UKAWA TUTAREJESHA HESHIMA YA TANZANIA KIMATAIFA
KUPITIA
makala hii, naamini Watanzania watatumia fursa ya uchaguzi Oktoba 25, kuifufua
Tanzania ya Mwalimu Nyerere kupitia sanduku la kura kwa kuichagua Serikali ya
Ukawa.
Mwasisi
wa taifa letu, Mwalimu Nyerere aliipenda Tanzania na Afrika, hakupenda
ukandamizaji ndani na nje ya mipaka yetu.Tanzania ilijiweka katika ramani ya
dunia kutokana na msimamo na uongozi shupavu wa Mwalimu Nyerere kiitikadi,
kifalsafa na kimaono.
Aliposimama
katika Jukwaa la Umoja wa Mataifa kule New York, Afrika na mataifa mengine
yaliyopinga ukandamizaji yalikuwa nyuma yake. Aliposimama katika Jukwa la Umoja
wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kule Addis Ababa-Ethiopia, wanamajumui
(Pan-Africanist) walisimama nyuma yake.
Hakika
Afrika na dunia katika changamoto za leo itamkosa sana gwiji huyu mwana halisi
wa Afrika. Kwa Tanzania siku ya leo ni msiba zaidi. Tutapata fursa ya kupunguza
majonzi haya kwa kuifufua Tanzania ya Nyerere Oktoba 25, kwa kufanya mabadiliko
kupitia sanduku la kura na kuichagua Serikali ya Ukawa.
Itakuwa
hatari sana kumchagua Rais mwenye upeo mdogo kimataifa. Rais asiyejua hata
Saddam Hussein alikuwa Rais wa nchi gani? Anasema hadharani kwa ujasiri kuwa
alikuwa Rais wa Kuwait? Yaani kama hajui mtu maarufu wakati wa vita ya Marekani
na Iraq, Saddam Hussein alikuwa Rais wa nchi gani ataelewa nini kuhusu sera ya
Tanzania Mashariki ya Kati na Bara Asia? Kweli ataweza kuirejesha heshima ya
Tanzania ya Mwalimu Nyerere katika ramani ya dunia? Ataelewa nini kuhusu
diplomasia ya uchumi?
Katika
dunia ya leo pale ambapo dunia yetu inafanywa kama kijiji, huku mataifa
yakiungana na kuridhia uhusiano wao juu ya masuala mbalimbali na hasa ya
kiuchumi, taifa kuwa na sera ya nje makini inayolinda maslahi yetu katika
uhusiano wetu na mataifa mengine ni kitu muhimu sana. Ukitazama namna mataifa
yenye viongozi makini yanavyoendesha siasa zake za nje, utakuta suala la
maslahi ya kiuchumi limepewa kipaumbele sana. Diplomasia ya uchumi ndio
kiongozi wa nchi miongoni mwa mataifa mengine.
Hivyo
ni jambo lililo wazi kuwa hata wakija hapa, habari yao kubwa itakuwa ni
diplomasia ya uchumi. Watanzania tutumie fursa hii kujiuliza je, Tanzania kama
taifa huru limejiandaa vipi katika uhusiano huu ili kuhakikisha kuwa raia wake
wanafaidika na uhusiano huo? Sera yetu ya nje inasemaje? Wagombea urais na
vyama vyao wanasemaje kuhusu nafasi ya Tanzania katika medani za kimataifa?
Sera zao zinalinda vipi maslahi yetu wote?
Je,
viongozi wetu wanaitekeleza hata sera ya serikali iliyotokana na Chama Cha
Mapinduzi (CCM)? Haya tunayoyashuhudia hivi sasa ikiwemo safari nyingi za
gharama kubwa za Rais wetu aliyefikisha idadi ya ziara zaidi ya 410 nje ya nchi
(zaidi ya mwaka mmoja ) katika awamu zake mbili madarakani, ni utekelezaji wa
sera yetu wenyewe? Je, utekelezaji wa sera yetu unaleta uwiano mzuri na sera za
mataifa mengine na jumuiya za kimataifa?
Je,
sera hiyo inaleta uwiano mzuri na sera zetu za ndani na hasa katika masuala ya
uchumi? Je, tunaweza kusimama na kuizungumza sera hiyo kwa mwananchi wa kawaida
na akatuelewa na kuona maslahi yake kama Mtanzania ndani yake? Je,
inatekelezeka?
Maneno
Diplomasia na Sera ya Mambo ya Nje yamekuwa yakitumika wakati mwingine
kumaanisha kitu kimoja (Interchangeably), ingawa yana maana tofauti.
Kwa
mfano diplomasia maana yake ni uhusiano wa kimataifa kati ya nchi na nchi na
kati ya nchi na mashirika ya kimataifa (Mult-National Corporations). Uhusiano
huu hutengenezewa mbinu na mikakati endelevu (sustainable strategies) ya
utekelezaji wake kwa kila nchi kupitia sera zao za mambo ya nje.
Sera
ya Mambo ya Nje (Foreign Policy) ni tamko la nchi lenye kutoa mwongozo na
mwelekeo kuhusu madhumuni, malengo na misingi ya nchi katika kuhusiana na nchi,
mashirika ya kimataifa na wadau wengine nje ya nchi. Tamko hili pia ni
mwendelezo wa sera ya ndani ya nchi kama vile kwenye sera ya elimu, viwanda na
biashara, nishati, ulinzi, afya, kilimo na vitu vingine kama dira ya maendeleo
.
Sera ya Mambo ya Nje ya nchi ni chombo kinachobeba dhana na mbinu za
utekelezaji wa diplomasia.
Sera
hutoa mwelekeo juu ya misimamo ambayo nchi inaipigania na ile isiyokubaliana
nayo katika medani za kimataifa na itataka kutambuliwa msimamo wake wazi
kupitia sera. Sera hii ndiyo kitambulisho cha taifa husika katika kulinda tunu
(values) zake na kujipambanua miongoni mwa mataifa. Kwa hiyo ni jambo muhimu
kwa kuwa ni utambulisho wa nchi kimataifa, na tamko hili huakisi sera na
misingi ya ndani ya nchi husika.
Kwa
kawaida mratibu mkuu (coordinator) wa utekelezaji wa sera hii ni Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na sera hii hutekelezwa na serikali
nzima na wadau wengine ndani ya nchi, ambao shughuli zao zinahusiana na masuala
ya kimataifa.
Mkuu
wa nchi ndiye mwanadiplomasia namba moja, na Waziri wa Mambo ya Nje ni
mwanadiplomasia namba mbili katika nchi yoyote. Hawa ndio sura ya nchi mbele ya
dunia na ndiyo maana inabidi kuwa makini sana katika uchaguzi hasa uchaguzi
wetu mkuu kwani Uchaguzi Mkuu pamoja na kuwa unamchagua Rais wa Watanzania
lakini pia unamchagua mtu atakayebeba haiba ya Watanzania nje ya nchi, misimamo
yake ndiyo itakayowakilisha Watanzania nje ya nchi.
Ni
lazima kuwa na Rais mwenye uzoefu wa kiuongozi, mwanadiplomasia kwa muonekano
na kifikra. Tanzania ina sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 ambayo ilipaswa
kutoa mwongozo katika kufikia malengo ya nchi nje.
Kama
zilivyo nchi nyingine nyingi baada ya Uhuru tulikuwa na sera ya ukombozi ndiyo
maana tulijikuta tumechagua maadui na marafiki wakati wa ukombozi wa nchi za
kusini mwa Afrika.
Diplomasia
yetu sasa tofauti na awali, inatakiwa ilete manufaa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja
na kufungua masoko kwa biashara za Watanzania, bidhaa, kuvutia wawekezaji na
kuongeza watalii. Mkakati huu wa kutekeleza sera, umepewa jina la Diplomasia ya
Uchumi.
Diplomasia,
kama ilivyo mikakati mingine inayo vigezo na vipimo vyake. Diplomasia hufanyiwa
tathmini mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya kidunia.
Uimara
wa diplomasia ya nchi ni ushawishi wake kimataifa. Ushawishi wa nchi,
kihistoria umekuwa ukiambatana na nguvu ya kiuchumi au kijeshi (Diplomasia ya
Nguvu). Nguvu hizi mbili ni matokeo ya sera za ndani ya nchi. Pamoja na kuwa,
si lazima kuwa kila nchi yenye moja au vigezo hivyo viwili kufanikiwa katika
diplomasia. Ziko nchi ambazo zimefanikiwa sana kuwa na ushawishi mkubwa, pamoja
na kutokuwa na nguvu hizo duniani, kutokana na uimara wa sera yake ya mambo ya
nje, na wanadiplomasia wake (Nguvu ya Diplomasia).Tanzania chini ya Mwalimu
Julius Nyerere na Wanadiplomasia kama akina Salim Ahmed Salim ilikuwa miongoni
mwa nchi hizo.
Tanzania
imekuwa ikitoa misimamo mikali katika medani za kimataifa chini ya Mwalimu
Nyerere kutokana na haiba na misimamo yake kifikra iliyobeba mantiki za
kiushawishi kidiplomasia miongoni mwa mataifa makubwa.
Tanzania
kama mwanachama wa jumuiya ya kimataifa ni lazima irejeshe heshima na
utambulisho wake uliopotea baada ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.
Serikali
ijayo chini ya Ukawa imepanga kuanzisha harakati mpya za kuwezesha kuwepo mfumo
wa uchumi na biashara duniani wa haki na usiokandamiza nchi changa na pia
kuendelea na harakati za kujenga msingi wa nchi masikini kushirikiana zaidi
ikiwemo kufanya biashara zaidi baina yetu. Ni harakati za kurekebisha taasisi
za utawala wa siasa za kimataifa zizingatie matakwa na maslahi ya mataifa mengi
zaidi
Lazima
kuendelea kupambana na ukoloni-mamboleo (Neo-Colonialism) ambao kila kukicha
unachukua sura mpya ikiwemo kuhusisha misaada kwa nchi yetu na maslahi ya
kibiashara ya mashirika ya nchi zinatoa misaada hiyo, kupewa masharti ya kupata
misaada isiyo na msingi, na mashinikizo ya kufuata sera na kuchukua misimamo
isiyo na manufaa kwa nchi yetu.
Tanzania
imeshindwa kutoa misimamo yake thabiti kwenye majukwaa ya kimatifa kukemea
udhalilishji wa kushinikizwa kupewa misaada kwa masharti ambayo ni kufuru
katika Imani ya dini zote hasa masharti ya ndoa za jinsia moja.
Yote
haya ni kwa sababu sera yetu imepoteza mwelekeo na diplomasia yetu sio ya
uchumi bali ni diplomasia ya kuomba na kushukuru kutoka kwa mataifa makubwa
yenye kiu na ndoto za ubeberu.
Serikali
mpya ya Ukawa inalenga kuhakikisha kuwa utambulisho na sifa ya Tanzania
kimataifa inabebwa na Watanzania nje ya nchi badala ya sifa ya Rais kutunukiwa
shahada lukuki zisizo na tija katika medani za kiuchumi.
Diplomasia
yetu kimataifa ni lazima ilenge katika utamaduni, uchumi na biashara kuliko
ilivyo sasa ambapo diplomasia yetu ni ya kisiasa zaidi na haimgusi Mtanzania wa
kawaida. Rais wa nchi anapowekeza katika sifa na ufahari binafsi kwa kutunukiwa
medali ambazo hazina manufaa kiuchumi kwa Watanzania sio diplomasia ya uchumi
bali ni diplomasia inayotumikia na kutumikishwa kisiasa.
Majirani
zetu Kenya kwa mfano, wanapotoka nje ya mipaka yao na kujitambulisha kuwa wao
ni Wakenya moja kwa moja wanatambulika kutokana na umahiri wao katika mchezo wa
riadha. Riadha ni mchezo lakini unakuza uchumi wa Wakenya na utambulisho wao
kimataifa.
Nchi
kama India na wananchi wake kwenye sura ya kimataifa wanatambulika kwa umahiri
wao katika teknolojia ya mawasailiano, famasia na katika nyanja za utabibu huku
mataifa kama Ujerumani, China na Japan, raia wake wakionekana kuwa mahiri
katika Uhandisi. Ni lazima sera msukumo sahihi wa sera zetu za ndani kama
nilizoeleza katika mfululizo wa makala zilizopita ulenge kuhakikisha Watanzania
wanabobea katika nyanja mbalimbali ambazo zitaleta ushawishi katika diplomasia
yetu kimataifa na kuwa sura ya Tanzania nje ya mipaka yetu.
Ndio
maana katika ilani ya Chadema inayoungwa mkono na Ukawa tumewekeza na kuipa
kipaumbele elimu kwa sababu ni kupitia elimu tu tunapoweza kutoa vichwa ambavyo
vitaweza kuiweka Tanzania katika ramani ya juu kimataifa.
Iwe
katika soka, filamu au muziki ni lazima elimu ipewe kipaumbele ili tuweze
kufikia hatua walizofikia wenzetu kama Nigeria na Nollywood yao, Marekani na
Hollywood yao.
Katika
ushawishi kimataifa, mataifa makubwa kama Marekani yalitambua umuhimu wa kuitumia
burudani kupitia muziki, mpira wa vikapu, filamu katika kueneza ubeberu wa
kiutamaduni (cultural imperialism) kiasi ambacho vijana wengi duniani wakafikia
hatua ya kuiga utamaduni wa Marekani katika mavazi, katika kutembea na pia hata
watu wa daraja la kati wa nchi mbalimbali wakawa wanaiga staili za maisha za
Wamarekani katika maisha ya kila siku ili waonekane kuwa wameendelea na hata
katika lugha imekuwa hivyo hivyo. Hiyo yote ni mikakati iliyosukwa kueneza
ubeberu wa kiutamaduni.
Kupitia
mkakati huo taifa la Marekani likaendelea kupata ushawishi katika maisha ya
kila siku ulimwenguni na wakati huo huo wanamuziki, wacheza filamu na
wanamitindo wa Marekani wakaendelea kunufaika kiuchumi kutokana na kazi zao
kuwa na ushawishi kwa watu wengi duniani na kuwa soko la shughuli zao huku pia
taifa la Marekani likiingiza fedha nyingi.
Hapa
Afrika, Nigeria na Afrika Kusini zinakuja kwa kasi katika kutumia tasnia ya
filamu na muziki kueneza utamaduni wao hapa Afrika na kuwa na ushawishi.
Tanzania haiwezi kuendelea kubaki nyuma.
Vilevile,
katika kulenga kuitumia nafasi ya kidiplomasia kukuza uchumi wetu; serikali
ijayo ya Ukawa itaandaa sera maalumu kati ya Tanzania na nchi au kanda
mbalimbali ambazo ni muhimu kimkakati kama Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU),
Tanzania na nchi za Asia Mashariki (SEATO), Tanzania na nchi za Ukanda wa
Pacific, Tanzania na Mashariki ya Kati na pia Sera ya Tanzania katika
ushirikiano wake na mtangamano wa kikanda (regional Intergration) kama vile
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC na katika njia ya kuelekea (roadmap)
katika Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism) kupitia dhima ya Tanzania kwa Umoja
wa Afrika (AU).
Ni
kupitia mikakati hii tutakapoweza kutumia utalii wetu kukuza uchumi, pia
kulinda rasilimali za nchi yetu na kukomesha uporwaji wa rasilimali za taifa
letu.
Kwa
mfano, Tanzania ina uhusiano na baadhi ya nchi ambazo sio wazalishaji wa vito
vya Tanzanite lakini nchi hizo ndio wauzaji wakubwa wa Tanzanite duniani kuliko
mzalishaji wake halisi Tanzania. Kama Balozi zetu zingekuwa makini hali hii
ingerekebishwa.
Kuna
nchi ambazo korosho ya Tanzania imeuzwa kwenye soko la kimataifa kuliko
Tanzania wakati wazalishaji halisi ni Tanzania. Haya yote ni kutokana na
serikali yetu kutokuwa makini katika diplomasia ya uchumi.
Teuzi
za mabalozi wetu nje zimekuwa teuzi za kulipa fadhila badala ya teuzi
zinazozingatia taaluma. Tuna mabalozi na wanadiplomasia wasioifahamu sera
iliyopo na pia hawaelewi maana ya diplomasia ya uchumi. Wanadhani kuiwakilisha
Tanzania nje ni kushiriki dhifa za kitaifa wanazoalikwa na viongozi wa nchi
wenyeji na kutoa visa kwa raia wa kigeni kuja Tanzania tu basi.
Serikali
ijayo ya Ukawa itazingatia weledi katika teuzi za mabalozi na maofisa wa balozi
zetu nje. Ni lazima idara muhimu ya Usalama wa Taifa ihusishwe kikamilifu
katika teuzi za maofisa hawa. Ni lazima tuzingatie taaluma na uzoefu katika
nyanja za uchumi, biashara, uhandisi na intelijensia ya uchumi ili tuweze
kubadili mfumo wa ushirikiano kati ya Tanzania na jamii ya kimataifa.
Teuzi
ni lazima zizingatie msingi mkuu wa uadilifu na uzalendo. Watanzania waliowahi
kwenda nje ya nchi na waliopo watakubaliana name kuwa mabalozi wetu wengi na
baadhi yao maofisa wa ubalozi wamepoteza uzalendo na hadhi ya kutumikia nafasi
zao.
Watanzania
waliopo nje hawaoni ofisi za balozi zao kama nyumbani kwao kutokana na jeuri,
viburi na manyanyaso wanayopewa na baadhi ya maofisa wa ubalozi kinyume na
ilivyo kwa nchi nyingine. Wafanyabiashara wanaofanya biashara za nje hawapewi
ushirikiano wa kutosha kutoka ofisi za ubalozi wa Tanzania. Hii yote ni
kutokana na balozi zetu kujaza maofisa wasiokuwa na uzalendo, wavivu, wazembe
na wabinafsi waliopindukia huku wakilipwa kwa kodi za Watanzania. Hatuwezi
kuendelea kwa namna hii, tutaishangaza dunia.
Watanzania
wanaofanya kazi nje ya nchi maarufu kama wana-diaspora wanaweza kuwa mabalozi
wetu wazuri kiuchumi ikiwa mikakati thabiti itawekwa. Watu hawa wana mchango
mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu kiuchumi hasa katika sekta ya elimu,
afya na nyinginezo, Watanzania hawa wanaofanya kazi au biashara wamekuwa
wakitafuta fursa za kuwekeza nchini na kurudisha nyumbani walichovuna nje na
pia kuwasaidia ndugu zao.
Kwa
mfano nchi kama Nigeria mwaka 2013 wana-diaspora (Wanigeria waishio nje ya
nchi) walirudisha kati ya dola za Marekani bilioni tano hadi 10 kwa mwaka yaani
zaidi ya trilioni 10 na 20 kwa fedha za Kitanzania ambazo zinakaribiana na
bajeti yetu ya mwaka 2014/2015.
Tanzania
inapaswa kufuata nyayo hizi kwa kuwapa wana-diaspora umuhimu mkubwa katika
kukuza uchumi wa taifa letu.
Pia
serikali mpya ya Ukawa itatetea haki za binadamu, usawa wa nchi na kuimarisha
ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa. Tanzania haitakubali
kufumbia macho ukandamizaji wa haki za binadamu na itasimama kidete kupitia
nafasi yake kulinda ustawi wa demokrasia, utawala bora na kutetea haki za
binadamu kwa kuwa tunaamini dunia ni yetu sote na hakuna mwenye haki ya
kukandamiza haki ya mwingine.
Tutasimama
kidete kusimamia misingi ya uanzishwaji wa Umoja wa Afrika, Mkataba wa
Uanzishwaji wa Umoja wa Mataifa (UN Charter) kama ambavyo Tanzania chini ya
Mwalimu Julius Nyerere ilivyofanya katika medani za kimataifa.
Ni
katika misingi hii, tutaheshimu ujirani mwema, kulinda na kuheshimu mikataba na
majukumu ya kimataifa (International Obligation) ambayo Tanzania iliridhia.
Tutaimarisha
Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kudai mabadiliko ya mfumo ili kuleta usawa
wa nchi shiriki. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN Security Council)
lina changamoto ambazo tumekua tukizipigia kelele hasa juu ya upanuzi wa wigo wa
kidemokrasia na utendaji wake unaozingatia maslahi ya wachache na hivyo kubeba
ajenda za mataifa yenye nguvu kuamua juu ya masuala mazito ya dunia. Amani ya
dunia imewekwa rehani kwa mataifa haya matano tu.
Naomba
nimalizie kwa leo, kwa kuwataka wasomaji wangu na Watanzania kwa ujumla
mtafakari sana siku ya leo tunapoadhimisha miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa.
Tunayo fursa ya kuirejesha Tanzania inayojisikia fahari na itakayotembea kifua
mbele miongoni mwa mataifa na pia raia wenye ujasiri wa kujitambulisha kuwa
Watanzania miongoni mwa raia wa mataifa mengine.
Kupitia
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, tunayo fursa kupitia sanduku la kura
kumchagua Rais atakayesimamia kuirejeshea Tanzania nafasi yake kimataifa na
kuwanufaisha Watanzania kupitia nafasi ya Tanzania kimataifa.
Ni
hatari sana kuendelea na uongozi na mfumo wa chama tawala, CCM, ulioporomosha
heshima ya taifa letu mbele ya uso wa dunia. Kwa bahati mbaya, CCM
wamemsimamisha mgombea John Magufuli ambaye ameonyesha upeo mdogo sana katika
masuala ya kimataifa. Ndio maana sikuona ajabu kuona akimtaja Rais wa zamani wa
Iraq Saddam Hussein, kama Rais wa Kuwait mbele ya mkutano wa hadhara.
Sikushangaa
zaidi alipoonyesha upeo mdogo kwa kutaja kuwa Muammar Ghaddafi wa Libya
aliondolewa madarakani na wananchi wa Libya wakati Watanzania na hata dunia
inajua kuwa Muammar Ghaddafi aliondolewa kwa njama za mataifa ya nje kupitia
azimio namba 1973 la Baraza la Umoja wa Mataifa, lililoweka zuio la kuruka kwa
ndege za kivita (no-fly zone) na kusababisha Majeshi ya Kujihami ya Marekani na
Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia Libya. Ndiyo maana hapo juu nimegusia
umuhimu wa kupanua wigo wa kidemokrasia ndani ya Umoja wa Mataifa. Haya ya
Libya yasingefanyika kama kungekuwa na haki tunayoipigia kelele ndani ya Umoja wa
Mataifa.
Magufuli
bila haya au kutokana na kutoelewa masuala ya kimataifa haoni kuwa Serikali ya
Tanzania ilikuwa na fursa ya kuitetea Libya kupitia Umoja wa Afrika na au
Balozi wake wa kudumu kule Umoja wa Mataifa. Ni kutokana na Tanzania kupoteza
imani kimataifa ndio maana imekosa ujasiri wa kupaza sauti kama Tanzania ya
Nyerere ilivyokuwa mstari wa mbele kutetea haki na kulinda amani ya dunia.
Naamini
Serikali ya Chadema itakayoundwa kwa ushirikiano wa vyama washirika wa Ukawa
itairudishia Tanzania ujasiri wake wa awali. Edward Lowassa ambaye anatazamia
kushinda Uchaguzi Mkuu kwa bahati nzuri ana uzoefu mkubwa kimataifa na hadi
Bunge lilipovunjwa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya
Nje. Kutokana na ufinyu wa nafasi, naomba kuishia hapa kwa leo. Tukutane
Jumatano ijayo Mungu akipenda.
Mwandishi
wa makala haya ni Ben Saanane anapatikana kwa namba 0768078523.
Post a Comment: