Madiwani CCM GEITA washindwa kusoma kiapo
KATIKA hali ya kushangaza Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya
ya Geita juzi liligeuka kituko baada ya madiwani wanne kati ya 49 wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kusoma kiapo kwa ufasaha.
Hali hiyo ilisababisha vicheko kutawala katika ukumbi wa halmashauri walimokuwa wanaapishwa madiwani hao.
Tukio hilo lilitokea saa 11:32 asubuhi muda mfupi baada ya mwenyekiti
wa muda wa kikao hicho, Gaspar Kanyairita kufungua na hakimu mkazi,
Joseph Wiliam kuanza zoezi la kuwaapisha madiwani hao.
Madiwani walioshindwa kusoma kiapo na kata zao kwenye mabano ni Heche
Mathias (Nyakagomba), Khadija Joseph (Nyamigota), Daud Simeo (Nyamboge)
na Sele Juma Isene (Nyamwilolelwa).
Mkuu wa wilaya ya Geita, Omari Mangochie na Mbunge wa Geita, Joseph
Musukuma hawakuweza kuvumilia hali hiyo na kujikuta wakiangua kicheko
cha nguvu ambacho pia kilipokewa na wageni waalikwa na kusababisha
ukumbi mzima kuzizima kwa kicheko wakati Diwani wa Kata ya Nyamboge
akiapa kwa tabu mithili ya mwanafunzi wa shule ya awali.
Kutokana na hali hiyo, zoezi hilo la uapishwaji lilichukua muda mrefu kukamilika huku ukumbi mzima ukizidi kuzizima kwa vicheko.
Baadhi ya wananchi walishangazwa na hatua hiyo, ambapo mmoja wao
alisikika akisema kutokana na baadhi ya madiwani kutokujua kusoma na
kuandika kutazorotesha maendeleo yao.
“Kama diwani hajui kusoma hivi hapa wananchi waliomchagua watarajie
maendeleo kweli au ndiyo wamejikaanga kwa mafuta yao…diwani kama huyu
(anamtaja) anawezaje kukwepa kupitisha mikataba mibovu…hakika hii ni
kali,’’ alisikika mwananchi mmoja aliyekuja kushuhudia viapo vya
madiwani hao.
Post a Comment: