VIJANA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wametakiwa kujizatiti zaidi kulinda na kuendeleza Mapinduzi ya mwaka
1964 na Muungano uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu
ndiyo hazina na rasilimali kubwa waliyoachiwa na viongozi na waasisi wa
Taifa la Tanzania, Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume.
Mwito huo umetolewa na Makamu
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wakati alipozungumza na
viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa kichama wa Mjini
Unguja ikiwa ni sehemu ya ziara ya kuangalia maendeleo ya jumuiya
mbalimbali za chama hicho Visiwani.
Alibainisha kuyalinda na kuyadumisha
Mapinduzi na Muungano ni kulinda na kuendeleza amani na utulivu nchini
hivyo vijana hilo ndilo jukumu lao la msingi kama warithi wa taifa, na
kusema chama kilichoonesha nia ya kuyadumisha mambo yote ya msingi
yaliyoachwa na waasisi wetu ni Chama Cha Mapinduzi.
“Hakuna mbadala wa
Mapinduzi, hakuna mbadala wa Muungano wala hakuna mbadala wa amani na
utulivu wa nchi yetu hivyo ni lazima vijana mchukue nafasi yenu kulinda
misingi hiyo ya nchi yetu kwani baadhi ya vyama vya siasa havina nia
kama hiyo ya Chama Cha Mapinduzi cha kulinda urithi huo,” alisisitiza Dk Shein.
Alisema kazi kubwa iliyofanywa na
waasisi hao wakati huo wakiwa vijana matunda yake yameonekana kwa hivyo
aliwataka vijana wa sasa kufanya kazi kwa bidii na kuyaenzi mambo yote
mazuri waliyoachiwa kwa faida ya kizazi kijacho katika kupiga hatua
kubwa ya maendeleo na kupambana na umasikini.
Post a Comment: