CHAMA CHA NKURUNZINZA CHAUNGA MKONO JITIHADA HIZI ZA RAIS MAGUFULI
Tuesday, February 09, 2016
SERIKALI ya Burundi na chama tawala cha
nchi hiyo CNDD-FDD imewataka Watanzania kumuunga mkono Rais John
Magufuli katika azma yake ya kusimamia nidhamu ya viongozi na kuleta
maendeleo kwa taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Kibago mkoani Makamba
nchini Burundi, Juma Albert alitoa kauli hiyo akiongoza ujumbe wa watu
watano wa kiserikali na chama tawala cha nchini humo, waliohudhuria
maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
yaliyofanyika kimkoa kwenye kijiji cha Munzenze, wilayani Buhigwe mkoani
hapa.
Albert alisema, Serikali ya Burundi na
chama tawala cha CNDD- FDD imekuwa ikifuatilia mambo yanayofanywa na
Rais Magufuli na kwamba, wanamuunga mkono kwa yale anayofanya ambayo
yamekuwa na tija kwa uchumi wa Tanzania.Alisema,
Magufuli pia amekuwa akilenga kuimarisha uchumi wa nchi yake sambamba
na ustawi wa jirani zake ikiwemo Burundi. Pamoja na hayo viongozi hao
walitoa shukrani zao kwa wananchi wa Kigoma kuendelea kuwahifadhi ndugu
zao katika kambi mbalimbali za wakimbizi, kufuatia mapigano ya wenyewe
kwa wenyewe nchini mwao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo,
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Dk Walid Kabouorou aliwataka viongozi
wa upinzani kukubali kwamba uchaguzi umekwisha na CCM ndio mshindi.
Alisema, kutokana na hilo, hawana budi
kuungana na kutekeleza Ilani ya CCM kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo
iliyopangwa kutekelezwa inafanikiwa. Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa
Machibya aliwataka wananchi kupeleka watoto wao shule ili kuunga mkono
mpango wa Serikali wa kuondoa ujinga kwa Watanzania kutojua kusoma na
kuandika.
Alisema, kumekuwa na tabia ya kuwaficha
watoto walemavu na kuwanyima haki yao ya kupata elimu, hivyo aliitaka
jamii kuwafichua wote wenye kuendekeza ukatili huo dhidi ya wenye
ulemavu.
Post a Comment: