MO DEWJI FOUNDATION YATOA MSAADA WA MIL. 110/- KWA TAASISI INAYOWASAIDIA WATOTO WENYE KANSA YA TUMAINI LA MAISHA
Meneja
Mwendeshaji wa Taasisi ya MO Dewji, Francesca Tettamanzi (kulia) akitoa
neno la ukaribisho kwa uongozi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha
inayohudumia watoto wenye kansa nchini na waandishi wa habari katika
hafla fupi ya kukabidhi msaada wa fedha kwa ajili ya watoto wenye kansa
iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za MeTL Group jijini Dar
es Salaam. Wa pili kulia ni Mmoja wa Wakurugenzi wa Taasisi ya Tumaini
la Maisha, Gerard Mongera na Wa pili kushoto ni Ofisa anayesimamia
utekelezaji wa Programu wa Taasisi ya Tumaini la Maisha , Lilian
Ndyetabula.
Afisa
Mahusiano wa Taasisi ya MO Dewji, Zainul Mzige (kulia) akisoma taarifa
kuhusu madhumuni ya kuanzishwa kwa MO Dewji Foundation pamoja na kazi
wanazofanya katika kusaidia jamii ikiwemo sekta ya Afya na Elimu.
Meneja
Mwendeshaji wa Taasisi ya MO Dewji, Francesca Tettamanzi (kulia)
akikabidhi mfano hundi ya Shilingi Milioni 110 kwa Mjumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha inayohudumia watoto wenye
kansa nchini, Gerard Mongera (wa pili kushoto) kwa ajili ya kusaidia
watoto wenye kansa wanaopata matibabu yao katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili. Kushoto ni Ofisa anayesimamia utekelezaji wa Programu wa
Taasisi ya Tumaini la Maisha inayohudumia watoto wenye kansa nchini,
Lilian Ndyetabula.
Pichani
juu na chini baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali
waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi
za MeTL Group jijini, Dar es Salaam.
Taasisi
isiyo ya kiserikali ya MO Dewji iliyo chini ya makampuni ya Mohammed
Enterprises (MeTL Group) inayojishughulisha na kusaidia jamii imetoa
msaada wa Shilingi Milioni 110 kwa taasisi ya Tumaini la Maisha ambayo
inajihusisha na kuwasaidia watoto wenye kansa kupata matibabu pamoja
kuwahudumia kwa kipindi chote wanachokuwa katika matibabu.
Akizungumzia
msaada huo, Afisa Mahusiano wa MO Dewji Foundation, Zainul Mzige
alisema kuwa MO Dewji Foundation imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa
watoto ambao wanagundulika kuwa na kansa kuja Dar es Salaam kupata
matibabu na msaada ambao wameutoa wanataraji kuwa utatumiwa vizuri na
taasisi hiyo ili kuzidi kusaidia watoto.
Alisema
wameshafanya kazi nyingi na Taasisi ya Tumaini la Maisha na
wanawatambua katika utendaji wao wa kazi kusaidia watoto ambao wana
kansa na msaada huo wa milioni 110 wanataraji utakuwa na faida kubwa kwa
kutumika kusaidia watoto waliopo mikoani na hapa Dar ambao wanakutwa
wakiwa na kansa na hivyo msaada huo utasaidia kuokoa maisha ya
watanzania wengi.
“MO
Dewji tumekuwa tukisaidia miradi mbalimbali ya kijamii na kama jinsi
tunavyosaidia katika miradi hiyo na leo tunafuraha kutoa Shilingi
Milioni 110 za kitanzania kwa Tumaini la Maisha tunaamini ni shirika
linalotoa matumaini mapya kwa wagonjwa na familia zao,
“Tumekuwa
tukishirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kijamii tunafahamu ni
jinsi gani wanavyosaidia watoto wenye kansa na kama jinsi tulivyokuwa
tunashirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kimatibabu na leo
tunatoa msaada mwingine ili kuwawezesha kuzidi kuwasaidia watoto hao,”
alisema Mzige.
Aidha
Mzige alisema kuwa MeTL Group kupitia kwa MO Dewji Foundation
wanatambua ni jinsi gani serikali imekuwa ikipambana na ugonjwa huo kwa
kuwasaidia watoto wenye kansa na wao wanaahidi kuendelea kuwasaidia kwa
kutoa misaada kwa watoto wenye kansa ili waweze kupata matibabu na
kuokoa maisha yao.
Awali
Afisa Mahusiano huyo alisema kuwa Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni
ya MeTL Group, Mohammed Dewji aliamua kuanza kuwasaidia watoto wenye
kansa baada ya kukutana na mtoto wa miaka 7 aliyetambulika kwa jina la
Zakia mwaka 2012 wakati akiwa mbunge wa Singida Mjini ambaye alikuwa
akisumbuliwa na kansa ambayo ilikuwa imeshasambaa mwili mzima.
Mzige
alisema Dewji baada ya kukutana na mtoto huyo alimchukua na kumpeleka
hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu lakini walikuwa
wameshachelewa kutokana na kansa kusambaa mwilini na hivyo mtoto huyo
kupoteza maisha hali ambayo ilimfanya Dewji kujitoa kusaidia watoto
wenye kansa ili waweze kupata matibabu na kwa mapema kabla kansa
haijasambaa zaidi.
Nae
Gerard Mongera ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya
Tumaini la Maisha aliishukuru MO Dewji Foundation kwa msaada ambao
wanaowapatia kwa kipindi chote ambacho wamekuwa wakishirikiana na
kuitaja MO Dewji kama taasisi ambayo imekuwa ikiwasaidia zaidi hivyo
kuwa na matarajio ya kuzidi kushirikiana
Mongera
alisema msaada umetolewa na MO Dewji Foundation utatumika kuwasaidia
watoto hao kupata matibabu na chakula kwa watoto wanaoumwa kansa walio
katika hosteli za taasisi hiyo na walezi wanaowasimamia watoto hao kwa
kuwanunulia chakula na mahitaji mengine muhimu ambayo yanahitajika kwa
watoto hao.
“Tumekuwa
tukishirikiana kwa muda mrefu na MO Dewji Foundation na natumia fursa
hii kuwashukuru kwa msaada wanaotupatia wamekuwa wakitusaidia kwa muda
mrefu na tunawaomba wazidi kuwa na moyo huo wa kuwasaidia watoto wenye
kansa ambao wengi wao wanatoka mikoani na kwa kusaidiana nao tunaamini
tutaweza kuwasaidia watoto wengi zaidi,” alisema Mongera.
Mongera
aliongeza kuwa tangu mwaka 2013 walipoanza kufanya kazi na MO Dewji
Foundation wamefanikiwa kuokoa zaidi ya asilimia 50 ya maisha ya watoto
ambao wamekutwa na kansa na kutumia fursa hiyo kuyaomba makampuni
mengine pamoja na watu binafsi kujitokeza kuisaidia taasisi hiyo ili
kuwa na uwezo zaidi ya kuwahudumia watoto ambao wanakuwa wanasumbuliwa
na kansa.
CHANZO : Modewjiblog
Post a Comment: