Viashiria Vya Uvunjifu Wa Amani Wiki Moja Kabla Ya Uchaguzi Ni vingi -Tamko Kali La Asasi Za Kiraia
TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU
VIASHIRIA VYA UVUNJIFU WA AMANI WIKI MOJA KUELEKEA TAREHE YA UPIGAJI KURA KATIKA
UCHAGUZI MKUU TANZANIA TAREHE 25.10.2015
Asasi
za Tanzania tumeendelea kufuatilia mchakato wa uchaguzi mkuu 2015 tangu
uandikishaji wapiga kura, uhamasishaji hadi kampeni zinazoendelea kwa umakini
mkubwa.
AZAKI
tumefanya hivyo tukiamini kuwa uchaguzi ni sehemu kuu ya michakato ya kidemokrasia
hapa nchini kama ilivyo duniani kote. Sisi asasi za kiraia Tanzania, tukiwa
watetezi na wasimamizi wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu,
hatumuungi mkono mgombea yeyote wala chama chochote cha kisiasa kinachotafuta
kuingia madarakani wala hatulengi kuchukua dola.
Kwa
ujumla wake, uchaguzi hufanikishwa na wadau wengi tukiwemo sisi AZAKI, Vyombo
vya usalama, viongozi wa Dini, Taasisi za Umma kama Tume na Vyombo vya habari.
Lakini makundi makuu mawili ya wahusika wakuu ni wapiga kura na wapigiwa kura.
Ili wapiga kura waweze kuchagua kiongozi
atakayeweza kusimamia maendeleo ya nchi na kuhakikisha amani ya nchi
inazidi kudumu ni lazima viashiria vyote vya uvunjifu wa
amani na mazingira ya vitisho kwa wapiga kura
vijadiliwe na wadau na vidhibitiwe mapema.
Usalama
na amani wakati wote wa uchaguzi ni suala la muhimu sana na ndio maana Asasi za
Kiraia (AZAKI) nchini zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015 unakuwa wa kidemokrasia, wa haki
na wa amani.
Tanzania
ni Taifa lenye amani kwa muda mrefu sasa, lakini tusipokuwa makini katika
kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya haki na usawa huenda
tukalitumbukiza taifa hili katika machafuko.
Angalizo
hili ni muhimu zaidi kwa mwaka huu ambapo hamasa na mashindano vimekuwa kwa
kiwango cha juu kuliko miaka mingine yoyote ya nyuma.
Ili
kuweza kuhakikisha uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 unafanyika kwa usalama na amani AZAKI zimeona ni vyema kuanisha masuala mbalimbali
yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani nchini
kama angalizo kwa sekta na
taasisi husika kuchukua hatua stahiki mapema.
Mchakato huu umejaa changamoto mbalimbali
ambazo kama hakutakuwa na jitahada za ziada basi ni wazi kuwa tutakwenda
kufanya uchaguzi tukiwa katika hali tete zaidi. Kati ya hizo changamoto nyingi
zinazojitokeza, sisi wana AZAKI tumeanisha mambo sita makubwa yanayohitaji
ufumbuzi wa haraka kabla ya tarehe 25 oktoba. Mambo hayo ni kama yafuatayo;
(i)
Matumizi Makubwa ya nguvu ya Vyombo vya Usalama
AZAKI zimegundua kuwa vyombo vya usalama kama Jeshi
la Polisi na makundi mengine ya usalama Tanzania Bara na Zanzibar zimekuwa
zikilalamikiwa sana kwa kuona kuwa tishio kwa wananchi badala ya kuwa msaada
kwa wananchi. Kwa mfano, majeshi haya
yamekuwa yakifanya mazoezi waziwazi
na karibu na makazi ya watu suala
linalopelekea kujenga uoga na hofu kwa
wananchi .
Pia baadhi yao
wameonekana wakitapakaa kwenye makazi ya wananchi huku wakiwa wamevaa
sare zao. AZAKI zinatambua umuhimu wa vyombo hivi kipindi cha uchaguzi, AZAKI tunataka vyombo hivi kufanya kazi zao
bila kujenga hofu kwa wananchi na kwa mujibu wa Sheria.
Wito
Wetu kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama
Vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi zake
kwa uweledi na tahadhari ya kutowatia hofu wananchi na wapiga kura. Vyombo vya
ulinzi visitumie vitisho, nguvu, na silaha za kivita wakati wa mikutano ya
kampeni na siku ya kupiga kura.
Vyombo
vya usalama kwa namna yoyote visiegemee
upande wowote wa chama cha siasa bali vitende haki kwa vyama vyote na
wananchi wote wakiwemo wagombea mmoja mmoja na wala visikubali kuyumbishwa na
mamlaka yoyote nje ya sheria inayovipa mamlaka kutekeleza wajibu wao.
Tunalishauri
Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutojihusisha na mchakato wa uchaguzi kuanzia
kipindi cha maandalizi, cha
kampeni, upigaji kura na baada ya upigaji kura.
(ii)
Daftari la Wapiga Kura na Taarifa za Msingi
Kwa mujibu wa Katiba na Sheria, Uchaguzi wa
Tanzania unasimamiwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar( ZEC). AZAKI zimebaini pia pamoja na kufanya vizuri
katika hatua zingine Tume za Uchaguzi kwa sasa zimeonyesha udhaifu mkubwa
katika eneo la utoaji wa taarifa za msingi kwa wadau na umma kwa ujumla.
Tumeshudia
ukinzani wa taarifa mbalimbali zinazotolewa na Tume kama taarifa za idadi
halisi ya wapiga kura walioandikishwa pamoja na idadi ya vituo vya kupigia
kura. Ukinzani wa takwimu za muhimu kama hizi ni jambo linaloweza kupelekea
uvunjifu wa amani kama lisipo simamiwa vyema.
Mambo
haya pamoja na mengine yanawaweka wananchi katika hofu kubwa kwa kutokujua kama
watapiga kura ama la na endapo idadi halisi ya wapiga kura ni ipi. Hofu
inaongezwa na ukweli kuwa Sheria za uchaguzi Tanzania haziruhusu kulalamikia
matokeo ya uchaguzi hususani katika ngazi ya urais.
Wito
wetu kwa Tume za Uchaguzi
Tume
ya Taifa ya uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar zitimize majukumu yao kisheria kwa kutangaza rasmi takwimu za mwisho za idadi ya vituo vya kupigia kura na kujibu
hoja zinazaoibuliwa na wanasiasa badala ya kuwabeza na kuwapuuza.
Tume
Itoe Daftari la wapiga kura lenye vigezo
vyote kwa wadau wote na wanachi kwa
ujumla mapema iwezekanavyo ili kutoa fursa ya kurekebisha makosa
yatakayobainika.
Tume
ibandike majina ya wapiga kura kwenye vituo vyote wiki moja kabla ya siku ya
kupiga kura kama ilivyoahidi kwa ajili ya wapiga kura kujua vituo
watakavyopigia kura.
Tume
za uchaguzi zifanye kazi kwa uhuru, kufuata sheria, kusimamia kanuni
walizokubaliana na vyama vya siasa na kujiepusha kwa namna yoyote kukipendelea
chama chochote wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
Tume
zinapaswa kuhakikisha kuwa zimewapa mafunzo ya uhakika maofisa na wasidizi wa
uchaguzi na kuchunguza mienendo yao kabla hawajawakabidhi vituo vya kazi ili
kuepusha makosa yaliojitokeza wakati wa kuandikisha wapiga kura.
Tume
za Uchaguzi zinapaswa kufanya maandalizi mapema, pia kusambaza vitendea kazi
vinavyotakiwa kwa wakati ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza siku ya
upigaji kura pamoja na hisia kuwa baadhi ya maeneo yanacheleweshewa vifaa kwa
makusudi.
Tume
zihakikishe kuwa watu wote wenye sifa na kustahili kupiga kura ambao
hawakuandikishwa katika vituo waliko siku ya upigaji kura wanawezeshwa kufaidi
haki yao ya kupiga kura kwa mujibu wa sheria.
Tunazitaka
Tume ziruhusu mawakala wa vyma vya siasa kuingia kwenye chumba cha mwisho cha ujumlishaji
wa kura za urais (National Tallying Centre) ili kuondoa hofu ya kuibiwa kura.
Ifamike kuwa matokeo ya urais yakishatangazwa hayawezi kupingwa
mahakamani. Ni kinyume na taratibu za
uchaguzi kuwazuia mawakala wa vyama vya siasa kuingia kwenye kituo kikuu cha
kitaifa cha ujumlishaji wa kura.
Tume
zitangaze matokeo sahihi bila ya kuchelewesha ili kuepusha kutokea kwa vurugu
zinazoweza kujitokeza.
(iii)Mgogoro
wa Kusubiri Matokeo katika umbali usiopungua Mita 200
AZAKI
tumebaini kuwa jambo lingine linaloweza kuchangia uvunjifu wa amani ni mgogoro uliobuka kuhusu uhuru wa wapiga kura
kubaki vituoni katika umbali usiopungua mita 200.
Kwa mujibu wa
sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 sura ya 343 ya sheria za
Tanzania kama zilivyopitiwa mwaka 2010
mpiga kura anapewa haki ya kupiga kura na kuondoka kuendelea na shughuli
nyinginezo au kubaki kituoni kusubiri matokeo ili mradi anafanya hivyo katika
umbali usiopungua mita 200 toka kituoni na kwamba hafanyi mkutano. Kwa tafsiri
hii, mpiga kura hajalazimishwa kurudi nyumbani baada ya kupiga kura wala
hajakatazwa kuwepo nje ya eneo la katazo la kisheria kwa mujibu wa kifungu cha
104 (1).
Sheria
inamtaka mpiga kura asionekane ndani ya eneo la
kituo cha kupiga kura baada ya kumaliza kupiga kura(within the vicinity)
na haimlazimishi mwananchi arudi nyumbani mara baada ya kupiga kura au asogee
umbali wa mita 200 bali sheria ya uchaguzi inaweka bayana kwa wananchi/mpiga
kura kutokupiga kampeni au kuvaa nguo zenye alama au nembo ya chama chochote katika
siku hiyo.
Wito
Wetu kwa Tume za Uchaguzi na Jeshi la Polisi
Kwa
kuwa hili limekuwa kawaida sasa katika
chaguzi zilizopita hapa Tanzania
wananchi kubaki vituoni na kusubiri
matokeo karibu na vituo kwa umbali wa mita 200, na kutokana na ufinyu wa muda usioweza kutoa
mwanya wa kurekebisha sheria hii, Tunazitaka Tume za uchaguzi
zitumie busara katika kuamua suala hili kwa kupima faida na hasara za
kuzuia wananchi kubaki vituoni kwa umbali wa mita 200 kama walivyozoea
katika chaguzi zilizopita.
Pia, Tume zitoe maelekezo yenye kuangalia
zaidi maslahi ya Taifa kwa wananchi
badala ya kusikiliza upande wowote kati ya wanaovutana kuhusu suala
hili. Ushauri wetu kuhusu jambo hili ni
kuwa wapiga Kura waamue kuendelea na shughuli zao baada ya kupiga kura lakini
wanaotaka waweze kubaki vituoni kwa umbali wa mita 200 kwa kadri ya mapenzi yao
huku wakiepuka kufanya kinachofanana na mikutano.
Mahakama
isadie kutatua mgogoro huu wa tafsiri ya kisheria ili kuepusha machafuko katika Taifa hili yanayoweza kutokana
na imani kuwa kukatazwa kubaki vituoni kuna nia ya kutaka kufanya ujanja Fulani
kuhusu kura zao ikiwemo kuziiba.
Pia
tunataka Jeshi la Polisi wasitumie nguvu yoyote kwa wananchi endapo itafika
siku ya kupiga kura bila suala hili kupatiwa ufumbuzi. Hii ni kwa sababu kwa
jinsi Sheria ilivyo, imeruhusiwa wananchi kubaki umbali wa mita 200 kutoka
vituoni.
Pia
tunawataka wapiga kura endapo wataona umuhimu wa kukaa umbali wa mita 200 kusubiri matokeo, basi wafanye hivyo kwa
unyenyekevu mkubwa ili kulinda amani na pia kuepuka kuzuia wananchi wengine
kutumia haki zao.
(iv)
Suala la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na watumishi waliohamishwa vituo vya kazi
Ni
kwa mara nyingine sasa katika uchaguzi mkuu wanafunzi wa vyuo vikuu
wanakoseshwa haki yao ya kupiga kura kwa
sababu zisizoridhisha.
Wanafunzi wengi walijiandikisha katika maeneo
ambayo hawatakuwepo siku ya kupiga kura na hawataweza kupiga kura zote tatu
kutokana na kwamba vyuo vitakuwa vimefungwa siku hadi tarehe ya upigaji kura.
Aidha,
baadhi ya watumishi wa umma waliohamishwa vituo vya kazi katika miezi na siku
za karibuni nao wamejikuta katika hali ya ugumu waliyonayo wanafunzi na
wanavyuo.
Wito
Wetu kwa Tume za Uchaguzi
Asasi
za kiraia zinasisitiza watanzania walio katika makundi hayo mawili wapewe fursa ya kuwezeshwa kufanya taratibu za
kisheria kuwawezesha kupiga kura ya Rais siku ya tarehe 25 Oktoba. Aidha,
katika miaka ijayo, Tume zihakikishe kuwa technolojia ya habari inawezesha
upigaji kuwa wa waliojiandikisha popote nchini bila matatizo yoyote kwa kuwa
mfumo ni wa kielektroniki.
Asasi
za Kiraia hazioni ulazima wa Tamko la Tanzania Commission for Universities
(TCU) kwamba vyuo vikuu visifunguliwe mpaka baada ya uchaguzi kwani amri hii inanyima wanafunzi wa vyuo
hasa wale wachache walijiandikisha vyuoni
haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kinaweza kuwa ni kichocheo cha
uvunjifu wa amani. Suala hili linapaswa
liangaliwe upya kwa miaka ijayo.
(v)
Kauli za Vitisho na Lugha Chafu
Kwa
muda huu mchache uliobaki, vyama vya siasa na wanasiasa vinapaswa kuendesha kampeni za kistaarabu
zinazoheshimu misingi ya sheria na siasa za ushindani ambazo zinatambua kuwa
kuna kushinda na kushindwa.
Kwa
hivyo, kusiwepo na kampeni za vitisho, matusi na ubaguzi wa aina yoyote na
badala yake kuwepo kampeni za kistaarabu zinazoheshimu na zinazozingatia
maadili ambayo vyama vyote vya siasa vimesaini ili kuliepusha Taifa hili na
Machafuko.
Tunazitaka
Tume zote mbili kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kwa wale watakaotoa vitisho
kwa wananchi ama kwa wagombea. Tumesikitishwa na kitendo cha Tume kuacha
kuchukulia hatua baadhi ya wanasiasa wanaotumia lugha za vitisho kwa wananchi
au vyama vinavyokiuka muda wa kumaliza kampeni za uchaguzi.
Aidha,
tunavitaka vyombo vya habari vya umma kuacha mara moja kutoa fursa kwa chama
kimoja tu wakati tunafanya uchaguzi wa vyama vingi.
Taarifa
za kila wiki za Baraza la Habari na
Taarifa ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu zinaonyesha kuwa toka kampeni zianze vyombo vya Umma
hasa TBC na Habari leo vimekuwa zikionesha wazi wazi kukipendelea zaidi chama
Tawala katika habari zake na kuziacha ama kuzipa uzito mdogo taarifa za vyama
vingine.
Tunakemea
na kuvitaka pia baadhi ya vyombo vya habari vya binafsi kuacha kutoa taarifa za
kichochezi na za uongo kwa wiki moja hii kuelekea siku ya kupiga kura ili
kulinda amani ya Taifa.
Kipekee,
tunapenda kuvipongeza vyombo vya habari ambavyo vimefuatilia na kutoa taarifa za
kampeni za uchaguzi wa Tanzania 2015 kwa uhuru na haki wakati wote wa mchakato
huu.
Kwetu,
tunaona kuwa vyombo hivyo vimechangia kudumisha amani na vinastahili tuzo
maalum.
Pia
kwa umoja wetu tunatoa tahadhari kwa AZAKI
na viongozi wake kutokushiriki katika shughulizi za kampeni za vyma na
wagombea ili waweze kutimiza wajibu wa uwaanngalizi bila kukiuka maadili ya
AZAKI.
Tunawasihi
viongozi Wakuu wa Kitaifa wastaafu hasa Marais kutokuonyesha upande kipindi cha
uchaguzi na nyakati zingine zote ili waweze kuwa wasuluishi endapo hali ya
amani na usalama itapotea.
Taifa
linahitaji wasuluhishi wa ndani hivyo ni vyema viongozi wakuu wastaafu
wakalizingatia hili ukizingatia Tanzania
tumekuwa tukisifika kwa kuwa wasuluishi wa majirani zetu.
Mwisho
Sisi
ni Asasi za Kiraia (AZAKI) za nchini Tanzania zilizoundwa na kutambulika
kisheria na zinazofanya kazi katika
masuala mbalimbali ya kisheria, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Kwa
umoja wetu tunasimamia na kuhimiza utawala wa sheria na haki za binadamu na
masuala yote ya kimaendeleo ili kuhakikisha maisha ya watanzania yanakuwa bora
katika nyanja zote.
Kwa sababu hiyo, tunajiona tukiwa na jukumu
kubwa la kukemea na kuvitaka vyombo husika kufanyia kazi viashiria vyote vya
uvunjifu wa amani ili kulinusuru Taifa letu. Kamwe hatuwezi kunyamazia uovu
wala kunyamazishwa!
Imetolewa
kwa niaba ya AZAKI 300 nchini na asasi
miavuli zilizofanya mikutano mikuu ya mashirika wanachama kati ya tarehe 14 na
17 Oktoba 2015,
Dar
es Salaam
Tarehe
17/10/2015 na:
Ismail
Suleiman
Katibu
Mkuu
Baraza
la Taifa la Asasi za Kiraia

Post a Comment: