UTATA WA MADARAKA YA SHEIN
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
Unguja.
Ukomo wa madaraka wa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein umeibua utata na
kusababisha wanasheria na polisi kutoa tafsiri zinazokinzana.
Wakati
Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) kikisema kwa mujibu wa Katiba ya
Zanzibar tarehe ya mwisho ya Dk Shein kuingia ofisini ni leo Novemba 2, polisi
kwa upande wao wanasema Rais huyo anatakiwa kushika madaraka hayo hadi pale
rais mpya atakapoapishwa.
Rais
wa ZLS, Awadh Ali Said alisema mwishoni mwa wiki kuwa moja ya athari za tamko
la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi wa Zanzibar ni kusababisha
mgogoro wa kikatiba hasa katika muda wa rais kushika madaraka.
Said
alisema Ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza kuwa Rais
ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula
kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais.
Alisema
tafsiri yake ni kuwa tangu Dk Shein alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha
kuwa rais Novemba 3, 2010 atakuwa ametimiza miaka mitano Novemba 2, 2015.
“Hivyo
akiendelea kushikilia madaraka ya urais zaidi ya tarehe hiyo itakuwa kinyume na
Katiba ya nchi,” alisema.
Kutokana
na madai hayo, Jeshi la Polisi Zanzibar limewatahadharisha wananchi
kutojihusisha na vitendo vya fujo kwa madai kwamba kuanzia leo hakutakuwa na
Serikali.
Walichosema
ZLS
Kwa
mujibu wa Rais wa ZLS, maudhui ya Ibara 28 (1) hiyo ni kumpa uwezo wa kikatiba
Rais kuendelea ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo kwa Rais anayefuata
tu na si kuendelea kukaa madarakani bila ya kufanyika kwa uchaguzi au kwa
sababu ya Uchaguzi kufutwa.
Hata
hivyo Said alisema nchi kuendeshwa muda mrefu bila ya Baraza la Wawakilishi
(MBW) kama mazingira yaliyopo yanavyoonyesha ni tatizo.
Alisema
Katiba ya Zanzibar imeruhusu hali ya kuendesha nchi bila ya BLW kwa muda
usiozidi siku tisini (90) tu kuanzia siku Baraza lilipovunjwa.
“Kwa
mazingira tuliyonayo, siku tisini (90) zinazokubalika kikatiba zinaishia
Novemba 12, 2015 kwa kuwa BLW lilivunjwa Agosti 13, 2015,” alisema.
Rais
huyo wa TLS alionyesha pia hatari ya kuwa na rais ambaye yuko juu ya Sheria na
Katiba, akibainisha Ibara ya 37 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inayoipa Mamlaka
Baraza la Wawakilishi kuondoa kinga ya Rais kutoshtakiwa anapokuwa madarakani
kama inavyotolewa na Ibara ya 36 ya Katiba.
Alisema
katika mazingira yaliyopo hivi sasa ambapo ifikapo tarehe 12 Novemba, 2015,
Baraza la Wawakilishi halitakuwapo na haliwezi kuitishwa kikatiba, ni wazi kuwa
ikiwa Rais atafanya matendo yoyote yenye kuvunja katiba ya nchi na kukiuka
kiapo chake, hakutakuwa na mamlaka nyingine yoyote yenye uwezo wa kuhoji
matendo ya Rais.
Alidai
hii inatoa fursa na inatengeneza hatari ya kuwa na Serikali inayoongozwa na
‘dikteta’.
Kauli ya Polisi
Kamishna
wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema jana kuwa kutokana na taarifa
hizo za wanasiasa na watu wengine, huenda wananchi watakuwa huru kufanya watakavyo
na hivyo kuvunja sheria.
“Tunawaomba
wananchi kuacha ushabiki na jazba ili kuwaepusha na gharama za matatizo, wao
wenyewe na familia zao. Waswahili wanasema ‘vyako ni vyako, likikupata ni la
kwako na kila mchumia janga hula na mwanawe’,’’ alisema Kamishna Makame.
Makame
alisema ni vyema kipindi hiki kuhubiri amani na kuwa na subira kuiachia ZEC
ambayo ndiyo yenye dhamana na mamlaka ya kutangaza tarehe ya kurejewa kwa
uchaguzi na si mtu mwingine.
Kamishna
Makame alinukuu kifungu cha 28 (1) cha Katiba ambacho pia wanasheria wa ZLS
walikitoa na kumwomba Rais wa Zanzibar kuchukua tahadhari ili asiwe wa kwanza
kuvunja Katiba ya Zanzibar kwa kuvuka terehe ya mwisho kuwapo madarakani.
Kifungu
cha 28 (1) cha Katiba kinasema, “Kufuatana na Katiba hii mtu ataendelea kuwa
Rais mpaka (a) Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais, au (b)afariki wakati
akiwa Rais, au (c) hapo atakapojiuzulu; au (d) iwapo amechaguliwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ; au (e) kwa sababu yoyote nyingine ameacha
kuwa kiongozi kwa mujibu wa vifungu vingine vya katiba hii.
“Ikumbukwe
kuwa kutokuwapo Rais wa nchi kama inavyodaiwa, haimaanishi sheria hazipo na
watu wafanye watakavyo. Kuna makosa ukiyafanya moja kwa moja sheria itachukua
mkondo wake ikiwamo kufanya kitendo cha uvunjifu wa amani, kufanya maandamano
au mikusanyiko ya watu isiyo halali,” alisema kamishna huyo.
Lipumba: Ni jukumu la JK
Sakata
hilo la Zanzibar kwa mara ya pili lilimwibua mwenyekiti wa zamani wa Chama cha
Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akimtaka Rais Jakaya Kikwete kumaliza
tatizo la Zanzibar kwa kuiamuru ZEC kumtangaza mshindi wa uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25 ili kuliepusha Taifa lisiingie kwenye machafuko.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Lipumba alisema ni muhimu Kikwete akahakikisha
anatekeleza hilo kabla ya kumaliza muda wake, badala ya kumwongezea matatizo na
mzigo rais mpya, Dk John Magufuli anayetarajiwa kuapishwa Novemba 5.
“Alhamisi
ijayo Dk John Magufuli ataapishwa kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya
Ulinzi na Usalama vya Tanzania, Kikwete usimwongezee Magufuli matatizo,
yaliyopo yanamtosha,” alisema Lipumba ambaye wiki iliyopita akizungumzia pia
mgogoro huo akiitaka ZEC imtangaze mshindi.
Lipumba
aliyepokewa na wafuasi zaidi ya 100 kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho,
Buguruni , Dar es Salaam, alisema amelazimika kutoa ushauri huo baada ya kuona
hatari iliyo mbele, iwapo wananchi wa Zanzibar watanyang’anywa haki yao.
“Vigogo
wa Tanzania na Zanzibar wasisubiri hadi maafa yatokee ndipo waanze kuchukua
hatua, watumie muda huu kuyazuia,” alisema na kuonya:
“Nayakumbuka
mauaji ya wafuasi wa CUF yaliyotokea mwaka 2001 na wengine kukimbilia
uhamishoni Shimoni nchini Kenya, nimeona kukaa kimya kutaleta madhara katika
nchi hii,” alisema.
Mmoja
wa wanachama wa chama hicho, tawi la Buguruni, Ashura Mohammed alisema ni
muhimu Wazanzibari wapewe haki yao kwa matokeo ya uchaguzi walioufanya
kutangazwa.
ADC : Jecha, ZEC wamekosa sifa
Wakati
huohuo, Mwenyekiti wa chama cha ADC, Said Miraaj Abdulla amesema ZEC chini ya
Jecha Salim Jecha haiwezi kusimamia tena uchaguzi wa Zanzibar baada ya siku 90
kwa sababu ina mapungufu mengi kama ilivyoyaainisha yenyewe.
Abdulla
alisema sababu zilizotolewa na Jecha kufuta matokeo hazina mashiko, zimelenga
kuficha ukweli na kutetea maslahi ya upande mmoja. Alisema chama chake kitasimamia
haki na ukweli kuhakikisha kwamba matakwa ya wananchi yanasikilizwa.
“Kwanini
Jecha aje leo kutueleza kuwa tume yake iliingiliwa na wanasiasa? Siku zote
alikuwa wapi na alichukua hatua gani katika kuhakikisha tume yake inakuwa
huru,” alihoji mwenyekiti huyo na kusisitiza kuwa kuna ajenda inafichwa na
Jecha.
Mwenyekiti
huyo aliendelea kusema, Jecha alisisitiza katika matamshi kwamba wajumbe wa ZEC
walikuwa wamegawanyika kwa misingi ya vyama vyao lakini hakueleza ni kwa namna
gani mgogoro wa wajumbe hao umeathiri kura zilizopigwa.
Aliwataka
viongozi kuwa makini na matamshi yao ili yasije kusababisha migogoro na kuvunja
amani ya nchi na vyama vyote kuwa na sauti moja ili viweze kutetea haki za
wananchi wa Zanzibar ambao wamechagua viongozi wao kwa misingi ya kidemokrasia.
“Viongozi
wa CUF na CCM waache kuangalia maslahi ya vyama vyao bali waangalie maslahi
mapana ya umma. Chama changu kiko tayari kushirikiana na chama chochote katika
kuhakikisha kwamba suluhu ya mgogoro huo inapatikana,” alisema.
SOURCE : Mwananchi,Nov 2/2015
Post a Comment: