huishia kufanya
uchambuzi wa taarifa za miamala ya fedha na kuziwasilisha ama Jeshi la Polisi
au PCCB, wakati huo huo PCCB inalazimika kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP) ili atoe ruhusa ya kufungua mashitaka.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kuwa FIU haina uwezo wa kufanya uchunguzi, wala
kuendesha mashitaka dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu jambo ambalo ni
mwanya unaotumiwa na watu waovu na mafisadi kama ilivyokuwa katika wizi wa
Mabilioni ya Rada, wizi wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na wizi wa
fedha katika Mkopo wa Serikali dola milioni 600 kutoka Stanbic Bank.
Mheshimiwa Spika, mahakama ya mafisadi inayokusudiwa kuanzishwa na Serikali haitaweza
kufanya kazi kwa ufanisi kama mifumo iliyopo yenye mianya ya kifisadi
haitazibwa. Mfumo wa FIU ya Tanzania ni “administrative model” wakati mfumo
imara zaidi ni ule wa “Judicial Model” ambao unakiongezea nguvu kitengo hicho
cha kuzuia miamala ya biashara haramu za kutakatisha fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa “Egmont[13]
Group of Financial Intelligence Units” Judicial Model of FIU inamaanisha kuwa
“The Judicial Model is established within the judicial branch of
government wherein “disclosures” of suspicious financial activity are received
by the investigative agencies of a country from its financial sector such that
the judiciary powers can be brought into play e.g. seizing funds, freezing
accounts, conducting interrogations, detaining people, conducting searches,
etc.”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuimarisha kitengo
cha FIU kwa kukiundia Mfumo wa Judicial Model ili kuepuka aibu ambayo Taifa
letu limekuwa likiipata kutokana na Serious Fraud Office ya Uingereza
kuwana na uwezo wa kurudisha fedha za zilizoibiwa kwa njia ya kifisadi wakati
kazi kama hiyo ingeweza kufanywa na vyombo vya hapa nchini endapo
vingeimarishwa kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inavyoshauri.
14 MADENI AMBAYO SERIKALI INADAIWA NA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina mifuko sita ya hifadhi ya jamii ambayo inachangia kwa
kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa lakini pia maendeleo ya kiuchumi ya
wanachama wake. Mifuko hii ni
Parastatals Pensions Fund (PPF), Public Service Pension Fund (PSPF), Local Authorities
Pension Fund (LAPF) National Social Security Pension Fund (NSSF), National
Health Insurance Fund (NHIF) na Government Employees Pension Fund (GEPF).
Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango mkubwa wa mifuko hii ya jamii katika uchumi wa taifa
na maendeleo ya kiuchumi ya wananchama wake; mifuko hii imeathiriwa vibaya na
mikopo isiyo na tija (non- performing loans) inayotoa kwa Serikali na taasisi
zake. Mifuko hii iko katika hatari ya kufilisika kutokana na mikopo hiyo kukosa
dhamana (guarantee) au mikataba rasmi na Serikali jambo linalopelekea uwezekano
wa fedha hizo zilizokopeshwa kwa Serikali na taasisi zake kupotea au kurejeshwa kwa kasi ndogo sana na hivyo kukosa tija.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
kwa mwaka wa fedha 2013/2014 madeni ya Serikali kutoka katika hifadhi za jamii
yamekuwa yakiongezeka huku kukiwa na kasi ndogo sana ya urejeshaji wa mikopo hiyo na wakati mwingine hakuna
kabisa urejeshaji unaofanyika.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, mpaka kufikia tarehe 30 Juni, 2014,
deni la Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia takriban shilingi trilioni
1. 69 ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha takriban shilingi bilioni 975 kilikuwa kimeiva tayari kulipwa
katika mifuko hiyo ya hifadhi lakini Serikali haikulipa.
Jedwali Na.1. Mchanganuo wa
madeni ya Serikali katika kila mfuko wa hifadhi ya jamii, hadi kufikia tarehe
30 Juni, 2014
MFUKO WA HIFADHI YA JAMII
|
JUMLA YA DENI (Tshs)
|
KIASI KILICHOIVA TAYARI KULIPWA (Tshs)
|
LAPF
|
173,231,417,845.00
|
94,655,371,891.00
|
PSPF
|
460,995,168,878.82
|
251,942,767,372.27
|
PPF
|
221,070,451,951.77
|
27,252,909,658.32
|
NHIF
|
105,792,983,055.76
|
26,325,247,799.96
|
NSSF
|
722,460,946,894.36
|
575,048,756,582.94
|
GEPF
|
14,333,964,512.22
|
0
|
JUMLA
|
1,697,884,933,137.93
|
975,048,756,582.94
|
CHANZO: Ripoti ya CAG ya 2013/14
Mheshimiwa Spika, kufuatia malimbikizo ya madeni ya Serikali katika mifuko ya hifadhi
za jamii, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliitisha kikao
cha baina ya Serikali na mifuko ya hifadhi za jamii tarehe 24 Oktoba, 2014 ili
kupata maelezo ya Serikali kuhusu ulipaji wa madeni hayo. Katika kikao hicho,
ilibainika kwamba kulikuwa na tofauti ya kiwango cha deni la mkopo katika taarifa ya Serikali na ile ya mifuko
ya hifadhi za jamii. Kutokana na hali hiyo, kiliundwa kikosi kazi cha
kilichojumuisha wadau kutoka Serikalini, taasisi za Serikali na mifuko ya
hifadhi za jamii ili kufanya uchunguzi kujua kiwango halisi cha deni ambalo
Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi za jamii.
Mheshimiwa Spika, CAG anaeleza kwamba ripoti ya kikosi kazi hicho kilichoundwa ili
kubaini deni halisi Serikali inayodaiwa na mifuko ya jamii ilionyesha kwamba
hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2014 jumla ya deni halisi ambalo Serikali ilikuwa
inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ni takriban shilingi trilioni 1.875, ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 937.865 kilikuwa
kimeiva tayari kulipwa lakini Serikali ilikuwa haijalipa fedha hizo kwa mifuko
ya hifadhi ya jamii. Hata hivyo, hadi kufikia tarehe 7 Machi, 2015 Serikali
ilikuwa haijalipa kiasi hicho kilichoiva kwa mifuko ya hifadhi za jamii.
Jedwali Na. 2 Mchanganuo wa madeni ya Serikali katika kila mfuko wa
hifadhi ya jamii yaliyofanyiwa uhakiki na kikosi kazi hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2014.
MFUKO WA HIFADHI YA JAMII
|
JUMLA YA DENI HALISI
|
KIASI KILICHOIVA TAYARI KULIPWA
|
LAPF
|
173,231,417,845.00
|
94,655,371,891.00
|
PSPF
|
478,564,986,495.99
|
273,422,154,530.03
|
PPF
|
275,682,357,071.87
|
53,269,846,358.40
|
NHIF
|
106,576,578,959.00
|
27,651,457,652.66
|
NSSF
|
827,506,941,339.53
|
488,866,404,953.71
|
GEPF
|
14,333,964,512.22
|
0
|
JUMLA
|
1,875,896,246,224.49
|
937,865,235,385.80
|
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG, deni hili la trilioni 1.875 ambalo
Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii, halijumuishi deni la shilingi
trilioni 7.066 ambalo PSPF inaidai Serikali kutokana na kuwahamishia wananchama
waliokuwa chini ya mifuko ya pensheni kwenda PSPF ambao makato yao hayakuwa
kwenye mfuko wa PSPF lakini Serikali ikaamuru walipwe penshini jambo ambalo ni
kinyume na sheria ya mifuko ya hifadhi za jamii.
Mheshimiwa Spika, ikiwa deni hili la shilingi trilioni 7 litajumlishwa na lile la
awali, Serikali sasa itakuwa inadaiwa na mifuko ya jamii Jumla ya shilingi 8,942,426,246,224.49 (trilioni 8.942), na
hii ni mbali na madeni mengine ambayo Serikali inadaiwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Seirkali kutoa maelezo mbele ya bunge
hili, ni kwa nini hailipi madeni (tena yaliyoiva tayari kulipwa) kwa mifuko ya
hifadhi ya jamii.
15 KODI KATIKA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI- PAYE
Mheshimiwa Spika, wakati Rais Magufuli akilihutubia Taifa wakati wa sherehe za siku ya
Wafanyakazi Duniani alizungumzia suala la makato ya mishahara ya wafanyakazi
(PAYE). Na kwa mamlaka aliyonayo kama
Mkuu wa Nchi aliasema kuwa amepunguza makato hayo ya PAYE kutoka asilimia 11
hadi asilimia 9, na kuagiza kuwa suala
hilo lianze kufanyiwa kazi katika mwaka wa fedha 2016/2017 .
Mheshimiwa Spika, kodi hii ya mshahara imekuwa
ni kilio kikuu kwa wafanyakazi na ni ukweli ulio wazi kuwa kundi hili la
wafanyakazi ndilo linalolipa kodi kubwa kuliko makundi mengine katika jamii
yetu. Busara iliyotumiwa na Mhe. Rais
Magufuli kupunguza Kodi hii ya PAYE kwa
ngazi ya chini iliyokuwa inalipa asilimia 11 na kuwa asilimia 9 kwa wale
wote ambao wanapokea mshahara wa kati ya
shilingi 170,000 na 360,000/-, na kiwango kitakachokatwa hiyo asilimia 9 ni
shilingi 190,000/- ambayo ni tofauti kati ya (360,000-170,000). Kwa wale ambao mshahara wao ni shilingi
540,000/-, PAYE itakuwa 17,100 + 20%
ya tofauti kati ya silingi 540,000- na 360,000/- ambayo ni shilingi 36,000/-,
hii inafanya mshahara huo kukatwa shilingi
53,100/-. Na kwa wale wanaopokea Mshahara wa shilingi 720,000/- kwa
mwezi kodi ya PAYE ni shilingi 53,100 + 25% ya tofauti kati ya shilingi
540,000/- na 720,000/- ambayo ni shilingi
45,000/-, hivyo kufanya PAYE kwa
mshahara wa shilingi 720,000/ kuwa shillingi
98,100/-.
Mheshimiwa Spika, na kwa wale wote wanaopokea zaidi ya shilingi 720,000/- kwa mwezi kodi
ya Mshahara ni sawa na Tsh 98,100 +30%
ya tofauti ya shilingi 720,000/- na kiwango cha juu cha mshahara. Mathalani kwa
mtu anayepokea mshahara wa shilingi
2,500,000/- kwa mwezi, PAYE ni sawa na Tshs 98,100+ 30% ya 1,780,000/-
(534,000) na hivyo makato ya PAYE kuwa shilingi
632,100/-
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri lengo la Mheshimiwa Rais lilikuwa zuri la kuwapunguzia mzigo
wa kodi watumishi wa umma, lakini inawezekana kabisa Mheshimiwa Rais bado hajaelewa utaratibu mzima wa makato,
kwani ingekuwa ni bora kama punguzo la asilimia 2 lingekwenda sambamba kwa kila
ngazi ya mshahara (yaani punguzo la 2%
kwa 20%, 25% na 30%) kwa kulingana na utaratibu wa makato kama ulivyowekwa
na TRA.
Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwamba Serikali itoe punguzo la 2% kwa ngazi zote
za mshahara kama ambavyo Rais Magufuli alivyokuwa amedhamiria, kinyume na
hapo punguzo hilo la PAYE kutoka
asilimia 11 hadi 9 itakuwa ni kiini macho kwa wafanyakazi.
Na hii ni kutokana na ukweli kuwa wafanyakazi hawa
bado wana mzigo mkubwa sana wa kodi katika kupata huduma mbalimbali ambazo ni
mahitaji muhimu katika maisha yao ya kila siku kama vile VAT, na kodi
nyinginezo , hivyo kuwapunguzia makato ya kodi katika mishahara yao
itawawezesha kuwa na kipato cha kuwawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku.
16 UPOTEVU MKUBWA WA
MAPATO ITOKANAYO NA MISAMAHA YA KODI
Mheshimiwa Spika, misamaha
ya kodi imekuwa ikilikosesha taifa fedha nyingi. Kambi Rasmi ya Upinzani
imekuwa ikishauri kila mara katika mapendekezo ya hotuba ya bajeti kuwa
misamaha ya kodi angalau isizidi asilimia 1ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia (Opening the gate 2012) Tanzania
ilikuwa ikipoteza takribani trillioni 2.9 kwa upotevu holela wa kodi bandarini
peke yake. Mwaka 2013/2014 misamaha ya kodi iliongezeka kutoka 1.4 trilioni
mpaka 1.8 trilioni. Mwaka 2014/2015 serikali ilitoa misamaha ya takribani
shilingi bilioni 1,627 sawa na 2% ya GDP.
Mheshimiwa Spika, kwa
takribani miaka mitano sasa serikali haijaweza kufikia lengo la kupunguza
kudhibiti misamaha ya kodi angalau
isiyozidi 1%ya GDP. Hii ni kutokana na uzembe mkubwa wa serikali katika
kukusanya kodi, sera mbovu za ukusanyaji wa mapato, udhaifu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania katika kukusanya kodi,
vitendo vya rushwa kubwa na zile ndogo ndogo zinazotokana na uswahiba wa
karibu na baadhi ya viongozi wasio waaminifu.
Mheshimiwa Spika, sambamba
na misamaha ya kodi baadhi ya makampuni ya madini yenye mikataba maalumu
yameruhusiwa kuwekeza nje mauzo yake yote kinyume na utaratibu wa kampuni
nyingine ambazo hutakiwa kurejesha nchini mauzo yao. Kwa mujibu wa gazeti la
Mwananchi la April 29, 2016, makampuni
hayo yenye mikataba maalum yameruhusiwa kuwekeza mauzo yake nje ya nchi (illicit financial
flows) ambapo jambo hilo limerasimishwa
katika sheria ya madini ya mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika, Jambo
hili linaisababisha hasara kubwa serikali, ikiwa ni pamoja na mapato yatokanayo
na kodi zinazopotea tu kiholela. Ni wazi sasa serikali iko katika wakati mgumu
kifedha na maisha ya wananchi yanazidi kuwa magumu kutokana na kupanda kwa
gharama za bidhaa mbalimbali ikiwemo sukari, mafuta ya magari, vyakula n.k
Hivyo ni aibu kwa serikali kuendelea kulegeza, au kutojali kabisa hasara kubwa
inayotokana na misamaha ya kodi, mianya ya udhibiti wa makusanyo ya kodi,
mikataba na sera mbovu ambazo hazinufaishi taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa maelezo juu ya maswali
yafuatayo:
i.
Je, ni kampuni zipi
na ngapi zenye ruhusa ya kuwekeza mapato yake yote nje ya nchi?
ii.
Je, serikali
imefanya tathimini kuwa tunapoteza kiasi gani cha fedha za kigeni yaani
(foreign reserves) kutokana na mikataba ya namna hii?
17. MAMLAKA YA
MAPATO TANZANIA-UKUSANYAJI KODI
Mheshimiwa
Spika, Ili kuijengea uwezo
TRA kutokana na uwezo mdogo wa kukusanya mapato kulingana na vyanzo vilivyopo
na uwepo wa mianya mingi ya ukwepaji kodi na kushindwa kusimamia sera za
misamaha ya kodi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Serikali iridhie
mpango wa kufanya mapitio makubwa ya Mfumo
Mzima wa Ukusanyaji wa kodi nchini (Robust and Comprehensive Tax Regime Review)
ili kuusuka upya kwa kuondoa na kuziba kabisa mianya yote ya upotevu mkubwa wa
mapato uliosababishwa na uzembe wa Serikali kuisimamia TRA katika ukusanyaji wa
Mapato.
18.KIZUNGUMKUTI
CHA MABILIONI YA JK
Mheshimiwa Spika,
itakumbukwa kuwa toka serikali ya awamu ya nne iwepo madarakani uliimbwa wimbo
maarufu wa mabilioni ya Kikwete au JK ambayo yalitolewa na serikali wakati huo
ikiongozwa na Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete. Kambi Rasmi ya Upinzani
kupitia hoja mbalimbali za wabunge na maswali yao hapa Bungeni walizungumzia na
kuhoji utaratibu wa mgawanyo wa mabilioni hayo na serikali haikuwahi kuweka
wazi utaratibu mgawanyo huo zaidi ya kutoa majibu ya kisiasa kuliko uhalisia wa
jambo husika.
Mheshimiwa Spika,
wakati akijibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka (Viti Maalum) katika
Mkutano huu wa Bajeti Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana,
Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mheshimiwa Abdalah Possi alieleza Bunge hili
kuwa kiasi cha shilingi bilioni 50.6 kilitolewa kama mikopo kwa ajili ya
mabilioni ya Kikwete lakini ni kiasi cha bilioni 41.53 ndicho kilichorudishwa
na wakopaji. Hii inamaanisha kuwa takribani bilioni 9 hazikuweza kurudishwa na
walionufaika na mabilioni hayo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuhoja masuala yafuatayo; mosi, ni kwa
nini fedha hazikurudishwa zote? Kwa sasa fedha hizo zilizorudishwa zipo wapi na
zinafanya kazi gani? Je serikali imechukua hatua gani kwa fedha ambazo
hazijarudishwa? Na je ni utaratibu gani uliotumika kugawanywa fedha hizo na kwa
vigezo gani?
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali kuwa pamoja na majibu ya maswali
yaliyoulizwa kuhusu mabilioni haya imwagize Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha
za serikali kufanya uchunguzi maalum juu ya fedha hizi na kuwasilisha taarifa
yake kwa Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC) na taarifa ya Kamati
kujadiliwa katika Bunge hili.
19 MIKATABA MIBOVU
SEKTA YA MADINI NA NISHATI INALIKOSESHA TAIFA MAPATO
Mheshimiwa Spika,
kutokana na serikali kuendelea kuingia mikataba mibovu na ambayo haina maslahi
kwa taifa na kuifanya mikataba kuwa ni siri hata kwa Bunge letu tumeendelea
kupata hasara kama taifa kutokana na ukweli kuwa mikataba imekuwa mibovu na
ambayo inawanufaisha zaidi wawekezaji kuliko taifa .
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa kitabu cha mapato volume I
kinaonyesha kuwa Gesi italiingizia taifa katika mwaka huu wa fedha 2016/2017
kiasi cha shilingi Bilioni 115.127
(kwa mujibu wa kifungu 140274 - sale of Gas).
Aidha
sekta ya Madini inategemewa kuliingizia Taifa kiasi cha shilingi Bilioni 180.803 ambazo ni fedha
zitakazotokana na mrabaha wa madini (kifungu cha 140353 --Mineral Royalities)
na kiasi cha shilingi Bilioni 29.494
ni kodi mbalimbali kutoka sekta ya Madini (kifungu 140101 –mineral Rent)
Mheshimiwa Spika,
serikali mara zote imekuwa ikijitapa hapa Bungeni na huko nje kwa wananchi kuwa
sasa uchumi wa gesi unaenda kutuondoa katika umasikini kumbe ni hadaa na hali
hii haikubaliki kila mwaka kuendesha serikali kwa fedha za pombe na sigara
ambazo ni nyingi kuliko fedha za sekta ya nishati na madini –kwa mfano mapato ya VAT kutokana na sigara na bia ni shilingi bilioni 263.940 mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye bia,
sigara na vinywaji vikali ni kiasi cha shilingi Bilioni 544.112 (kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato volume 1)
Kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni , tunaitaka serikali
kuiwasilisha mikataba yote ya sekta ya Nishati na Madini hapa Bungeni ili Bunge
liweze kuipitia na kuchukua hatua za kuisimamia serikali kwa mujibu wa katiba,
na hii ndio itakuwa njia sahihi ya kuliokoa taifa na upotevu huu wa
mapato.Aidha tunamtaka waziri aeleze huu uchumi wa gesi ambao unasemwa kila
mara uko wapi ?
20. UUZWAJI
WA HISA ZA TBL
Mheshimiwa Spika, Msajili
mkuu hazina Lawrance Mafulu alinukuliwa wakati serikali ikipitisha bajeti
ya mwaka 2015-2016 kuwa moja ya vyanzo vya mapato ni kodi na mapato
yasiyo ya kodi ambayo yanapatikana na shughuli za kibiashara
ambazo hufanywa na mashirika ya umma ambayo huleta faida katika
mfuko wa serikali kwa njia ya gawio.
Mheshimiwa Spika,
Serikali ilikuwa inamiliki hisa milioni
11.7 katika Kampuni ya bia ya Tanzania, lakini kwa utaratibu ambao
haukueleweka Serikali mwishoni mwa mwaka jana iliuza hisa hizo kwa thamani ya shilingi 15,200/- kwa kila hisa na
hivyo kufanya jumla ya mauzo kuwa shilingi
bilioni 177.84
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inalazimika kukubali na kutaka maelezo ya mauzo hayo,
kutokana na ukweli kuwa katika bajeti ya mwaka 2015/16 Serikali kutokana na
hisa hizo ilipata gawio la jumla ya shilingi
5,700,000,000/- na kwa mwaka huu wa bajeti 2016/17 kitabu cha mapato VOLUME I Kampuni ya Bia
inatoa gawio la shilingi 1,000/- tu.
Hoja ni kuwa inawezekanaje gawio liporomoke kutoka shilingi Bilioni 5.7 mwaka jana hadi shilingi
1,000 mwaka huu?
Mheshimiwa Spika,
taarifa ya kamati ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara ya Fedha na
Mipango uk.21 inaonesha kuwa mauzo ya hisa asilimia 4 za Kampuni ya Bia na
asilimia 2.5 za Kampuni ya sigara zingeuzwa kwa shilingi bilioni 200. Aidha,
taarifa hiyo inasema kuwa makusanyo hadi februari, 2016 zilikuwa ni shilingi
344,470,000,000/- Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kupata maelezo ni kwa nini
fedha hizi hazikuwa zimeoneshwa kwenye makisio ya makusanyo kwenye kitabu cha
JUZUU ya I uk. 10 hadi 13?
21. KUFUTWA KWA
MISAMAHA YA KODI KWA MAJESHI YETU
Mheshimiwa Spika
, wakati waziri wa Fedha akiwasilisha hotuba ya Bajeti alisema kuwa moja ya
hatua ambazo serikali inachukua ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali ni
pamoja na kufutwa kwa misamaha ya kodi kwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na
badala yake alipendekeza kuwepo kwa Posho maalum kwa ajili ya kuwawezesha
wanajeshi wetu kununua mahitaji yao muhimu.
Mheshimiwa Spika, waziri
wa Fedha katika hotuba yake uk.88 alisema kuwa tarehe ya kuanza kutumika kwa
utaratibu huu ni kuanzia Julai 1,2016 .
Kambi rasmi ya
Upinzani Bungeni, inataka kupatiwa
majibu juu ya masuala yafuatayo;
i.
Fedha za kulipa
Majeshi yetu ‘posho maalum’ zipo katika fungu lipi la fedha za bajeti na hasa
ikizingatiwa kuwa mafungu yote katika wizara husika yalishapitishwa na Bunge
hili na posho hiyo haikuwepo?
ii.
Je zile bidhaa na
vifaa vilivyopo kwenye bohari za majeshi yetu zitapelekwa wapi na zipo kiasi
gani kwani utekelezaji wa jambo hili umekuwa wa ghafla sana? yaani chini ya
wiki tatu kabla ya utekelezaji wake kuanza
iii.
Kwanini serikali
isingewachukulia hatua wajanja wachache waliokuwa wanajinufaisha na msamaha huo
na badala yake imeamua kuyaadhibu majeshi yetu yote?
22. BAJETI
MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KWA MWAKA WA 2016/2017
Mheshimiwa
Spika,
bajeti mbadala ya KRUB, ni tulivu na yenye
kuleta matumaini yenye heri kwa Watanzania. Katika kitabu cha Hali ya Uchumi wa
Taifa katika mwaka 2015, cha mwezi Juni
2016 kilichotolewa na wizara ya fedha
Sura ya I ukurasa wa 1 aya ya 2 kinaonesha takwimu za awali za Pato la
Taifa kwa mwaka husika ni shilingi 90,863,681,000,000.
Angalia
jedwali la I;
Jedwali
I
Maelezo
|
Shilingi
|
Asilimia
|
Mapato ya kodi na
yasiyo ya kodi ya Pato la Taifa
|
18,172,736,200,000
|
20
|
Pato la Taifa
|
90,863,681,000,000
|
100
|
Mheshimiwa
Spika, ni ukweli ulio wazi kwamba; tukiweka
mazingira mazuri na rafiki kwa mlipa kodi, tukipanua wigo wa kodi, tukiwa na
sera na viwango vya kodi vinavyotabirika na endelevu, ufanisi ukiongezeka TRA kwa asilimia 50, kudhibiti ukwepaji wa
kodi, kupunguza misamaha isiyokuwa na tija hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la
Taifa, kuongeza ufanisi bandari ya Dar-es Salaam, kuweka mazingira mazuri na
endelevu sekta ya Utali, kukusanya kwa ufanisi mapato kwenye sekta za madini,
uvuvi, maliasili, nyumba,ardhi n.k.
Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na
yasiyo ya kodi hadi kufikia aslimia 20.
Mheshimwa
Spika, inawezekana kutekeleza kwa mambo
hayo hapo juu. Hivyo, KRUB inapendekeza kukusanya shilingi 18,990,509,329,000/-
ambapo mapato ya kodi na yasiyo ya kodi shilingi
18,172,736,200,000/- sawa na asilimia 20 ya Pato la Taifa. Aidha,
mapato ya Halmashauri ni asilimia 0.9
ya pato la Taifa sawa na shilingi
817,773,129,000/-
SURA YA
MBADALA YA BAJETI 2016/17
|
MAELEZO
|
MAPATO KATIKA SHILINGI (TZ)
|
|||||
A
|
Mapato ya ndani ya Kodi na yasiyo ya kodi
|
18,172,736,200,000/-
|
|
|
|||
B
|
Mapatoya Halmashauri
|
817,773,129,000/-
|
|
|
|||
|
JUMLA MAPATO YA NDANI
|
|
18,990,509,329,000/-
|
|
|||
C
|
Mikopo na misaada ya mashart nafuu
|
383,002,000,000
|
|
|
|||
D
|
Misaada na
Mikopo ya miradi
|
2,745,659,000,000
|
|
|
|||
E
|
Misaada na mikopo ya Kisekta
|
372,147,000,000
|
|
|
|||
|
JUMLA YA MIKOPO NA MISAADA YA NJE
|
|
3,500,808,000,000/-
|
|
|||
|
|
|
|
|
|||
|
JUMLA YA MAPATO YOTE
|
|
|
22,491,317,329,000/-
|
|||
|
|
|
|
|
|||
|
MATUMIZI
|
|
|
|
|||
E
|
Matumizi ya Kawaida
|
|
15,410,000,000,000/-
|
|
|||
|
(i).Deni miradi
ya maendeleo
|
8,000,000,000,000/-
|
|
|
|||
|
(ii).Mishahara
|
6,600,000,000,000/-
|
|
|
|||
|
(iii) Matumizi
mengineyo
|
|
|
|
|||
|
|
360,000,000,000/-
|
|
|
|||
|
|
450,000,000,000/-
|
|
|
|||
|
|
|
|
|
|||
H
|
Matumizi ya Maendeleo
|
|
7,081,317,329,000/-
|
|
|||
|
|
2,478,461,065,150/-
|
|
|
|||
|
|
1,982,768,852,120/-
|
|
|
|||
|
|
1,203,823,945,930/-
|
|
|
|||
|
|
849,758,079,480/-
|
|
|
|||
|
|
566,505,386,320/-
|
|
|
|||
|
JUMLA YA MATUMIZI YOTE
|
|
|
22,491,317,329,000/-
|
|||
Mheshimiwa
Spika, Bajeti Mbadala ya Kambi Rasmi ya
Upinzani inategemea misaada toka kwa nchi wa hisani na kwa mashirika ya kimataifa (utegemezi) kwa
16% tu na tunaamini kwa mazingira mazuri yakiendelea kuwekwa bila ya kuwa kero
kwa wadau wa sekta mbalimbali, na pia kuondoa mchwa wanaokula fedha za miradi
katika halmashauri, ni dhahiri kwa miaka miwili ijayo tungeweza kujitegemea.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani
imekuwa inatilia mkazo juu ya ukuzaji uchumi vijijini (Rural Growth) na hivyo
kuwa ni kipaumbele cha kwanza katika Bajeti zake Mbadala. Vivyo hivyo kwa mwaka
huu imetenga 35%. Tunaamini kabisa kuwa ili Tanzania tuwe na uchumi wa viwanda
ni lazima miundombinu ya barabara kutoka pembezoni mwa wilaya zetu, maji na
nishati viwe ni vya uhakika, kwa njia hiyo hata uhamiaji wa vijana kutoka
vijijini kuja mijini utapungua kabisa kwani wawekezaji watafungua viwanda vya
uzalishaji na hata kilimo cha uhakika kitafanyika kwani masoko yatakuwa na
uhakika vile vile.
Mheshimiwa
Spika, Kipaumbele cha pili ni kwenye huduma
za jamii ambazo kwa muktadha wetu ni elimu, afya na maji kwa ajili ya matumizi
ya majumbani, ambapo Bajeti Mbadala imetenga 28% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Kipaumbele cha tatu ni Miundombinu
kwa maana ya Barabara za kuunganisha wilaya na wilaya, usafiri wa reli, usafiri
wa ziwani n.k na imetengewa 17% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Kipaumbele cha nne ni kwenye
usimamizi wa ardhi, kwani tumeshindwa kutumia fursa ya ardhi yetu kukuza
uchumi, na kwakuwa tulipendekeza uwepo wa chombo cha kusimamia na kuratibu
sekta nzima ya majengo (Real estate regularatory authority-Rera) na
pia kuhakikisha kuwa kodi za ardhi zinalipwa kwa utaratibu unaoeleweka, hivyo
basi, imetengwa 12% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, kipaumbele cha tano na cha mwisho
ni kuwekeza katika sekta ya utalii, kwani sekta hii ndiyo itakayoleta fedha za
kigeni na kwa muda mfupi kama tutapunguza vikwazo vinavyopunguza idadi ya
watalii wanaoingia na kukaa nchini kwa muda mfupi. Hivyo basi,bajeti mbadala imetenga 8% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya
Upinzani haikopi mikopo ya kibiashara kwani mikopo ya kibiashara hasa kwa
mabenki ya ndani ndio chanzo kikuu cha kuua sekta binafsi hapa nchini. Hivyo
basi kwa kuliona hilo bajeti mbadala ni bajeti ya kuweka mazingira wezeshi kwa
wajasiliamali wa ndani na nje kuwekeza maeneo ya vijijini kwa sekta zote za
uchumi.
24. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa
kusema kwamba, Serikali hii ya awamu ya tano imeanza vibaya muhula wake
wa uongozi kwa kulidanganya bunge kwa kuleta bajeti yenye takwimu
zinazokinzana. Serikali imeeleza katika bajeti yake kwamba inakusudia kukusanya
na kutumia shilingi trilioni 29.539 lakini
cha ajabu ni kwamba vitabu vya mapato vinaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni 22.063 na cha ajabu
zaidi vitabu vya matumizi vinaonyesha
kwamba Serikali itatumia shilingi
trilioni 23.847 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya shilingi trilioni 1.784 nje ya makusanyo.
Mheshimiwa Spika, Ukichukua
jumla ya bajeti yote iliyotajwa na Serikali ya shilingi trilioni 29.539 ukatoa jumla ya makusanyo halisi ya shilingi trilioni 22.063 utapata
tofauti ya shilingi trilioni 5.476 ambazo
haziko kwenye makusanyo wala haziko kwenye matumizi. Ukichukua tofauti hiyo ya shilingi trilioni 5.476 ukajumlisha na shilingi trilioi 1.784 ambazo ziliingizwa kwenye matumizi nje ya
makusanyo utapata jumla ya shilingi
trilioni 7.26 ambazo hazimo katika makusanyo halisi ya Mapato.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani imetafakari kina jambo hili na kufikia uamuzi kwamba;
Serikali imelihadaa bunge na wananchi kwa kuliaminisha Bunge na wananchi kwamba
ina bajeti ya shilingi trilioni 29.539
wakati ki-uhalisia Serikali hii ya awamu ya tano ina bajeti ya shilingi
trilioni 22.063 tu ikiwa ni pungufu ya shilingi
bilioni 432 ukilinganisha na shilingi
trillioni 22.495 za bajeti ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
David Ernest Silinde (Mb)
NAIBU WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA
KAMBI RASMI YAUPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA
YA FEDHA NA MIPANGO
10 Juni, 2016
Post a Comment: