Monday, 25 January 2016

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA  USIMAMIZI WA MAZINGIRA-NEMC

 Katika kikao kilichoitishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba (Mb), tarehe 24 Januari 2016, mjini Dodoma kuhusu kuimarisha utendaji  ndani ya Baraza la Taifa la Hifadhi na  Usimamizi wa Mazingira-NEMC maamuzi yaliyofikiwa  ni kama ifuatavyo:
 1.     Kuhusu suala la kiwanda cha kusindika minofu ya punda Mkoani Dodoma, imegundulika kulikuwa na ukiukwaji  mkubwa, wa makusudi na wa wazi wa miiko ya kazi  kwa watumishi  wa NEMC  walioshughulika  na kiwanda hicho. Hivyo, Mhe. Makamba ameagiza  watumishi wa NEMC wafuatao wasimamishwe kazi mara moja:
a.     Dkt. Eladius Makene -Afisa Mazingira Mwandamizi,  
b.     Wakili  Heche Suguta Manchare - Mwanasheria  Daraja la  II
c.      Mhandisi Boniface Benedict  Kyaruzi, Afisa Mazingira
Hatua nyingine za kinidhamu na kisheria zitafuatia.
 2.     Vilevile, imebainika kwamba usimamizi wa watumishi wa NEMC siyo makini na thabiti na kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza. Hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Bonaventura Baya apewe barua ya onyo kali la mwisho kwa udhaifu  katika usimamizi wa watumishi wa Baraza.

3.     NEMC kama chombo muhimu nchini kilichopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya  Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira inatarajiwa kazi zake zifanyike kwa ufanisi wa kiwango cha juu kulingana na majukumu yaliyoko kwa mujibu wa Sheria. Hivyo, kwa mapungufu yanayojitokeza  Mhe.  Makamba, ndani ya wiki moja ataunda jopo la wataalamu wasiozidi watano ili kutathmini utendaji wa NEMC na changamoto mbali mbali katika usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kuishauri Serikali ipasavyo.
4.      Ili kuimarisha ufanisi na udhibiti wa utendaji wa NEMC, ndani ya wiki moja  litatolewa Tangazo litakalokuwa na mambo yafuatayo: Anwani ya barua pepe (email), Nukushi (fax), Namba ya simu, Namba ya Whatsapp ili mtu yeyote mwenye malalamiko au aliyewahi kuombwa rushwa ama chochote na watumishi wa NEMC ambacho ni kinyume na  maadili ya kazi yao atoe taarifa mara moja ili uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe.
5.     Kutokana na mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, ndani ya wiki moja,  NEMC ipitie upya orodha  ya wataalamu na taasisi elekezi zilizosajiliwa na kufuta wataalamu na taasisi zote ambazo zimekuwa zikikiuka maadili ya kazi zao likiwemo suala la kuwasilisha taarifa zilizo chini ya viwango, kuchelewesha kazi za wateja wao na kutowasiliana na wateja wao kuhusu hatua za utekelezaji wa maombi yao.
6.     Ndani ya wiki tatu uitishwe mkutano wa dharura wa Bodi ya NEMC kujadili na kufanya maamuzi juu ya changamoto za utendaji katika Baraza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016

Post a Comment: