Sunday, 18 October 2015









Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyama vya siasa, hasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) viko kwenye mzozo mkubwa wa wapi wananchi wanatakiwa wasimame baada ya kupiga kura Oktoba 25.

Sura ya 343 ya Sheria ya Uchaguzi, kifungu cha 104 (1) kinaeleza bayana kuwa mikutano wala watu waliovalia sare za chama au mabango yenye mwelekeo wa itikadi ya chama fulani hayataruhusiwa ndani ya eneo la mita 200 kuzunguka kituo cha kupigia kura.

Tume ya Uchaguzi, kwa kutumia sheria hiyo, inasisitiza watu kuwa mbali na kutotakiwa kufanya mikutano ndani ya eneo hilo, wananchi wanatakiwa warudi nyumbani baada ya kupiga kura siku hiyo.

Serikali nayo inaeleza kuwa ni marufuku kwa mtu kubakia eneo la kituo kulinda kura kama NEC inavyosisitiza kwenye matangazo yake, lakini vyama vya upinzani vinapingana na maelezo hayo.

Chadema, ambayo inaungwa mkono na vyama vya CUF, NLD na NCCR Mageuzi, imekuwa ikiwasisitizia wafuasi wake kuwa watakapomaliza kupiga kura wahesabu mita 200 kutoka kituoni na hapo ndipo wasimame kulinda kura zao.

Suala hili limezua utata mkubwa na tayari limepelekwa mahakamani kutaka tafsiri ya sheria hiyo, hasara kipengele hicho ambacho kisipotafsiriwa vizuri, kinaweza kuwa chanzo cha vurugu kubwa siku ya uchaguzi.

Ni kutokana na sababu hiyo tumeona tuwasihi wahusika wote kuliangalia suala hilo kwa makini badala ya kila upande kushikilia msimamo wake bila ya kujali athari.

Tatizo la sheria hiyo ni kukosa uhalisia katika mazingira ya makazi ya watu. Ni kwa nadra sana vituo vya kupigia kura vitakuwa maeneo ambayo yako mbali na makazi ya wananchi. Vingi viko ndani ya uzio wa mita zisizozidi 50 na hivyo wakati wowote polisi, ambao wanasimamia utekelezwaji wa sheria, wanaweza kuwakamata watu wakati wowote ule kwa kosa la kufanya mkutano ndani ya mita 200 bila ya kujali kuwa eneo walilokamatwa ni makazi yao.

Polisi wanaweza kutafsiri uvunjwaji wa sheria hiyo hata pale wanafamilia watakapokuwa kwenye shughuli zao za kijamii siku hiyo na hivyo kuamsha vurugu ambazo zinaweza kuepukika iwapo busara itatumika.

Serikali, NEC, Jeshi la Polisi na vyama vya siasa hawana budi kuacha kutoa kauli kali zinazoonyesha kutobadilika kwa misimamo yao na badala yake wakutane na kutathmini njia bora ya kuhakikisha sheria hiyo inaheshimiwa na wakati huohuo, amani inalindwa.

Siku zote pande zinazovutana zinapokutana, hupatikana njia bora ya kumaliza tatizo kuliko kila upande kutangaza misimamo yake kwa wakati wake na kuendelea kuchanganya wananchi.

Misimamo kama hiyo inawaandaa wananchi kwa vurugu, inawatisha wananchi kwenda kupiga kura kwa kuhofia vurugu zinaweza kutokea wakati wowote na inajenga picha kuwa wizi ni lazima utokee. Hakuna wakati ambao uchaguzi umetawaliwa na amani kama mwaka huu. Kumekuwa na matukio machache ya kuvunjika kwa amani tofauti na miaka mingine na pia Jeshi la Polisi limetekeleza wajibu wake sehemu nyingi bila ya kutumia nguvu za ziada kulinganisha na chaguzi zilizopita.

Ni rai yetu kuwa mwenendo huu usitibuliwe hatua za mwisho za uchaguzi kwa sababu tu ya utekelezaji wa kipengele hicho.

Tuna imani kuwa pande zinazohusika zitakutana mapema iwezekanavyo kujadili suala hilo na kulipatia suluhisho litakalokubaliwa na wote ili Uchaguzi Mkuu uishe kwa amani.

Post a Comment: