Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imevipa
siku saba vyama 14 vya siasa kuthibitisha kama vitashiriki uchaguzi wa
marudio utakaofanyika Machi 20 mwaka huu.
Vyama hivyo, kikiwamo cha CUF, ndivyo
vilivyosimamisha wagombea wa nafasi za urais, uwakilishi na udiwani
katika majimbo 54 Unguja na Pemba katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka
jana, kabla ya matokeo kufutwa na ZEC.
Uchunguzi wa Nipashe mjini Zanzibar
umebaini kuwa wagombea wote tayari wamepewa mwongozo kupitia barua ya
Januari 25, mwaka huu, na kutakiwa kuthibitisha kama vitashiriki
uchaguzi wa marudio kuanzia kesho hadi Februari 11, mwaka huu.
Mwongozo huo umetolewa na Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, na unavitaka vyama hivyo kuthibitisha ushiriki wao kwa maandishi.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa tarehe ya
kufanyika uchaguzi imetangazwa rasimi katika gazeti la serikali tangu
Januari 29, mwaka huu.
Mbali na wagombea katika majimbo, ZEC
imewataka pia wagombea wa viti maalumu kukamilisha kuthibitisha kama
watashiriki hadi ifikiapo Febuari 11 lakini hakutakuwa na kampeni kwa
wagombea.
Salum katika barua yake hiyo alisema
kazi ya kupiga kura na kuhesabu pamoja na kutangaza matokeo itakamilika
ndani ya siku tatu.
“Kazi ya kutangaza matokeo itafanyika Machi 23, mwaka huu,” imeeleza sehemu ya waraka huo.
Akizungumza Mkurugenzi huyo wa ZEC, alithibitisha kutolewa mwongozo wa kushiriki uchaguzi wa marudio visiwani humo.
Wakati ZEC ikitoa mwongozo huo,
kumetokea mgawanyiko mkubwa miongoni mwa vyama vilivyosimamisha wagombea
katika uchaguzi uliyofutwa matokeo yake.
Vyama 10 vimeunda ushirikiano na
Mwenyekiti wake ni Kassim Ali Bakar Ali ambaye ni mgombea urais kupitia
chama cha Jahazi Asilia. Alisema wanatarajia kukutana leo kujadili na
kutoa msimamo kama watashiriki uchaguzi huo wa marudio au la.
Alisema ajenda kubwa ya kikao hicho ni
kujadili waraka wa tume wa kuwaarifu kurudiwa kwa uchaguzi lakini baadhi
ya viongozi wa vyama vitatu ambao ni wagombea, walikanusha kuhusika
katika mpango huo. Vyama hivyo ni TLP, SAU na CCK.
Vyama 10 vinavyounda umoja huo ni Jahazi Asilia, NRA, Chauma, TLP, SAU, CCK, ACT- Wazalendo, DP, CCK na Demokrasia Makini.
Viongozi waliokanusha kuwemo katika
ushirikiano huo Naibu Katibu Mkuu wa CCK, Ali Khatibu Ali; Makamu
Mwenyekiti wa SAU, Issa Mohamed Zonga, na Makamu Mwenyekiti wa TLP
Zanzibar, Hafidh Hassan Suleiman, ambao pia ni wagombea wa urais wa
Zanzibar
Hata hivyo wagombea urais, Juma Ali
Khatib (TADEA) na Soud Said Soud (AFP) walisema kuwa wametengwa katika
umoja huo.“Sifahamu kwa nini tumetegwa katika umoja huo wa vyama lakini
sisi tutatoa msimamo wa kushiriki baada ya kufanyika kikao cha
Halmashauri Kuu ya TADEA mwezi huu,” alisema Khatib.
Soud alisema chama chake kinajipanga
kuingia katika uchaguzi baada ya kupokea rasmi barua ya tume ya kutakiwa
kuthibisha ushiriki kabla ya Febuari 11, mwaka huu.
Taarifa za uchunguzi zilizopatikana
mjini Zanzibar zinasema Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi, ameanza kukutana na viongozi wa vyama kwa mafungu baada ya
kuwepo tishio la kususia uchaguzi kama ilivyotangaza CUF.
Viongozi wa vyama vitatu, CCK, Jahazi
na SAU wanadaiwa kukutana na Msajili na kuzungumza kwa kina juu ya
ushiriki wao katika uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, wagombea watatu
wametangaza kushiriki uchaguzi wa marudio. Wagombea hao ni Ali Khatib
Ali (CCK) Issa Mohamed Zonga (SAU) na Hafidh Hassan Suleiman ambao
walitangaza hatua hiyo jana.
“Sisi wagombea wa urais wa vyama vya
CCK, SAU na TLP tunatoa tamko rasmi kuwa tutashiriki uchaguzi wa
marudio,” alisema Ali wakati akisoma tamko la pamoja.
Aliwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha
amani na utulivu pamoja na kujitokeza kwa wingi wakati wa kupiga kura
na baada ya kukamilisha kazi hiyo, warudi nyumbani kusubiri matokeo.
Upande wake, CUF imesema imeanza kutengwa na tume tangu kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa
CUF, Omar Ali Shehe, alisema barua za mwongozo wa uchaguzi wa marudio
zilizotolewa na ZEC ilikuwa haijawafikia hadi jana.
Alisema pamoja na CUF kutoshiriki
uchaguzi huo, kama chama hawatakiwi kukatiwa mawasiliano ili wafahamu
kinachoendelea katika uchaguzi huo.
Alisema kutokana na hali hiyo,
wamewasilisha rasmi malalamiko kwa mkurugenzi wa uchaguzi juu ya
kunyimwa taarifa ya mchakato wa uchaguzi.
Wagombea wa urais wa Zanzibar walikuwa
14 ambao ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (CCM), Khamisi Iddi
Lila (ACT-Wazalendo) Juma Ali Khatib (TADEA), Hamad Rashid Mohamed
(ADC), Said Soud Said (AFP), Ali Khatib Ali (CCK) na Mohamed Masoud
Rashid (Chauma).
Wengine ni Maalim Seif Sharif Hamad
(CUF), Tabu Mussa Juma (Demokrasia Makini), Abdalla Kombo Khamis (DP),
Kassim Bakar Ali (Jahazi Asilia), Seif Ali Iddi (NRA), Issa Mohamed
Zonga (SAU) na Hafidh Hassan Suleiman (TLP).
Post a Comment: