ZAWA NAKO HALI TETE,BALOZI SEIF ALI IDDI AAGIZA UCHUNGUZI UFANYIKE HARAKA
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwasili mtaa wa Mlandege
kukagua kiwanja cha nyumba ya Ghorofa kinacholalamikiwa na Wakaazi wa
Mtaa huo kwamba kimevamia pia eneo la wazi linalotumika kwa shughuli za
Kijamii.
Mmiliki
wa Kiwanja cha nyumba ya Ghorofa Mlandege Bwana Anuari Abdullah
akijitetea kupata kibali kinachomruhusu kuendeleza ujenzi wa nyumba
yake.
Baadhi
ya Wakaazi wa Mtaa wa Mlandege wakitafakari na kufurahia maamuzi
yaliyochukuliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ya
kuzuia ujenzi wa jengo la Ghorofa kwa kukosa taratibu zinazozingatia Mji
mkongwe wa Zanzibar.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemuagiza
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kufanya uchunguzi wa
kina na kuwachukulia hatua za nidhamu kwa mujibu wa sheria watendaji wa
Mamlaka hiyo wanaotumia dhamana yao katika kusimamia huduma za maji kwa
njia ya kuwanyanyasa Wananchi.
Alisema zipo dalili za wazi zinazoonyesha kwamba baadhi ya
Watendaji wa Mamlaka hiyo wanatekeleza majukumu yao ya kazi kwa
kuendesha utashi wao binafsi zaidi wa kisiasa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati akiwapa pole
Wananchi wa Shehia ya Dole Wilaya ya Magharibi “B” mara baada ya kukagua
mifereji ya huduma za Maji safi na Salama ya wananchi wa Shehia hiyo
ambayo ilikatwa na mengine kung’olewa kabisa vianzio vyake kufuatia
operesheni iliyofanywa na watendaji wa Mamlaka hiyo.
Opereshi hiyo ya Tarehe 22 Oktoba iliyoathiri nyumba 24 zenye
familia 22 ililalamikiwa na Wananchi hao kwa vile ilitekelezwa siku
mbili tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Tarehe 25 Mwezi Oktoba mwaka huu
ikionyesha wazi kuwa baadhi ya watendaji wa Mamlaka hiyo waliweka utashi
wao wa Kisiasa.
Balozi Seif alisema Tabia iliyofanywa na baadhi ya Watendaji hao
wa Zawa ya kuendesha operesheni hiyo kwa kumsingizia yeye ndie
aliyeagiza kutekelezwa ilikuwa na lengo la kumchafua kisiasa.
Alisema hilo ni jambo linaloonekana kupangwa maalum ndani ya
kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu ambalo si vyema likachanganywa
pamoja kati ya huduma za Kijamii na itikadi za Kisiasa.
Akiwapa pole Wananchi hao wa Dole kwa kukosa huduma za maji safi
aliwataka watendaji wa Mamlaka ya Maji kuhakikisha kwamba huduma hiyo
katika Shehia ya Dole inarejeshwa tena kama kawaida ndani ya kipindi cha
wiki mbili zijazo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr.
Mustafa Garu aliahidi kutekeleza agizo hilo na kuwaeleza Wananchi hao
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachokifanya kwao ni kuwataka
wachangie huduma za Maji safi na salama ili kuiwezesha Mamlaka hiyo
ipate nguvu zaidi za kuimarisha miundo mbinu yake.
Alisema takwimu ziko wazi zikionyesha kwamba Serikali Kuu imekuwa
ikibeba gharama za upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama kwa
zaidi ya asilimia 65% wakati punguzo lililobaki la asilimia 35% tu
huomba kuchangiwa na Wananchi.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amemuagiza Mmiliki wa Kiwanja kinachotaka kujengwa Nyumba ya
Ghorofa katika Mtaa wa Mlandege Bwana Anuari Abdulla kusitisha mara moja
ujenzi huo.
Hatua hiyo ya Balozi Seif imekuja kufuatia malalamiko makubwa
yaliyotolewa na wakaazi wa Mtaa huo wakimshutumu Mmiliki huyo kuvamia
pia eneo la wazi { Open Space } la shughuli za kijamii katika sehemu
hiyo.
Balozi Seif alimuonya Mmiliki huyo kwamba endapo ataendelea
kukaidi agizo alilopewa na Mamlaka Nne zinazosimamia na kushughulikia
masuala ya Ujenzi Serikali italazimika kumchulia hatua za kisheria dhidi
yake.
Alifahamisha kwamba wakaazi wa Mtaa wa Mlandege ambao wanaishi
ndani ya eneo la Mji Mkongwe lililopata hadhi ya kuwa Urithi wa
Kimataifa wanapaswa kuzingatia matakwa yaliyokubalika katika uhifadhi wa
Mji huo wa Kihistoria.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji
Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alimueleza Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar kwamba Mmiliki wa kiwanja hicho amekuwa akikaidi
maamuzi anayopewa kuyatekeleza na mamlaka husika katika ujenzi huo.
Nd. Sarboko alisema Bwana Anuari ameamua kuendeleza ujenzi huo kwa
kutumia kibali alichopewa na Mmoja wa Afisa wa Baraza la Manispaa
ambacho tayari kimeshafutwa kwa vile kinakiuka na kutozingatia sheria na
taratibu zilizowekwa.
Alisisitiza kwamba Mmiliki huyo tayari ameshaonywa na Viongozi wa
Taasisi Nne waliokutana kujadili suala hilo na kumtaka asubiri maamuzi
ya pamoja yatakayotolewa baada ya kuzingatia hali halisi ya namna
yatakavyozingatia matakwa na haki ya kila upande unaohusika.
Alimtaka Mmiliki huyo kuhakikisha kwamba mabati yaliyowekwa
kufunga eneo la wazi lililokuwa likitumika kwa wapita njia pamoja na
kutumika kwa shughuli za Kijamii anayaondoa mara moja vyenginevyo
watendaji wa Mamlaka hiyo watalazimika kutekeleza amri hiyo kwa kutumia
kijiko katika kipindi kifupi kijacho.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
10/12/2015.



Post a Comment: