Thursday, 12 November 2015

Katika hali isiyotarajiwa na wengi, Katibu wa UVCCM wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Bi. Anna Gideria ameteuliwa na Chadema kuwa mbunge wa viti maalum.

Bi. Gideria amejiuzulu nafasi ya ukatibu na kukabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Manyara, Bi. Regina Ndege baada ya kutangazwa majina ya viti maalum na jina lake kuwa katika orodha ya wabunge wa Chadema.

Akizungumzia hatua hiyo, Bi. Ndege alieleza kuwa Bi. Gideria alipoteza imani na CCM muda mfupi baada ya jina la waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kukatwa katika kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Bi. Gideria alikuwa ‘Team Sumaye’ na aliomba likizo ya mwezi mmoja baada ya jina la waziri mkuu huyo wa zamani kukatwa.

“Baada ya Sumaye kutoswa, alipoteza imani na CCM na ilipofika wakati wa kampeni mwezi Agosti aliandika barua ya kuomba likizo na kukabidhi ofisini kwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UVCCM wilaya ya Mbulu,” alisema Bi. Ndege.

Blog SiasaLeoTz lilijitahidi kumtafuta Bi Anna Gideria ili kujua sababu zilizosemwa na mwenyekiti wake wa zamani zina ukweli kiasi gani, na kumpata ambapo yeye binafsi amekiri kuwa alipoteza imani na ccm tangu kwenye mchakato wa urais uliofanyika mwezi julai Dodoma, na si kwasababu mh Sumaye alikatwa ila ni kwakuwa  mchakato mzima ulikiuka taratibu za chama, na kuwepo ubabe wa hali ya juu kwa viongozi wakubwa dhidi ya demokrasia. hivyo hakuona tena haja ya kuendelea kuwa mwanachama na kiongozi wa chama kinachobaka demokrasia.

Post a Comment: