Saturday, 21 November 2015

15Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli akihutubia Bunge la Jamhuri kama ishara ya kuzindua Bunge la 11. mjini Dodoma.
…………………………………………………………….
Na: Immaculate Makilika, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amezindua Bunge la 11 leo mjini Dodoma na kusema anakusudia kuunda Mahakama ya rushwa na ufisadi ili kusaidia kutatua kero hiyo ambayo imeonekana kukera wananchi wengi. Rais Magufuli amezindua Bunge hilo kwa mujibu wa Ibara ya 97, Ibara ndogo ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Rais Magufuli amesema, “wananchi wamekua wakilalamika sana juu ya rushwa na ufisadi unaondelea nchini kwa kusababisha wananchi kutopata haki zao na kutatuliwa shida zao kwa wakati, kati ya mambo ninayokusudia kuyashughulikia ni pamoja na kuunda Mahakama rushwa na mafisadi.” Kwa mujibu wa Rais Magufuli maeneo mengine ambayo wananchi wameyalalamikia ni pamoja na matatizo ya upatikanaji wa maji, migogoro ya ardhi, mgogoro ya mipaka kati ya vijiji na hifadhi za taifa, huduma za afya ,madini, kilimo, reli, elimu, ajira, haki za wazee, na maslahi ya wafanyakazi na wasanii. Pamoja na hayo Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaondoa urasimu katika uwekezaji na kutowavumilia wale wote watakaokwamisha nia za wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchini. Aidha, Dkt Magufuli ameeleza kuwa awamu hii ya Tano, itaweka msisitizo katika ujenzi wa viwanda ambavyo vitazalisha mahitaji ya watu (mass consumption) na kusema kuwa “waliobinafsishiwa viwanda waanzae kazi mara moja ,Serikali yangu haitawavumilia.” “Tutatatua kero za wananchi, na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuimarisha Muungano. Muungano wetu ndio umoja wetu”. Kwa mujibu wa Rais huyo wa awamu ya Tano, yatakayoshughulikia ni pamoja na mchakato wa Katiba, Upanuzi wa barabara, reli na masuala ya uchumi. Rais Magufuli anakua Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1961 baada kuibuka mshindi kwa zaidi ya asilimia 50 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba , 2015.

Rais Magufuli azindua rasmi Bunge la 11 mjini dodoma

 2
Kabla ya Rais Dkt. Magufuli kuzindua Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju aliomba Bunge likubali kutenguliwa kwa kanuni za Bunge ili kuruhusu wageni kuingia ndani ya Bunge hilo.
1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli akihutubia Bunge la Jamhuri kama ishara ya kuzindua Bunge la 11.
21
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akitoa hotuba ya kuahirisha Bunge hadi mwezi Januari mwakani baada ya Mhe. Rais kulizindua Bunge hilo.
13
Spika Job Ndugai akatoa amri ya kuwataka wabunge hao kuwa watulivu na walipokaidi amri hiyo akatoa amri ya kuwataka watoke nje ya ukumbu wa Bunge.
3
Baada ya Mwanasheria Mkuu kutoa hoja Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson akawahoji wabunge.
4
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu akiomba mwongozo wa Naibu Spika kwa kile alichodai kuwa kanuni zimekiukwa.Hata hivyo, kiongozi huyo wa Bunge alitoa mwongozo na baadaye alisitisha Bunge kuwaruhusu wageni kuingia kwenye ukumbi wa Bunge.
9
Baadhi ya wabunge wa upinzani wakiteta jambo wakati wageni wakiingia Bungeni.
10
Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakifuatilia yanayojiri Bungeni.
11
Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson (kushoto), Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Jaji Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho wakiingia kwenye ukumbi wa Bunge huku wakiongozwa na mpambe wa Bunge.
12
Baada ya viongozi hao kuwasili kwenye ukumbi wa Bunge, wabunge wa Upinzani waliendelea kupiga meza na kuimba, hali iliyofanya ukumbi wa Bunge ukose utulivu.
  16
Viongozi mbalimbali wakiwemo Marais wastaafu, wakuu wa vikosi vya majeshi ya Ulinzi na Usalama, Maspika wastaafu, Watendaji Wakuu wa Serikali, Mawaziri Wakuu wastaafu na wageni wengine wakisikiliza hotuba ya Rais.
17
Baadhi ya wakuu wa mikoa, viongozi wa dini na wageni wengine waalikwa wakimsikiliza Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
14
Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya ukumbi wa Bunge isipokuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia ACT Wazalende,Zitto Kabwe aliendelea kubaki ukumbini.
18
Wabunge walionesha kuridhishwa na hotuba ya Mhe. Rais Makufuli, wakipiga meza kuunga mkono hotuba hiyo.
22
Baada ya kukamilika kwa kazi hizo, Mhe. Rais Magufuli akasindikizwa na wapambe wa Bunge kutoka nje ya Bunge huku akiambatana na Spika wa Bunge Job Ndugai.
20
Baadhi ya Mabalozi na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Mhe. Rais Magufuli.
23
Mhe. Rais Dkt. Magufuli (wa pili kushoto) akiwa na Marais Wastaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili kulia), Benjamin Wiliam Mkapa (kulia) na Alhaj Ali Hassan Mwinyi (kushoto).
24
Mhe. Rais Dkt. Magufuli (wa tatu kulia) akiwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (kulia kwake) na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein (wa pili kulia) na Marais Wastaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi (kushoto) na Amani Abeid Karume (kulia).

Post a Comment: