DARAJA LA CHIKWALE LITAKAMILIKA – WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Mandawa wilayani Ruangwa kabla ya
kuhutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo desemba 22, 2015. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa
akimtambulishasha diwani wa kata ya Mandawa kwa tiketi ya CUF, Said
Abdallah `Nachinga na kuahidi kuwa atashirikiana nae kwa karibu katika
kazi za kuwaletea maendeleo wananchi wa kata hiyo bila kujali tofauti za
vyama. Alikuwa katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mandawa
Desemba 22, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema darala la mto Mbwemkuru lililoko katika barabara ya kutoka
Chikwale hadi Liwale litakamilika kwa sababu ni kiungo muhimu kwa wakazi
wa eneo hilo.
Ametoa ahadi hiyo wakati
akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nangurugai katika kata ya Mbwemkuru
wilayani Ruangwa, mkoani Lindi ambako alikwenda kuwashukuru kwa
kumchagua kuwa mbunge wao.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja
za diwani wa Nangurugai, Bw. Selemani Likuche aliyetoa ombi la
kutengenezwa kwa daraja hilo kwani limekata mawasiliano baina ya kijiji
hicho na wilaya ya Liwale. Pia aliomba wapatiwe dawa na watumishi kwenye
zahanati yao.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu
alisema kazi ya ujenzi wa daraja hili itakamilishwa kwa sababu jukumu
kubwa alilonalo ni kuhakikisha ujenzi wa daraja la mto Mbwemkuru
unaisha.
Pia aliitaka Halmashauri ya
Ruangwa isimamie uboreshaji wa barabara ya kutoka Nangurugai hadi
Chikwale yenye urefu wa km. 35 kwa sababu ni muhimu kwa kusafirisha
mazao ya eneo hilo. “Hili eneo ni maarufu kwa zao la ufuta, kwa maana
hiyo linaongeza pia mapato ya Halmashauri, simamieni hii barabara ili
wananchi wasisumbuke kuuza mazao yao,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ruangwa,
Bw. Nicholas Kombe alisema milingoti (pillars) ya daraja hilo
ilikwishajengwa walikuwa wakisubiri kupokea vyuma vya kutandaza juu ya
daraja. “Tulikwishapeleka maombi yetu TANROADS na TAMISEMI lakini bado
hawajatujibu,” alisema.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji
wa dawa kwenye zahanati yao, Waziri Mkuu alisema ameshaongea na Mganga
Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye amemhakikishia kuwa ameanza maboresho ya
upatikanaji dawa katika zahanati zote. Kuhusu tatizo la watumishi wa
sekta ya afya, Waziri Mkuu
aliahidi kuwa watapatikana katika muda mfupi.
aliahidi kuwa watapatikana katika muda mfupi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa
Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo, alimweleza mwandishi wa habari hii kwamba
ameanzisha mfumo wa ukaguzi na udhibiti wa dawa zinazoletwa kwa kutumia
leja (ledger) tangu zinapoingia stoo hadi kwenye chumba cha kutolea
dawa.
“Kosa la kitakwimu halina msamaha, mtumishi akikosea kuoanisha mahesabu (tallying) anapaswa kujaza commitment form na sisi tunachukua hatua kuanzia hapo,” alisema Dk. Simeo.
“Pia nimeunda Kamati ya Wilaya ya
Ukaguzi wa Dawa ya Idara ya Afya kwa vituo vyote vya afya na zahanati
ambayo hufanya ukaguzi mara moja kila baada ya miezi miwili. Hii
inasaidia kufanya re-distribution ya dawa kwa zahanati zenye upungufu,” alisema.
Dk. Simeo alisema maboresho
mengine anayofanya ni kudai taarifa za mwezi ambazo ametaka zimfikie
tarehe 5 ya kila mwezi. “Nina zahanati 28, vituo vya afya vitatu na
hospitali ya wilaya moja, hizi ni taarifa 32 ninazopokea kila mwezi na
ninaipitia kila moja ili kujiridhisha licha ya kuwa zimetoka kwa
wasaidizi wangu. Inanisaidia kupata picha halisi ya utendaji kazi,”
alisema.
Post a Comment: