Katibu Mkuu Kiongozi awaasa watanzania kuzingatia Maadili katika Utumishi
Watanzania wameaswa kuzingatia
Maadili ya Kitaifa ambayo ni kiini cha kuboresha na kusimamia maadili ya
viongozi, watumishi wa Umma na watu wanaojishughulisha na sekta binafsi
nchini ili kuendelea kuimarisha utendaji kazi na kupambana na uovu
katika jamii.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
salaam na Mhe. Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ambaye alikuwa
Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo ambapo alisema kuwa maadili ya Taifa
ni moja ya tunu muhimu zinazolitambulisha taifa na kutofautisha taifa
moja na mataifa mengine.
“Maadili ya mtu binafsi au
yaTaifa hayaoti kama uyoga, lazima yajengwe, yaendelezwe na yalindwe
na watu waliodhamiria kufanya hivyo, siyo mara moja tu bali ni
muendelezo” alisema Balozi Sefue.
Balozi Sefue ameongeza
kuwa Serikali inaendelea kuimarisha utendaji na kupambana na uovu
katika jamii hususani rushwa na utovu wa nidhamu na ambapo Serikali
itaendelea kuchukua hatua kwa watumishi wa umma wanaotumia nafasi zao
kujitajirisha na kujilimbikizia mali kwa njia zisizo halali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Roundtable, Bw. Ali Mufuruki aliunga mkono hotuba ya Mhe. Balozi Sefue
kwa kusema kuwa hafikirii polisi au nguvu ya Mhe. Rais peke yake itaweza
kuzuia uvunjifu wa maadili bali wananchi wote wanatakiwa kushiriki
katika kuzuia uvunjifu huo wa maadili.
Maadhimisho ya Maadili ya Taifa
kwa Tanzania huazimishwa kila mwaka Desemba 10 kwa kuwa Desemba 09
Tanzania Bara huadhimisha sikuu ya Uhuru, chimbuko la sherehe hiyo ni
kumbukumbu ya vita dhidi ya rushwa ambayo hufanyika Desemba 09 kwa nchi
zote duniani.
Maadhimisho hayo yameambatana na
majadiliano yaliyoshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa
Taasisi za Umma, Wafanyabiashara, Muwakilishi kutoka USAID Bi Frola
Henjewele, Wawakilishi kutoka Sekta Binafsi, Taasisi za Kiraia,Viongozi
wa Dini pamoja na Wanafunzi kutoka Vyuo na Shule mbalimbali.
Na Jacquiline Mrisho -MAELEZO
Post a Comment: