MH EDWARD LOWASSA KUNGURUMA ARUSHA JUMAMOSI HII
Aliyekuwa mgombea wa urais
wa tiketi ya Chadema,Mh Edward Lowassa anatarajiwa kupanda jukwaani Jumamosi
kumuombea kura mgombea wa ubunge wa Chadema Jimbo la Arusha Mjini, Godbless
Lema.
Akizungumza katika mkutano
wa uzinduzi wa kampeni za ubunge katika jimbo hilo uliofanyika Soko Kuu jana,
Lema alisema Lowassa atazungumza na Watanzania na kuwashukuru pia kwa kura
nyingi walizompa.
Awali, mbunge mteule wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alieleza kuwa Lowassa na viongozi wa
Chadema watatoa tamko zito siku hiyo na kuwataka wakazi wa Arusha na Watanzania
kutega masikio.
Lema ambaye pia ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chadema, aliwataka wakazi wa Arusha, kutokatishwa tamaa na
kuendelea kuwa na huzuni kutokana na matokeo ya urais yaliyotangazwa na kuwa
bado kuna harakati za chama hicho kusaka haki.
“Ndugu zangu msikate tamaa,
tumesikia wengine wametupa shahada zao, hapana, kazi ndiyo imeanza na lolote
linaweza kutokea kwa uwezo wa Mungu,” alisema.
Alisema huzuni ya matokeo
yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haipo kwa wananchi tu, bali
hata wajumbe wote wa kamati kuu.
“...Kwenye kikao cha kamati
kuu, kuna wajumbe walimuomba Lowassa atoe tamko... kama angetoa tamko la kupinga matokeo na
kukubali watu kuingia mitaani, Tanzania ingekuwa imeingia katika machafuko
makubwa.
“Tunaendelea kutumia taasisi
za kimataifa kudai haki, ndiyo sababu mnaona Zanzibar wameshindwa kujitangazia
matokeo, hii ni kazi kubwa ya Ukawa,” alisema.
Katika mkutano huo, Lema
alieleza njama alizosema zinapangwa kumnyima ushindi na akaonya kuwa hatakuwa
tayari kuona ameshinda lakini mwingine akatangazwa kushinda.
“Najua Arusha nitashinda kwa
kura nyingi, lakini kama wakitaka kunipora ushindi sitakubali,” alisema Lema.
Aliwaomba wakazi wa Arusha
kujitokeza kwa wingi Desemba 13 kumpigia kura nyingi, ili pia kuwezesha Chadema
kupata viti viwili zaidi vya wabunge wa viti maalumu.

Post a Comment: