HALI BADO TATA ZANZIBAR
UCHAGUZI mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uchaguzi wa
kumchagua Rais wa Zanzibar unaotarajiwa Oktoba 25 unakabiliwa na mtihani
mgumu kutokana na kampeni chafu inayoendeshwa na makada wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Ni Dk. Ali Mohamed Shein peke yake anayeeleza atawafanyia nini
wananchi akichaguliwa tena akianzia na kutaja mafanikio ya serikali
tangu 2010, na kutoa ahadi mpya nyingi na kubwa zisizotekelezeka.
Wasaidizi wake katika chama hawamsaidii bali wanaeneza uongo sana.
Fikiria wanapotaja Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaohusisha Chama
cha Wananchi (CUF) chenye nguvu kubwa Zanzibar na vyama vingine vitatu
kuwa ni kundi la magaidi ambalo eti linatumia Jumuiya ya Uamsho kueneza
ugaidi nchini.
Huku ni kukosa umakini na kuamua kwa makusudi kuchochea chuki za
kidini Zanzibar ambako kilio kikubwa cha wananchi ni masheikh wao
kutungiwa kesi ya ugaidi na kuwekwa jela Tanzania Bara bila ya
kujulikana kikomo cha kadhia hiyo.
Ni fitna tosha dhidi ya kile walichokuwa wakikisema viongozi Uamsho
kuwa Muungano unainyima haki Zanzibar ya kujitawala na kujiamulia mambo
yake
.
Kitendo cha Zanzibar kuingiliwa uhuru wake CCM na Serikali ya
Muungano (SMT) ambayo imehodhi sio tu nguvu zote za dola bali pia za
kiuchumi kupitia Benki Kuu (BOT) iliyo na mamlaka ya kusimamia na
kuidhamini Zanzibar iweze kupata mikopo ya nje, kinazidi kuthibitisha
udhaifu wa viongozi wa CCM.
Si hilo tu lakini Zanzibar haiwezi kujitegemea chini ya muundo wa
Muungano uliopo wa serikali mbili na kuwepo ulazima kwa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikitaka isitake ifuate Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 ambayo imehodhi mamlaka ya mambo yote ya ulinzi
na usalama na kwamba Rais wa Zanzibar si amiri Jeshi mkuu, hana mamlaka
ya kikatiba ya kuamuru vyombo vya dola kwa lolote lile.
Na kwa sababu hiyo, hana uwezo wa moja kwa moja wa kuamuru Jeshi liwe
la Polisi au la Ulinzi (JWTZ), lazima apewe idhini ya kufanya hivyo na
mamlaka iliyo juu yake – Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Ni uongo usio na kificho kuwaeleza wananchi kuwa Zanzibar ina mamlaka
kamili ya kidola na vikosi vyake havitasita kuchukuwa hatua kudhibiti
vitendo vya kigaidi view vinafanywa na masheikh au na watu wengineo.
Kwamba hakuna atakaeachwa, atashikwa hata akiwa ni mfuasi wa chama
gani, ni kauli za vitisho zinazochapuzwa na uongo wa kujikweza katika
majukwaa ya kampeni ambayo wagombea hasa wa CCM wanaona ni sawa tu
kutumia misamiati ya kushabikia kuwepo ugaidi, pasina kutafakari athari
za propaganda za aina hiyo.
Ugaidi si suala la mzaha bali ukatili na unyama usioendana na heshima
na utu wa binaadamu. Ugaidi ni ushenzi na uwendawazimu usioweza kuwa
sera ya kuomba kura. Hakika makada wa CCM wanajenga watu chuki kwa
malengo ya kufanikisha matakwa yao ya kisiasa.
Hawajali kuwa vitendo kama hivi ndivyo vinavyopandikiza mihemuko ya
hisia ambayo katika wakati huu wa uchaguzi huweza kusababisha
kuitumbukiza nchi katika mauaji mabaya ambayo kwingineko yameishia
kuwasomokeza viongozi wa kisiasa, vyombo vya dola na waandishi wa habari
Mahakama ya Makosa ya Uhalifu wa Binadamu (ICC) iliyoko The Hague,
nchini Uholanzi.
Zanzibar tangu dahari ni nchi ya watu mchanganyiko wa makabila na
dini, wanaoishi kwa upendo mkubwa na kusaidiana. Waislamu na Wakristu
wamekuwa wakiishi kama ndugu miaka yote ya historia ya Zanzibar.
Kuwachochea chuki leo ni hatari isiyovumilika.
Wanaotaka ugaidi waone mifano ya nchi zilizofikwa na uovu huo. Hebu
waitazame Kenya inavyohaha kuimarisha ulinzi wa ndani na mipakani hasa
kaskazini katika kukabiliana na kinachoitwa ugaidi.
Basi makada wa CCM wasaka uongozi, wanaposimama majukwaani na kujenga
hoja ya ugaidi wakidhani ndio turufu ya kuweza kuchaguliwa, wajue
wanaota uwendawazimu badala ya ustaarabu na uzalendo, na wala
haitawasaidia ila hasara.
Mtu mwenye kufikiri vizuri anachokiona ni kushuhudia makada hao walivyofilisika kisiasa.
UKAWA kupitia viongozi wagombea urais wa Tanzania, Edward Lowassa, na
mgombea urais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, wanachosimamia sio
ugaidi isipokuwa kutumia akili kupambana na CCM kwa lengo la kutokomeza
mifumo ya utawala mchovu na kujenga badala yake, utawala mpya utaokuza
mifumo inayoimarisha haki, uadilifu na imani ya kuwaondolea shida
Watanzania na Wanzanzibari.
Wanalenga kupunguza athari za umasikini kutoka walikokuwa kwenye
ukiritimba wa CCM kujiona ni chama pekee chenye haki ya kutawala na
kufanya watakavyo hata kama viongozi na makada wake hadi Jumuiya zake
zinakosea.
Makada wa CCM kila leo wanawataja Lowassa na Maalim Seif kama ajenda
ya mikutano yao ya kampeni. Kila siku midomoni mwa viongozi wakubwa wa
CCM na makada wapandia meli iliyotoboka wakiwahusisha wagombea hao wa
CUF na CHADEMA katika uvurugaji wa nchi kukosa muelekeo na kuwaacha
mamilioni ya Watanzania na vilio vya unyonge, ulofa na hofu ya matumaini
ya kurudisha malengo ya Azimio la Arusha ambalo limepigwa teke na
watawala wa CCM na malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia manifesto ya
Chama cha ASP yaliyozikwa kwa kukumbatia viongozi wabadhirifu, wapenda
mali na wanaoabudu rushwa serikalini.
Zanzibar inanyonywa na wazawa wake wakibaguliwa na kuporwa ardhi
waliyorithi na kuitumia kama rasilimali ya kuendeleza maisha yao. Kwa
mgongo wa uwekezaji, wageni wamemilikishwa ardhi na kuwa kikwazo cha
maendeleo ya Wazanzibari.
Ni kwa muktadha huo, UKAWA kupitia CUF na CHADEMA wamevaa njuga na
kuhakikisha mfano uliopo wa serikali zote mbili za CCM, unabadilika na
kutoa nafasi kwao kuanzisha mfumo unaokidhi matumaini mapya ya wananchi
ya kujikomboa kutoka manyanyaso ya wageni wanaopora rasilimali za nchi
na zaidi kuondoa kabisa ubaguzi wa kipato na uchumi na miongoni mwa
Watanzania na Wazanzibari.
Kwa kasi yao kubwa na moyo wa kuzidi kujitoa mhanga, wanasiasa hawa
wawili wenye historia ya ushupavu kiuongozi wakiwa serikialini na katika
CCM kabla ya kufukuzwa kiaina, hakuna kurudi nyuma; dhamira ya
mabadiliko itazidi kuimarika kupitia sera za UKAWA zinazolingania
vuguvugu la kuondoa muundo wa serikali mbili na kuleta wa serikali tatu
unaotarajiwa kutambua haki ya kila nchi – Zanzibar na Tanzania Bara –
kuwa washirika wa Muungano usiokuwa na shaka ya nchi moja kuiburuza nchi
nyingine.
Chanzo: Makala ya Enzi Talib kwenye gazeti la Mawio la tarehe 2 Oktoba 2015
Post a Comment: