Sunday, 24 January 2016

 
 KUSAFIRI NJE YA NCHI

Ndugu Membe anapotosha ukweli anaposema Tanzania sio kisiwa na kwamba Raisi na waziri wake wa mambo ya nje lazima wasafiri nje ya nchi watake wasitake.

Tunapenda kumfahamisha ndugu Membe kuwa, mh. Raisi Dr. John Magufuli hajatoa kauli kuwa yeye au wasaidizi wake hawatosafiri nje ya nchi katika safari za muhimu na zenye tija. Isipokuwa, muongozo wa mh. Rais kuhusu safari za nje unalenga kupunguza safari zile ambazo hazina ulazima na tija kwa taifa.

 

KUHUSU MGOGORO WA UCHAGUZI WA ZANZIBAR

Katika maelezo aliyonukuliwa na gazeti la Mwananchi, ndugu Membe alieleza kupinga kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi wa Zanzibar yakiwemo ya wawakilishi, na kwamba jambo hili limeihuzunisha dunia.

Kauli hii ya ndugu Membe inatushangaza na kutusikitisha sana. Kwanza tunajiuliza, Je, ikiwa sehemu kubwa ya uchaguzi iligubikwa na udanganyifu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi kinyume na sheria za uchaguzi wa Zanzibar, ni kwanini ndugu Membe ashangae uchaguzi wote  kufutwa na tume ya uchaguzi ZEC?

Tunamtaka ndugu Membe atueleze, ni dunia ipi hiyo inayotushangaa?

Ni kwanini dunia hiyo anayoitetea ndugu Membe haijashangaa kumuona maalim Seif Shariff Hamad akijitangaza kuwa mshindi kinyume cha sheria za uchaguzi?

Ndugu Membe anapaswa kushangaa, ni kwanini hadi leo hii maalim Seif Shariff Hamad hajakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kujitangaza kuwa mshindi kinyume cha sheria.

KUHUSU VIKAO VYA MARIDHIANO

Kuhusu vikao vya maridhiano vilivyokua vinaendelea, ndugu Membe amekosoa kitendo cha Raisi wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na maalim Seif Shariff hamad kuachwa wakazungumza wenyewe wawili.

Kwanza tunasikitika kuwa ndugu Membe huenda ama hajui kinachoendelea Zanzibar au ameamua kupotosha umma kwa makusudi. Hii ni kwasababu mazungumzo yaliyokua yakiendelea Zanzibar, hayakuwahusisha Dr. Shein na maalim Seif Shariff peke yao. Bali yalishirikisha marais wastaafu wa Zanzibar, Raisi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.

Pili, katika muafaka wa kisiasa wa Zanzibar wa mwaka 2009/2010 uliopelekea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kwa kiasi kikubwa ni maalim Seif Shariff hamad na Rais wa Zanzibar wa wakati huo mh. Amani Abeid Karume pekee walioshiriki mazungumzo.

 

RAI KWA NDUGU MEMBE

Mosi, tunapenda kumkumbusha ndugu Bernard Membe kuwa yeye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa amewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM. Hivyo anajua utaratibu wa Chama na anayo nafasi ya kuyasema mawazo yake juu ya uendeshaji wa serikali ndani ya vikao halali vya chama. Aidha, ndugu Membe kwa nafasi yake kama mjumbe wa NEC na waziri wa zamaniwa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa,  anayo nafasi ya kutoa ushauri na maoni yake moja kwa moja kwa Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mh. Dr. John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM taifa Dr. Jakaya Kikwete au kwa Katibu Mkuu wa CCM ndugu Abdulrahman Kinana. 

Kutotumia fursa hizo kutoa maoni yake ni kujishushia heshima mbele ya jamii.

 

Pili, tunamkumbusha ndugu Membe kuwa yeye sasa ni mstaafu aliyeitumikia nchi yake kwa muda mrefu na nafasi mbalimbali. Ni vema sasa akatoa fursa kwa viongozi wengine walioko madarakani kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia watanzania. Muda wake umekwisha na sasa ni busara akakaa kimya na kuchunga maneno yake.

 

Raisi mstaafu wa awamu ya tatu mh. Benjamin William Mkapa aliwahi kusema (nanukuu):-

 

"Siku moja mtoto mdogo aliwahi kuniuliza. Nani ni bingwa wa kuendesha shughuli za serikali? Nikatafakati sana swali lile, kisha baada ya muda nikamjibu…Ni mwanasiasa aliyestaafu kisha akachunga ulimi wake…"

MWISHO

Tunamshauri ndugu Membe kuuchukua ushauri huu wa Raisi mstaafu Benjamin Mkapa, utamsaidia. Aidha tunamtaka afahamu kwamba watanzania wana imani kubwa na juhudi zinazofanywa na serikali katika kupunguza matumizi, kuziba mianya ya rushwa, ukwepaji kodi na ubadhirifu wa mali za umma. Wakati huu si wa kupika majungu, fitina wala ubabaishaji. Ni wakati wa kuungana pamoja kama taifa na kuchapa kazi tu.

Asanteni.

 

Imetolewa na ndugu

ALLY S. HAPI

KATIBU WA IDARA,

ELIMU, UTAFITI NA UONGOZI,

SHIRIKISHO LA VYUO VYA ELIMU YA JUU TANZANI

Post a Comment: