Lowassa chanzo cha Mwanri, Anne Kilango kuanguka - CCM
Mh. Edward Lowassa.
Katibu wa Jumuiya ya
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro (UVCCM), Yasini Lema,
‘amefunguka’ kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita namna ulivyokiathiri
chama hicho na kukifanya kipoteze majimbo ya uchaguzi ya Siha, Same Mashariki
na Moshi Vijjini waliyokuwa wakiyashikilia kwa zaidi ya miaka 15.
Lema amedai
kuangushwa kwa mawaziri wawili wa serikali iliyopita, Aggrey Mwanri aliyekuwa
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Anne Kilango Malecela (Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi) na Dk. Cyril Chami, kulitokana na ushawishi mkubwa wa aliyekuwa mgombea
urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Lema aliyasema hayo
jana wakati akizungumza kuhusiana na tathimini yao waliyoifanya
Novemba 7, mwaka huu baada ya kupitia zoezi zima la uchaguzi mkuu uliofanyika
Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema Lowassa ndiye
aliyeisaidia Chadema kuwapokonya majimbo hayo kutokana na kuungwa mkono na
wananchi wengi wakiwamo pia baadhi ya makada wa CCM ambao hawakufurahishwa na
kitendo cha Kamati Kuu ya chama hicho kuliengua jina lake wakati wa mchakato wa
uteuzi ndani ya chama hicho.
“Chadema imefanikiwa
kuchukua majimbo ya CCM kutokana na mkakati wa Lowassa pamoja na kuhama kwake,
kitu ambacho kilitengeneza mpasuko ulioiua CCM na wagombea wake,” alisema.
Alidai kulitokea
usaliti ndani ya CCM kwa madai kulikuwa na kundi ambalo lilikuwa likiendelea
kushiriki vikao vya ndani huku likikerwa na kuondoka kwa Lowassa jambo ambalo
lilisababisha chama hicho kushindwa katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Aidha, akizungumzia mkakati wa CCM kuyarejesha mikononi mwake majimbo ya Moshi
Mjini na Rombo, Lema alidai kuwa sababu ya kushindwa kwao ni kutokana na wagombea wa nafasi za ubunge
kupitia chama hicho kupora mamlaka ya viongozi wa wilaya.
“Wagombea ubunge
katika majimbo haya mawili walikuwa na nguvu zaidi katika chama, atakalolisema
yeye na atakalopanga ndilo atakalolisimamia lifanyike. Ukweli ni kwamba
viongozi wa wilaya nao waliwaogopa, huku kampeni zao zikikwepa kabisa
kuwashirikisha viongozi wa chama ngazi za matawi na kata” alisema Lema
.
Alisema pamoja na
kwamba CCM kilianzisha vikosi kazi maalum kwa ajili ya kutafuta kura, lakini
katika hali ya kushangaza wagombea wao wa ubunge katika majimbo yote tisa ya
Mkoa wa Kilimanjaro, walijiweka kando kuwatumia viongozi wa matawi na ngazi ya
kata.
Sababu nyingine ya kupoteza viti vingi vya udiwani
alisema ni wagombea wao kujiaminisha kwamba CCM ingewaletea fedha nyingi kwa
ajili ya kampeni huku wengine wakiamini wangesaidiwa na wagombea ubunge ambao
waliamini walikuwa na fedha nyingi kuwashinda wagombea wa vyama vya upinzani.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment: