Friday, 23 October 2015

Pg 4 oct 22


MVUTANO mkali wa zaidi ya saa sita umeibuka katika kesi ya kutaka kujua uhalali wa wananchi ama wapigakura kukaa nje ya mita 200 kutoka katika vituo vya kupigia kura na kutaka tafsiri ya mahakama kuhusu kifungu cha sheria ya uchaguzi namba 104(1).

Mvutano huo uliibuka kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wakili wa mleta maombi katika shauri hilo wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilipoanza kusikiliza kesi hiyo jana.

Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu, Sekieti Kihiyo, Aloycius Mujuluzi na Lugano Mwandambo, ilianza kusikilizwa saa nne asubuhi huku upande wa AG ukiwakilishwa na mawakili wanane na mleta maombi akiwakilishwa na wawili.

WAKILI WA MLETA MAOMBI

Akianza kuwasilisha hoja, wakili wa mleta maombi, Peter Kibatala, alidai anaiomba mahakama iweze kutoa tamko kuhusu maana halisi na kusudio la kisheria la kifungu namba 104(1) cha sheria ya uchaguzi sura namba 343.

Pia aliomba mahakama hiyo iangalie maana ya kifungu hicho katika haki za wapigakura ama watu wengine wenye shauku ya kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.

Kibatala alidai msingi wa shauri hilo ni matamko yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwamba mpigakura ama mtu mwingine mwenye shauku asikae mahali popote katika kituo cha kupigia kura, hata kama atakuwa umbali wa mita 200 kutoka katika kituo wakati upigaji kura unaendelea.

Maelekezo hayo yalitolewa tena na Rais Jakaya Kikwete katika kilele cha Mwenge wa Uhuru na maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, Oktoba 14, mwaka huu na hakusisitiza katazo bali alikwenda mbali zaidi na kuonyesha kwamba asiyetii atachukuliwa hatua za kisheria.

Wakili Kibatala alidai lengo la kifungu hicho cha sheria ni kuzuia mikutano ya kampeni siku ya uchaguzi kwa sababu siku hiyo ni ya kupiga kura na si watu kukaa umbali wa mita 200 kwa utulivu.

Alidai sheria hiyo haimaanishi asiyefanya kampeni anazuiliwa kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200 na mtu anaweza kuvunja sheria mahali popote.

“Endapo mtakubaliana nasi kwamba mikutano inayozungumzwa ni ya kisiasa ama kampeni, basi watu kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200 kutoka katika kituo cha kupigia kura ni haki na haki hiyo haiwezi kuchukuliwa kwa madhanio ama misingi ya woga au hofu,” alidai.

Akijibu hoja hizo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson, alidai utetezi wao wameuelekeza katika makundi manne ambayo ni kuhusu haki za mpigakura za kikatiba, tafsiri ya kifungu cha sheria ya uchaguzi namba 104(1), yale makatazo yaliyotolewa na NEC, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Rais Kikwete na hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo.
Dk. Tulia alidai kwamba vifungu alivyotumia mleta maombi kuwasilisha maombi yake mahakamani hakuna mahali ambapo vimevunjwa kwa mujibu wa sheria.
Alidai anasisitiza kifungu namba 104(1) kinakataza mikutano ya aina zote bila kujali umbali.
Dk. Tulia alidai kifungu namba 72 cha sheria ya uchaguzi kinaelekeza watu wanaotakiwa kuwapo mahali zinapohesabiwa kura ambao ni mawakala, wagombea, waangalizi wa uchaguzi na wengine wanaoruhusiwa, ambaye hakutajwa katika kifungu hicho hatakiwi kuwapo.
Alidai kilichozungumzwa na NEC kuhusu kukaa umbali wa mita 200 yalikuwa ni maelekezo, yaliyozungumzwa na IGP ilikuwa amri na alichozungumza Rais Kikwete kilikuwa ni msisitizo.
Dk. Tulia alidai maelekezo yaliyotolewa na NEC yalifuata utaratibu, na aliyosisitiza Rais Kikwete alifuata maelekezo yaliyotolewa na NEC ili kuwapo kwa uchaguzi wa amani, huru na wa haki.
Alidai sheria inakataza kufanyika kwa mikutano mahali popote siku ya uchaguzi na umbali wa mita 200 unahusu mtu kuonyesha alama, picha, bendera za chama zinazosaidia chama ama mgombea kutoka katika kituo cha kupigia kura.

“Ipo mikusanyiko ya kawaida kabisa ambayo hatuwezi kuita mikutano, mfano misiba, ibada ambavyo inaweza kutokea watu wakakutana, hatuwezi kuita mikusanyiko, hiyo ni mikutano.
“Katika hali tuliyonayo sasa, watu waliojiandikisha ni 22,751,292 na Zanzibar 502,193, katika mazingira hayo watu wote hawawezi kukaa mita 200 kwa sababu ni idadi kubwa ya watu ambayo hakuna uhakika kwamba wote watakaa kwa utulivu, na hasa ikizingatiwa baadhi ya vituo vya kupigia kura vipo karibu na makazi ya watu,” alidai.
Alidai watu wana mwamko mkubwa wa kisiasa, tunaomba tafsiri ya kifungu hicho ichukuliwe kwa uzito wake, kwamba mikutano hairuhusiwi.
Mlalamikaji katika kesi hiyo ni Amy Kibatala ambaye ni kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyegombea ubunge wa viti maalumu wilayani Kilombero kupitia chama hicho, ambaye pia amejitambulisha kuwa ana masilahi katika uchaguzi huo.
Kibatala amefungua kesi hiyo dhidi ya AG na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC.
Katika mijadala hiyo, mara kwa mara Jaji Mujuluzi alikuwa akiingilia kati kuwataka mawakili kutoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo kauli ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kutaka wananchi wakimaliza kupiga kura waendelee kukaa kulinda kura zao

chanzo : Mtanzania (fikra yakinifu)


Post a Comment: