KIGOGO MWINGINE WA SERIKALI ASOMBWA NA KASI YA RAIS MAGUFULI,KISA RUSHWA TU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) mkoani Katavi inamshikilia Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa
Kawajense, Manispaa ya Mpanda Catherine Kipeta kwa tuhuma za kuomba na
kupokea rushwa ya Sh 30,000.
Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa
Katavi, Christopher Nakua alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari
18, mwaka huu katika eneo la Mtaa wa Kawajense baada ya kuandaliwa
mtego ambao ulifanikisha kukamatwa kwake.
Alisema mtuhumiwa alikamatwa kufuatia
Ofisi ya Takukuru kupokea taarifa kutoka kwa mlalamikaji kuwa Ofisa
Mtendaji huyo anamuomba rushwa kiasi cha Sh 30,000 ili asimpeleke kwenye
Baraza la Kata kwa kosa la kufungua sehemu yake ya biashara wakati ni
muda wa kufanya usafi na kutokushiriki kufanya usafi.
Ilidaiwa kuwa baada ya kupokea taarifa
hizo ofisi ya Takukuru ilifanya uchunguzi na baada ya kuridhika na
maneno ya mlalamikaji ndipo mtego ulipoandaliwa na mtuhumiwa kukamatwa.
Kamanda Nakua alisema mtuhumiwa huyo
anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazomkabili ambazo ni
kuomba rushwa ya fedha taslimu Sh 30,000, shtaka la pili litakuwa ni
kupokea rushwa ya Sh 30,000 kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) cha
sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Na 11 ya mwaka 2007.
Post a Comment: