HOTUBA YA MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA JANGWANI OKTOBA 24, 2015
NDUGU
Watanzania wenzangu
• Ndugu
wanachama, marafiki na wapenzi wa
CHADEMA
• Ndugu
Viongozi
wakuu wa kitaifa na wanachama wa vyama vyetu vinne vinavyounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (UKAWA).
• Ndugu
Wana
mabadiliko na watetezi wa kweli wa maendeleo
• Mabibi
kwa Mabwana
Salaam Aleikum
Bwana Yesu Asifiwe
Tumsifu Yesu Kristo
NIANZE hotuba yangu hii ya kuhitimisha ziara ndefu za kampeni,
zilizonichukua mimi na timu yetu yote ya kampeni katika kaya, vijiji, kata,
tarafa, wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar katika kipindi chote
cha siku takriban 60.
Kama nilivyosema jana nilipozungumza na Watanzania kupitia
katika redio, televisheni na kwa njia tofauti za mawasiliano, tuna kila sababu
ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetuvusha salama.
Leo tunahitimisha safari ngumu, ndefu, iliyojaa miiba, milima
na mabonde tukitembea kifua mbele kwa namna mamilioni ya Watanzania
walivyojitokeza kutuunga mkono.
Kwa uchungu na masikitiko makubwa tunahitimisha safari ya
kampeni, tukiwa na kumbukumbu mbichi vichwani ya kuwapoteza wenzetu kadhaa.
Ni juzi tu, wiki hii hii tumemlaza katika nyumba yake ya
milele Mzee wetu, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Emmanuel Makaidi.
Tumewapoteza njiani kabla yake, Deo Filikunjombe, Dk. Abdallah
Kigoda, Mama Celina Kombani, kijana wetu Mohamed Mtoi na Estom Mallah, wote
hawa walikuwa wagombea ubunge.
Si hao tu, tukampoteza pia mmoja wa wanasiasa ambaye ni
muasisi wa mageuzi nchini, Mwenyekiti wa chama cha DP, Mchungaji Christopher
Mtikila.
Wote hao na wengine ambao sikuwataja hapa tunamuomba Mwenyezi
Mungu awapumzishe kwa amani. (Tusimame
dakika moja kuwakumbuka marehemu wote waliopoteza maisha katika kipindi hiki
cha kampeni)
Ndugu zangu
Mimi na mgombea
mwenza, Juma Haji Duni tumeona na kujifunza mengi. Tumejiandaa kikamilifu
kuijenga Tanzania Mpya. Tanzania ya ndoto ya waasisi wetu.
Ndugu Watanzania wenzangu
Katika ziara hizi,
nimeshuhudia vuguvugu la mabadiliko, kiu na ari ya Watanzania kuyapokea
mabadiliko hayo.
Lakini pia nimejionea
shida zinazowakabili wananchi hao.
Nimesikia na nyakati
nyingine kujionea kilio chao cha kunyanyaswa na kunyimwa haki zao na watendaji
wa serikali na baadhi ya vyombo vya dola.
Nimekisikia kilio
chao cha umaskini, afya na elimu duni.
Nimekisikia kilio
kikubwa cha vijana kukosa ajira na matarajio ya kesho bora.
Nimesikia rai za
Watanzania na ndoto zao za kupata maendeleo, maji safi, makazi bora na barabara
madhubuti.
Nimesikia malalamiko
ya wakulima na wafugaji kukosa maji, ardhi na namna wanavyotozwa ushuru na kodi
za kero katika mazao yao.
Nimesikia kilio cha madaktari,
wauguzi, walimu, askari na watumishi wa taasisi za umma kuhusu mazingira magumu
ya kazi, kodi za juu na maslahi duni.
Nimesikia kilio cha
wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusu ugumu wa mazingira ya kufanyia shughuli
zao, kodi kandamizi na kukosa mitaji.
Nimesikia kilio cha
wanawake kuhusu haki zao na ushiriki wao mdogo katika shughuli za kiuchumi.
Nimesikia kilio cha
wazee na wastaafu wasio na bima ya afya, wanaolipwa pensheni isiyokidhi
mahitaji yao na ugumu wa maisha yao uzeeni.
Tumekisikia kilio
dhidi ya rushwa na ufisadi uliokithiri
Tumekisikia kilicho
cha Watanzania juu ya udhaifu wa kiuongozi na utawala dhaifu wa CCM ulioshindwa
kuondoa umaskini
Tumekutana na vilio
vya watu walioonewa, kunyanyaswa na kupuuzwa na namna haki za raia zilivyopuuzwa.
Jibu langu ni fupi na
lile lile. TUMEONA, TUMESIKIA, TUMEELEWA NA TUTATENDA.
Baba wa Taifa,
alisema Uongozi ni kuonyesha njia. Tumejipanga vyema kuwaongoza Watanzania:
• Kwanza tumejiandaa kuongoza mapambano ya
dhati ya kuukataa na kuondokana na umaskini
• Tumejipanga vyema kupiga vita rushwa na
ufisadi kwa matendo na si kwa maneno matupu
• Tumejizatiti kuliandaa taifa kwa ajili ya
mapinduzi ya kweli katika elimu, kilimo, viwanda
• Tumejiandaa vyema kuwaongoza Watanzania
kuachana na mawazo ya kutegemea wafadhili na kuondokana na hulka za kuwa taifa
ombaomba
• Tumejipanga kufufua ari, dhamira na
misingi ya kujenga taifa linalojitegemea kiuchumi.
• Tumejiandaa vilivyo kuhakikisha tatizo
sugu la ajira linakoma.
• Tumeshaanza kufanya maandalizi ya
kuhakikisha serikali tutakayoiunda itafungua fursa mpya za ajira za ndani na
nje ya nchi kwa vijana wa Kitanzania
• Tumejizatiti kisera na kimikakati
kuwajengea Watanzania misingi na utayari wa kujiamini kifikra na kuchochea
fikra za kizalendo
• Tumejipanga na kujizatiti vyema kuleta
mabadiliko na mapinduzi katika utendaji wa kazi serikalini
• Tumejiandaa vyema kuijenga na kuiimarisha
sekta binafsi na kuijengea mazingira bora ya ushindani
• Tumejiandaa vyema kubadili na kuboresha
maisha ya wajasiriamali wadogo kama wamachinga, bodaboda na mama ntilie wakue
na kukomaa kibiashara.
• Tumejipanga vyema kuhakikisha raslimali
za taifa tulizonazo kama madini, gesi asilia na vivutio vya utalii
vinaimarishwa na kuwanufaisha Watanzania kwanza na siyo wageni kama ilivyo
sasa.
• Tumejizatiti kuifanya Tanzania kuwa taifa
la mfano kijamii, kiuchumi na kimaendeleo Afrika Mashariki na duniani kwa
kudumisha sera yetu ya uhusiano wa kimataifa ili iwe na tija kwa Watanzania.
• Tumejiandaa kuiondoa Tanzania kutoka
katika kundi la mataifa maskini duniani kwa kuhakikisha tunaanza kutumia vyema
raslimali zetu kujiletea maendeleo ya dhati.
Mambo hayo ndiyo msingi wa dhana ya mabadiliko tunayoyataka na
kuyahubiri.
Tunaamini na kutambua kwamba, mabadiliko yanaanza na fikra.
Sisi wana mabadiliko tunaamini kwa dhati kwamba MAENDELEO NI
AJENDA YA DHARURA kwa taifa na siyo jambo la lelemama.
Nimepata kulisema hilo siku zilizopita na nalisema tena leo
kwamba, serikali nitakayoiongoza itaanzisha mchakato mahususi wa MCHAKAMCHAKA
WA MAENDELEO.
Ni kwa sababu hizo, nawaomba Watanzania watuamini na wakubali
kutupa dhamana ya kuliongoza taifa kwa njia ya kura kesho.
Tuliyoona yamechochea ari na dhamira yetu ya dhati ya kuomba
ridhaa ya wananchi wa Tanzania na kushirikiana nao kuleta mabadiliko ya kweli.
Tulichokiona kimeniongezea ujasiri wa kuzidi kuuchukia
umaskini
Tumejipanga vyema na kwa kutumia Ilani yetu, utayari wetu,
uthubutu tulionao kuwaongoza Watanzania katika safari isiyo tu ya matumaini,
bali ya mabadiliko, uhakika na ushindi
Ndugu zangu,
Mimi na nyinyi, tuna kila sababu ya kukubaliana na Mzee wetu,
Kingunge Ngombale Mwiru, mmoja wa viongozi adhimu wa taifa hili ambaye amesema
CCM imeishiwa pumzi, hivyo haina uwezo tena wa kutufikisha katika kilele cha
mafanikio.
Mimi na ninyi Watanzania wenzangu tunapaswa kumuelewa kwa
vitendo Baba wa Taifa, aliyesema chama kimoja kinachokaa kwa muda mrefu
madarakani kinafikia hatua ya kujisahau. CCM ya leo iko mahututi.
Mimi na ninyi, tunapaswa kutambua kwamba maneno aliyopata
kuyasema aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba kwamba 'CCM
imepoteza dira' yana maana zaidi leo kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.
Mimi na ninyi tunapaswa kujifunza kutoka kwa majirani zetu
kama Kenya ambako wananchi walichukua hatua ya kuleta mabadiliko kwa njia za
kidemokrasia mwaka 2002 na leo hii Wakenya hawamo tena miongoni mwa mataifa ya
dunia ya tatu na maskini kama tulivyo sisi.
Mimi na ninyi, tunao wajibu wa kuikataa CCM kwa njia ya kura
tukitumia kauli ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe ambaye siku zote ametufundisha kwa
kusema chama kile kile, chenye watu wale wale na ambacho kina sera, fikra na
itikadi ile ile hakina uwezo wa kuongoza mabadiliko.
Ndugu zangu
Sina shaka hata kidogo kwamba, kwa njia ya sanduku la kura,
Watanzania wameamua kuongoza mabadiliko ya maisha yao na ya taifa lao.
Ndugu zangu.
Rais Bora ambaye Tanzania inamhitaji wakati huu Watanzania
wanapotaka mabadiliko ya kweli ni yule ambaye hata kabla hajakaa na wenzake na
kuafikiana mambo ya msingi ya kisera, kiitikadi na kimaandeleo, yeye mwenyewe
anayo maono ambayo anayaamini na kuyasimamia kwa dhati.
Urais si kazi ya
kubahatisha.
Urais si jambo la
pata potea.
Urais ni wajibu
na dhamana ya juu kabisa katika taifa
Urais si mamlaka
ya kutisha watu
Urais ni wajibu
wa kutoa dira ya taifa
Anayeomba urais anapaswa kuwa ni mtu aliyejiandaa na
kuandaliwa vyema kifikra, kinidhamu, kimaadili kimikakati na kimaono
Ili uwe rais bora unapaswa kwanza kuwa mtumishi bora wa
wananchi. Tunayo rekodi ya utumishi uliotukuka.
NDUGU zangu.
Ni jambo la kujionea haya sisi wenyewe kwamba miaka 54 baada
ya Uhuru, Tanzania bado ni taifa masikini, tegemezi na linalozidi kudidimia.
Ni jambo baya zaidi kwamba, CCM kwa njia za hila na rushwa
kinafanya juhudi kubwa kuzuia mabadiliko hayo.
Viongozi wakuu wa chama tawala, wanajaribu bila ya mafanikio
kupandikiza mbegu mbaya vichwani mwa Watanzania ili wayakatae mabadiliko.
Watanzania tunalo chaguo moja tu, kukubali kubadilika.
Tunayo fursa ya kufanya kile kilichofanyika kwa mafanikio
makubwa Zambia, Malawi, Kenya na kwingi kwingineko duniani.
Hatupaswi kusubiri hadi wananchi wakose subira na kupata
hasira na kukosa uvumilivu wa kuingia mitaani na kuwang'oa watawala
ving’ang’anizi wa aina ya CCM kama ilivyotokea, Libya, Tunisia, Irak na
kwingineko.
Tunapaswa pia kujifunza kutoka nje ya Afrika ambako yako
mataifa yaliyochupa kimaendeleo kwa sababu tu ya kupata uongozi madhubuti.
Siri wa mafanikio ya mataifa kama Malaysia, Korea Kusini,
Thailand na Singapore ambayo miaka 50 tu iliyopita yalikuwa katika kiwango cha
maendeleo kinachofanana na chetu ni UONGOZI wenye kuthubutu.
Ni fedheha kwetu kwamba, leo hii mataifa hayo ndiyo yamegeuka
kuwa nchi wahisani, wafadhili na wawekezaji wakubwa.
Je, ni sahihi kuendelea kushangaa na kuyatamani maendeleo
waliyopiga wenzetu hao? Jibu ni hapana.
Tunayo njia moja tu. Kuchukua hatua na kuleta mabadiliko yetu
wenyewe.
Hatuwezi tukatoka hapa tulipo iwapo tutaendelea kuwakumbatia
wale wale waliotukwamisha na ambao mawazo na mikakati yao ya kiuongozi ni ile
ile iliyoshindwa kutukwamua kutoka hapa tulipo kwa zaidi ya miaka 54 sasa.
Tutakuwa tukijidanganya iwapo tutawaacha watu hao ambao kwa
makusudi na kwa sababu zao walifikia hatua ya kukataa mawazo ya baadhi yetu
ambayo yalikuwa yanaakisi maono, fikra na mikakati tofauti na ile ya kimazoea
ambayo ndiyo hasa msingi wa kukwama kwetu.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo ambayo
nayasema tena leo kusisitiza kile ambacho nimekisema mara kadhaa:
1. Natambua kuwa uongozi ni dhamana. Mkinichagua
kuwa Rais wenu, nitaienzi dhamana hiyo kwa utendaji uliotukuka na kwa uadilifu
mkubwa.
2. Namuogopa Mungu, Nawaheshimu Watanzania. Naahidi
kwamba nitawatumikia kwa uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu zote.
3. Watanzania wenzangu, mabadiliko yanaendana na
kuthamini utu na kukataa hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya kuchagua.
4. Rushwa ya uchaguzi ndiyo sera ya CCM na ndiyo
nyenzo yao ya kuwakandamiza Watanzania. Tukatae.
Tuchague
mabadiliko, tuichague CHADEMA. Tuchague wagombea wa UKAWA.
5.
Mabadiliko ni fikra. Ili tubadilike ni sharti tuanze sasa kufikiri na
kutenda tofauti na ilivyo sasa.
6. Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kana
kwamba hatuna dharura ya maendeleo. Tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo
yetu wenyewe bila kutegemea wafadhili.
7. Nchi
nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika kizazi kimoja. Tujifunze kutoka
kwao. Tanzania pia inaweza. Tuchague Mabadiliko.
8. Tunapaswa tangu
sasa kuwa taifa linalotumia rasilimali zake kwa ufanisi zaidi kujiendeleza na
siyo kwa kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watwana katika nchi yao.
9. Umaskini si joho la ufahari. Tuukatae. Lazima
tuache kuwa taifa ombaomba. Hakuna faraja katika umaskini.
10. Mabadiliko hayawezi kuletwa na CCM. Miaka
zaidi ya hamsini ya utawala wake Watanzania bado ni maskini. Tusitegemee kuwa
wanalo jipya hii leo.
Ndugu zangu. Ilani yetu imechambua na kuainisha masuala ya
msingi ambayo serikali tutakayoiunda itayasimamia na kuyatekeleza hatua kwa
hatua.
• Katiba
–
Hili ndiyo msingi wa umoja na mshikamano wetu ndani ya CHADEMA na ndani ya
UKAWA.
-
Tutalifanya kwa umakini mkubwa huku tukiimarisha misingi ya umoja na mshikamano
wetu kitaifa.
• Elimu
• Hiki ndicho kipaumbele chetu. Elimu Elimu
Elimu
• Tunakwenda kuleta mapinduzi makubwa
katika elimu.
• Mfumo mzima wa elimu yetu utafumuliwa
• Serikali nitakayounda itagharamia elimu
bora tangu elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu.
• Ajira
• Hili ni tatizo sugu
• Tusipotatua tatizo hili tunatayarisha
bomu litakalolipuka
• Ni kwa kutambua umuhimu wa ajira ndiyo
maana nawatambua na kuwaheshimu vijana wabunifu – bodaboda, mama ntilie na
wamachinga.
• Hawa si wa kubezwa. Hawa si wa kuburuzwa
na kutishwa. Wanapaswa kuimarishwa ili waimarike kibiashara na kiuchumi
• Hawa kwangu ni mashujaa wa ajira.
• Afya
• Huku kunatakiwa mapinduzi makubwa.
• Tumejizatiti kujenga Hospitali za Rufaa
zenye hadhi katika kila wilaya
• Afya ndiyo msingi wa mafanikio yote
mengine. Pasipo afya hakuna tija
•
• Miundombinu
• Hii ndiyo injini ya uchumi wa mataifa
yote yaliyoendelea
• Miundombinu ni zaidi ya barabaraba
• Miundombinu ni reli, bandari, viwanja vya
ndege na kadhalika.
• Tumejipanga vyema kuimarisha eneo hili
kwa kujenga reli mpya
• Maji
• Hili ni tatizo mama
• Tunazidiwa hata na mataifa yaliyo
jangwani. Hii ni aibu kubwa
• Tunakwenda kujenga upya miundombinu ya
maji.
• Tatizo la uhaba wa maji litakuwa historia
• Michezo, Sanaa na Utamaduni
• Tumekuwa wasindikizaji katika eneo hilo
zima
• Tunayo mikakati ya kulikwamua taifa
kutoka huko
• Tanzania haitakuwa tena kichwa cha
mwendawazimu katika ulimwengu wa michezo
Tunayo Ilani ya CHADEMA na UKAWA inayotoa DIRA YA MABADILIKO
katika sekta na maeneo yote hayo.
Ndugu zangu Watanzania. Mkituamini, mkatuchagua.
Hatutawaangusha.
USHINDI WETU NI USHINDI WA WATANZANIA
NI WAKATI WA MABADILIKO
TUNAOMBENI KURA
Ahsanteni kwa kunisikiliza
Post a Comment: