Lowassa: Kwa siku 100 nitafanya mambo 13
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Edward Lowassa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika viwanja vya TP Sinza Uzuri, jijini Dar es Salaam. Picha na Othman Michuzi
Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa
ametaja mambo 13 atakayoyafanya ndani ya siku 100 iwapo atachaguliwa
kuwa Rais, huku akisema “atawakata kilimilimi” wanaombeza kuwa hawezi
kuondoa umaskini wa wananchi.
Lowassa alikuwa akihitimisha mikutano minne aliyofanya kwenye wilaya
tatu za Jiji la Dar es Salaam jana kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers,
Kawe.
Wakati Lowassa akieleza hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu
Lissu alitangaza azimio la Kawe lililobeba ajenda kuu tatu, ikiwamo ya
kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa mwongozo wa jinsi Serikali yake
itakavyokabidhi madaraka kwa Ukawa kutokana na suala hilo kutokuwapo
kikatiba, huku mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitangaza mkesha
kwa wananchi siku ya kuamkia tarehe ya kupigakura na kutaka wanaume
wabakie kulinda kura zisiibiwe.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya watu na
viongozi wakuu wa Ukawa, Lowassa alisema mambo hayo atayatekeleza kwa
kasi ya kilometa 120 kwa saa.
Lowassa alitaja jambo la kwanza atakaloanza nalo kuwa ni uhakika wa dawa na vifaa vya uzazi wa akinamama.
Alitaja mambo mengine kuwa ni umeme wa uhakika nchi nzima, kupunguza
foleni jijini Dar es Salaam, kuondoa kero kwa wafanyabiashara
wadogowadogo na waendesha bodaboda, kumaliza tatizo la maji nchi nzima,
mfumo bora na rafiki wa wafanyabishara wakubwa na wadogo.
Kufuta ada na michango kwa wanafunzi, kupunguza kodi ya mshahara kwa
wafanyakazi, kufuta kodi zote za mazao ya wakulima, mkakati wa kukuza
michezo na sanaa, kuunda tume ya kutatua migogoro ya wafugaji na
wakulima, kuanzisha kituo kila wilaya kwa ajili ya kutoa huduma za
serikali na kuboresha maslahi ya polisi, wanajeshi na walimu.
Mbali na mambo hayo 13, aliahidi kumaliza kilio cha wananchi cha
kupata Katiba mpya inayotokana na maoni yao, akisema ni suala
linalohitaji kutuliza kichwa kulipatia ufumbuzi.
“Umaskini si mpango wa Mungu,” alisema Lowassa ambaye alikuwa
akishangiliwa kwa nguvu. “Nina hasira ya kupambana nao na kuwaondoa
Watanzania katika umaskini.”
Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyeihama CCM mwishoni mwa mwezi Julai,
aligoma kushuka jukwaani akitaka awekewe muziki acheze na maelfu ya
wananchi waliokuwa wakimsikiliza na kumkumbatia mkewe, Regina ambaye
alifika uwanjani hapo wakati mkutano huo ukikaribia kumalizika, kisha
akambusu.
Awali, Lowassa alisema idadi ya kura anazohitaji ili ashinde urais ni milioni 14.
Akiwa Mafinga mkoani Iringa, Lowassa aliomba wananchi wampigie kura
milioni 10 ili awe Rais lakini jana alisema kuna haja ya kupata kura
nyingi iwezekanavyo ili ushindi wake usiathiriwe.
“Kilichonileta hapa ni kuomba kura,” alisema Lowassa. “Naomba
mnipigie kura milioni 14 na ushee ili ziweze kutosha kuwa Rais. Baada ya
kupiga kura, wananchi mnatakiwa kuzilinda ili zisiibwe.”
Lissu
Kabla ya Lowassa kupanda jukwaani, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu
Lissu alitoa ufafanuzi wa alichoita “tamko la Kawe” ambalo ni kutaka
ufafanuzi wa jinsi ya kukabidhiwa madaraka kwa upinzani, kitu ambacho
alisema hakijaelezwa kwenye katiba.
Alisema jambo jingine ni kumtaka Rais Kikwete ajibu kauli iliyotolewa
na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo kuwa CCM
haitatoka Ikulu.
“Kikwete atueleze kama hili ni tamko ni la chama au Bulembo,” alisema
Lissu, ambaye pia anatetea kiti chake cha ubunge cha Jimbo la Singida
Mashariki.
Mbowe
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Lowassa, Mbowe aliwataka wafuasi na wanachama wa Chadema na Ukawa kuhakikisha wanakesha Oktoba 24 kujiandaa kupiga kura siku inayofuata.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Lowassa, Mbowe aliwataka wafuasi na wanachama wa Chadema na Ukawa kuhakikisha wanakesha Oktoba 24 kujiandaa kupiga kura siku inayofuata.
“Bado siku 24 tufanya uamuzi wa hatma ya maisha yetu na kuonyesha hasira kwa kutoichagua CCM,” alisema Mbowe.
“Tunakwenda kuanza safari ya uhakika ya kutoa mwanga kwa Taifa letu na kuonyesha heshima ya nchi na watu wake.
“Oktoba 24 ni siku ya nini? Ni siku ya kukesha kusubiri kupiga kura. Tunakubaliana tutakesha?”
Wananchi walimjibu kwa kelele kuwa watakesha na ndipo alipotoa maelekezo.
“Akinamama mkishapiga kura rudini nyumbani mkaandae chakula, ila
wanaume watabaki vituoni kulinda kura. Lakini hesabu hatua ya kwanza, ya
pili… hadi zifike mia na hapo pigeni kambi kulinda kura,” alisema
Mbowe.
Kwenye mkutano wa Liwiti, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye
aliendeleza kampeni zake za kumnadi Lowassa huku akirusha tuhuma dhidi
ya CCM na Serikali.
Sumaye alisema ni aibu kwa meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas
Masaburi kugombea ubunge wakati jiji analoongoza limekithiri kwa
kipindupindu.
“Ni lazima tuwe na aibu. Masaburi, jiji ni chafu limekushinda
kipindupindu `kinatamba’ sasa unataka ubunge wa Ubungo, unadhani
wananchi hawana akili za kupima,” alisema.
Akiwa Kawe, Sumaye alimshangaa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli
akisema kuwa huwa ana maamuzi ya kukurupuka hadi ashikwe shati na kwamba
akiwa Rais hakutakuwa na mtu wa kumzuia.
Alisema alitaka kuvunja jengo la Tanesco la Ubungo ambalo limejengwa
kwa kodi za wananchi, lakini akazuiwa. Pia aliamua kujenga barabara bila
ya kuwa na fedha za kuwalipa makandarasi na kusababisha Serikali idaiwe
Sh900 bilioni za riba, huku uamuzi wake wa kukamata meli ya uvuvi
ukiigharimu Serikali mabilioni ya fedha.
Mbatia
Naye mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alikitaka Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) kuitisha mkutano utakaovishirikisha vyama vya
siasa ili Ukawa na CCM wakubaliane kuyakubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu
ikiwa tu utakuwa wa uhuru na haki.
Mbatia, ambaye anagombea ubunge jimbo la Vunjo, alidai kuwa Serikali
imeuza hisa zake katika kampuni ya bia ya TBL kwa Sh176 bilioni na
kuzipeleka fedha hizo katika uchaguzi, huku akikitaka CCM kuibuka na
kujibu jambo hilo akisema anao ushahidi.
Mnyika na Lubuva
Akizungumza kwenye mkutano huo wa Kawe, mgombea ubunge wa Jimbo la
Kibamba, John Mnyika alimtaka mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Jaji Damian Lubuva kuwapa jibu kabla ya Oktoba 4, mwaka huu
kuhusu kupeleka wataalamu wao wa Tehama kwenda kuhakiki mfumo wa
utakaotumika kupokea na kujumlisha kura za urais kwa lengo la kujua kama
uko salama ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Awanadi Kubenea, Mdee, Mnyika
Akimnadi Saed Kubenea, ambaye anagombea ubunge wa Jimbo la Ubungo,
Lowassa alisema sekta ya habari itapoteza mwandishi mahiri katika kazi
yake, lakini wana Ubungo watakuwa wamepata mtetezi wa haki za wananchi.
“Kubenea ni jembe mchagueni ili akafanye kazi bungeni na kusimamia maendeleo ya jimbo lenu,” alisema.
Pia alimnadi mgombea ubunge wa Kawe, Halima Mdee akimuelezea kuwa ni sululu badala ya jembe.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Kalunde Jamal, Suzan mwillo na Raymond Kaminyoge
Post a Comment: