NEC yatoa Taarifa kuhusu upigaji kura kesho
……………………………………………………
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) imetoa taarifa kuhusu upigaji kura katika uchaguzi utakaofanyika kesho
tarehe 22 Novemba, 2015 katika majimbo mawili na kata sita ambapo uchaguzi wake
ulihairishwa.
Akitoa taarifa hiyo leo
jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume ya Taifa ya uchaguzi
Bwa. Emmanuel Kawishe amesema kuwa Tume ilitoa taarifa kwa kuhairishwa kwa
Uchaguzi katika Jimbo ya Lushoto mkoani Tanga, Jimbo la Ulanga Mashariki mkoani
Morogoro, kata ya Muleba, Uyole, Bukene, Msingi, Bomang’ombe pamoja na kata ya
kasulo kutokana na vifo vya wagombea.
“Kesho ni siku ya kupiga
kura ya kuchagua Mbunge katika majimbo mawili na kuchagua Diwani katika kata
sita, natoa rai kwa wale wote mliojiandikisha kama wapiga kura katika majimbo
na kata hizo kujitokeza kwenye vituo mlikojiandikisha ili kuweza kupiga kura na
kuwachagua viongozi mnaowataka bila hofu, woga wasiwasi au ushawishi” aliongeza
Kaimu Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo Bwa. Kawishe
alisema kuwa vituo vitafunguliwa kuanzia saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi
jioni na kuwakumbusha wapiga kura kubeba
kadi yake ya mpiga kura.
“Kipaumbele kitatolewa kwa
wagonjwa, watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wajawazito au wenye
watoto wachanga na wazee ambao hawatatakiwa kujipanga kwenye foleni”
“Wakati wote wa kupiga kura
na kuhesabu kura, mawakala wa vyama vya siasa wawepo kwenye vituo na wajibu wao
ni kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea hivyo hawatakiwi kuingilia masuala
ya utendaji ambayo yamekabidhiwa kwa msimamizi wa kituo” alifafanua Bwa.
Kawishe.
Mbali na hayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi
amewapongeza wananchi kutoka majimbo na kata zinazofanya uchaguzi kesho kwa
uvumilivu waliouonyesha katika kipindi chote cha kusubiri siku ya kupiga kura
kumchagua Mbunge au Diwani wao.
Post a Comment: