CUF WAIJIBU ZEC BAADA YA KUJUMUISHWA KATIKA UCHAGUZI WA MARUDIO ZNZ
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema taarifa iliyotolewa jana na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ya kutotambua uhalali wa kujitoa kwa baadhi ya wagombea katika uchaguzi wa marudio, haitaathiri msimamo wa chama hicho Baadhi ya viongozi wa CUF jijini Dar es Salaam , wamesema kutoshiriki kwao uchaguzi wa marudio ni halali, wala hawajavunja sheria na katiba kama alivyosema Jecha. Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Umma wa CUF Taifa, amesema Jecha anajaribu kuudanganya umma kwa kutumia vifungu vya sheria na katiba ambavyo havina uhalisia wa anachokisema. “Katiba inasema mgombea ana haki ya kugombea na kujitoa katika uchaguzi kama hataki kugombea na si kumlazimisha kugombea kwa masilahi ya kundi fulani,” amesema Kambaya. “Wagombea wa CUF hawajitoi kwenye uchaguzi sababu uchaguzi walishafanya tarehe 25 Oktoba mwaka jana, ila tume ikatumia ujanja kuufuta na kulazimisha kurudiwa kwa uchaguzi,” amesema Kambaya. “Uchaguzi wa marudio hatuutambui sababu umekiuka sheria, tume haina mamlaka ya kufuta matokeo ya uchaguzi wote, bali wana mamlaka ya kufuta uchaguzi katika baadhi ya maeneo kama kulikuwa na dosari,” amesema. Amesema kama kulikuwa na makosa ilitakiwa chama chenye malalamiko kwenda mahakamani kupinga matokeo na si tume kuingilia kati na kuufuta uchaguzi kiholela. Kambaya amesema CUF haina sababu ya kwenda mahakamani kuapa kutoshiriki uchaguzi kwani hawakujaza fomu ya kushiriki uchaguzi wa tarehe 20 Machi, bali walijaza fomu ya kushiriki uchaguzi wa 25 Oktoba mwaka jana.
Post a Comment: