HAPA KAZI TU : Rais Dkt. John Pombe Magufuli ampiga chini mkurugenzi wa (RAHCO)
Rais wa Jamhuri ya Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO)
Mhandisi Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia ukiukwaji
mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa
zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya
habari, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli
amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka Wizara
na Taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji
wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani
“Standard Gauge”
Amesema pamoja na kumsimamisha
kazi Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya RAHCO
baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika
kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea
kilichofanyika
Aidha Rais Magufuli amemtaka
Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Benhadard Tito kutoa ushirikiano kwa
vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa
Zabuni hiyo.
Pia ameiagiza Mamlaka ya udhibiti
wa manunuzi ya umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya
kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo
itathibitika kuwa zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua nyingine Balozi
Sefue amesema, Rais Magufuli amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania
(TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia
ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
22 Desemba, 2015
Post a Comment: