Friday, 6 May 2016



Kitu ambacho hukijui ni kama sawa na usiku wa giza, mara nyingi huwa hakisumbui ni kama hakipo vile, hapo unakuwa ujinga na ujinga sio kilema ukipata elimu ujinga unaisha unakuwa mwerevu na kukielewa kile ambacho ulikuwa hukijui.

Hapo kabla ya elimu ya ulipaji kodi ilikuwa ikitolewa lakini haikuwa kwa kiwango cha sasa na ambacho kimejaa ubunifu. Tatizo halikuwa watu kutolipa kodi, tatizo lilikuwa njia ya kufikisha elimu ya mlipaji kodi katika njia inayostahili.

Wengi hawakufahamu umuhimu wa kulipa kodi, na hasara za kutolipa kodi, unaweza ukakwepa kulipa kodi sasa hivi lakini unamuharibia mtu ambaye ataishi baadae akiwemo mtoto wako mwenyewe.Ukilipa kodi Serikali itaweza kuboresha elimu, Miundombinu ya barabara, huduma za afya n.k, Mtanzania mwenzako anapokosa huduma nzuri za afya kwa sababu watu wamekwepa kulipa kodi tunajirudisha nyuma wenyewe na kujiua, sawa na mbwa mwitu aliyejing'ata mwenyewe anakula damu yake akidhani sio damu yake mpaka anakufa.

Chini ya Uongozi mpya wa Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata zimeonekana jitihada kubwa zinazofanywa katika kuhakikisha elimu ya kulipa inamfikia kila mwananchi kote nchini, vijijini na mijini.

Kwa sasa yameonekana matokeo makubwa ya hali ya ulipwaji kodi kwa mwezi Aprili 2016 kwa kukusanywa kiasi cha Trilioni 1.035 ikiwa ni mapinduzi katika ukusanyaji wa mapato hapa nchini.

Kuna uwezekano mkubwa chini ya usimamizi wa Kamishna Mkuu wa Serikali Bw. Kidata mapato yakaongezeka kwa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya kodi na kuendelea kutoa elimu kwa upana wake.

TRA imedhamiria kukusanya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.4 ili kufikia na kuvuka lengo la mwaka 2015/16 ambalo ni Shilingi Trilioni 12.3 na inawezekana, kama huamini utasikia mapato ya Mwezi Mei na Juni 2016 yatakuwa juu hivyo kufanya kufikia na kuvuka lengo hii ni kutokana na ufahamu mkubwa walioupata wananchi baada ya kutolewa elimu kwa kiasi kikubwa.

Manunuzi yeyote mwananchi unayoyafanya dai risiti, hapo utakuwa umelipa kodi na kuiwezesha Serikali kuleta maendeleo.

Vituo vya televisheni, redio,magazeti mitandao ya kijamii, vipeperushi kwa kiasi kikubwa vimesaidia kutoa elimu ambayo wananchi wamepata uelewa wa kutosha, sasa wanalipa kodi, Serikali inapata Mapato tayari kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Na kadiri ya siku zitakavyokuwa zikienda mabadiliko zaidi yatajitokeza katika kugundua njia rafiki za ulipaji kodi bila kuumiza upande wowote aidha Serikali au mwananchi.







Post a Comment: