MAHOJIANO YA BBC SWAHILI NA MH EDWARD NGOYAI LOWASSA
Zuhura Yunus alimhoji Lowassa akiwa
nyumbani kwake Monduli, Arusha na kwanza akitaka maelezo zaidi kuhusu
kipaumbele chake cha elimu.
Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo..
Edward Lowassa: Watanzania wengi sana
hawapati elimu, hawapati elimu inayopasa, elimu bora. Unajua dunia ya sasa
imebadilika. Dunia ni Teknolojia. Ajira za dunia huzipati kama huna elimu
inayopasa. Na sisi elimu tunayotoa kwa kweli hatuwezi ku-compete katika dunia
ya leo.
Zuhura Yunus: Lakini Mhe. Suala ni hilo
la bure. Kwa sababu tayari tunajua walimu wamekuwa wakilalamika sana mishahara
yenyewe ni midogo. Hizo fedha zitatoka wapi, za mpaka watu waende bure?!
Edward Lowassa: Mbona wanazoendeshea
mashangingi zinatoka wapi? Kuna mashangingi makubwa sana ya Milioni 230 mtu
mmoja. Utakosa hela za kugawa kwa ajili ya wanafunzi? Au kwa mfano, pesa za
gesi, tuna gesi nyingi tu kutoka kusini sasa hivi.
Zuhura Yunus: Kwahiyo nahisi tukitegemea
gesi kwa sasa haitokuwa sawa. Kuna namna nyingine?
Edward Lowassa: Kwanza kwamba gesi
haitokuwa sawa si kweli. Ghana walikuwa na mgogoro kama hivi hivi. Lakini
wakaruhusiwa kukopa Gas Reserve. Unakopa Gas Reserve kwamba itakapofika mwaka
fulani nita.....kiasi fulani, nitawalipeni kodi lenu. Ingawa wanasema mpaka
2020, tunaweza kuanza kutumia kwa kukopa.... ... kuwekeza katika miundo mbinu
na rasilimali zinazostahili.
Zuhura Yunus: Kitu gani kimefanya mpaka
sasa hivi isiwezekane (elimu) kuwa bure? Maana'ke unasema inawezekana lakini
kwanini mpk sasa?
Edward Lowassa: Waulize walionitangulia.
Zuhura Yunus: Mheshimiwa, wewe umekuwa,
tukizungumzia suala hilo la waliokutangulia, umekuwa katika chama cha CCM kwa
takribani miaka 35, kwahiyo ulikuwa katika serikali hiyo, bila shaka ulikuwa na
uwezo wa kutekeleza hayo ya elimu bure, lakini.....
Edward Lowassa: Ukitaka kutekeleza ni
yule mwenye mamlaka. Ama ni waziri, ama ni waziri mkuu ama ni rais. Lakini
vilevile, nilipokuwa waziri mkuu nimesimamia elimu. Tulijenga shule za sekondari
kwenye kila kata ya nchi hii.
Zuhura Yunus: Hilo ni jambo jema wote
kupata elimu lakini si ya bure. Na ambapo ulikuwa katika nafasi ya Uwaziri Mkuu
ambayo ulikuwa na uwezo wa kupendekeza hilo la elimu bure..
Edward Lowassa: Mimi sioni kwanini
unaugua habari ya bure! Inawezekana. Hivi huko Ulaya wanatoza shule kodi?
Zuhura Yunus: Sikatai mheshimiwa kwamba
inawezekana, lakini nani atatekeleza? Kwa sababu kila mtu anaahidi, kila mtu
anasema, lakini watekelezaji..
Edward Lowassa: Watanzania wanipe
Mandate tarehe 25 Oktoba utaona nitakavyoitekeleza.
Zuhura Yunus: Lakini ulikuwa na nafasi
hiyo zaidi.. Umechukua nafasi nyingi za uwaziri mheshimiwa, mpaka Waziri Mkuu
si jambo dogo hilo..
Edward Lowassa: Nisikilize basi. Ndio
maana naomba nafasi hiyo sasa. Tarehe 25 Oktoba wakinipa Mandate hiiyo utaona utekelezaji
wake. Na mimi nakuahidi Wallahi itakuwa maajabu!
Zuhura Yunus: Kwahiyo unatakiwa uwe rais
ndio uweze kutekeleza hayo, sio? Huwezi kuwa waziri tu, waziri mkuu, mbunge..
Edward Lowassa: Kuna mambo ambayo waziri
huna mamlaka nayo.
Zuhura Yunus: Kwahiyo uliwahi kushauri suala
hilo likakataliwa?
Edward Lowassa: Nina hiyari ya kukataa
na kukubali.. Kusema kwamba nilishauri au sijashauri siwezi kusema!
Zuhura Yunus: Ufisadi: Una mkakati gani
wa kupambana nao? Manake ufisadi huo uko katika ngazi ya juu mpk ya chini
Edward Lowassa: Hilo ni swali gumu, refu
na lingetaka mjadala wake peke yake. Mimi nimetafakari, kwa kuanzia tu, tuanze
na One stop center. Ambako huko huduma za serikali zinapatikana. Kwahiyo
nikija, dirisha hili linapata hiki, dirisha hili linapata kile, nikiondoka
nimemaliza kazi. Tupunguze kidogo urasimu.
Zuhura Yunus: Na katika ngazi ya juu?
Hizo ni katika ngazi za chini lakini kuna viongozi...
Edward Lowassa: Ngazi ya juu ningetaka
kulitafakari kidogo. Wametoa taarifa juzi ya PPA ya hali ya Ufisadi ulivyo
nchini na kuorodhesha wizara zile ambazo zinaongoza.
Zuhurua Yunus: Unajinadi Mabadiliko. Ni
mabadiliko gani hasa?
Edward Lowassa: Baada ya miaka 50 ya
kujitawala, tunataka mabadiliko katika nchi yetu.
Zuhura Yunus: Mabadiliko hayo unahisi
kwa upande wa UKAWA ndio yanaweza yakafanyika?
Edward Lowassa: Sio nahisi tu, naamini
hivyo.
Zuhura Yunus: Kuna tofauti gani ambayo
unahisi kule ulishindwa kufanya utaweza kufanya wakati ukiwa UKAWA?
Edward Lowassa: Miaka ya nyuma kabisa
Mwalimu amesema, akitambua kwamba ndani ya CCM huwezi kupata mabadiliko, nje ya
CCM ndio unaweza kubadilika kwa sababu ni mfumo. Nahitaji kubadilisha mfumo
mnzima.
Zuhura Yunus: Lakini Mheshimiwa ukisema
sera za CCM.. Una kama Miezi kadhaa tu ulikuwa humo humo. Na bilashaka kama
usingekatwa ungebaki na mfumo na sera hizo hizo za CCM, si ndio?
Edward Lowassa: Unanionea! Mimi nimekuwa
mbunge wa kawaida toka miaka 8 iliyopita, sikuwa na madaraka yoyote katika
nchi, nilikuwa mjumbe wa vikao lakini sikuwa na madaraka katika nchi.]]
Zuhura Yunus: Baadhi ya wapinzani
wanasema kutokana na nafasi hii kubwa ya urais, wamekuwa wakizungumzia afya
yako. Wewe unawaambiaje?
Edward Lowassa: Afya yangu nzuri kabisa!
Zuhura Yunus: Kwa mfano, ikatokea
hukufanikiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nini mipango yako?
Edward Lowassa: Nitakuja kuchunga
Ng'ombe. Nina Ng'ombe, nitakaa na Ng'ombe wangu kijijini na kuendelea na
maisha..
Mwisho.

Post a Comment: