HATUNA HURUMA NA WAZEMBE - MH KASSIM MAJALIWA

WAKATI Rais Dk. John Magufuli akisisitiza zoezi endelevu la utumbuaji majipu kufanyika hadharani bila kificho, pigo jingine kwa waliotumbuliwa na wanaosubiri kutumbuliwa, limetangazwa.
Akisoma Mwelekeo wa Kazi za Serikali bungeni jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mbali na kusisitiza kuendelea kushughulikia watendaji wazembe, wabadhirifu na wavivu, alitangaza kuwa Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi imeanzishwa katika Mahakama Kuu na itaanza kazi zake Julai mwaka huu.
Miongoni mwa wanasiasa waliojitokeza kulalamikia hatua ya watuhumiwa hao kuchukuliwa hatua ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Edward Lowassa.
Mahakama ya RushwaMahakama hiyo ni moja ya ahadi zilizonadiwa na Dk. Magufuli katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, akifafanua katika Hotuba ya Ufunguzi wa Bunge na kuirejea wakati wa uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria Duniani.
Akitangaza kukamilika kwa mchakato huo jana, Waziri Mkuu Majaliwa alisema: “Napenda kuliarifu Bunge kwamba Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi Julai, 2016.”
Uharaka wa kesiMbali na kuanza kufanya kazi kwa mahakama hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa pia alisema kuwa Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili ziharakishe utoaji wa haki.
Uimarishwaji wa ofisi hizo pia unatokana na agizo la Rais Magufuli alilotoa siku hiyo ya uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria Duniani, alipotaka kesi za uhujumu uchumi na ufisadi ziendeshwe kwa kasi, ili jitihada za Serikali za kupambana na matatizo hayo, ziweze kuzaa matunda.
Utumbuaji kuendeleaKatika hotuba hiyo ya Majaliwa, iliyokwenda sambamba na makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema Serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote ambao hawataendana na Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, lakini akasisitiza kwamba serikali itachukua hatua kwa kuzingatia na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Akizungumzia utekelezaji wa Sera ya Utoaji Elimu Bure kuanzia Darasa la Kwanza hadi Kidato cha Nne, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ipo changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha watoto shule bila malipo.
Kutokana na hilo, aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini waliokamata mbao kutokana na makosa mbalimbali kutozipiga mnada mbao hizo na badala zitumike mara moja kutengeneza madawati na pia halmashauri kutumia rasilimali zake kutengeneza madawati kwa kila shule.
Post a Comment: