TAARIFA DHIDI YA MAHUJAJI KUTOKA TANZANIA WALIOFARIKI NA KUJERUHIWA HUKO SAUDI ARABIA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz
Tovuti : www.foreign.go.tz
Nukushi: 255-22-2116600 |
KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,11466 DAR ES SALAAM, |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa za kufariki kwa Mahujaji zaidi ya 700 na
wengine zaidi ya 800 kujeruhiwa wakati wakishiriki ibada ya Hijja
iliyofanyika Makkah, Saudi Arabia tarehe 24 Septemba, 2015.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania, Saudi Arabia
Mahujaji hao walifariki na kujeruhiwa kutokana na msongamano mkubwa wa watu uliotokea kwenye eneo la Mina.
Aidha,
taarifa hizo zinaeleza kuwa hadi sasa Mahujaji wapatao watano (5)
kutoka Tanzania wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa. Majina ya
Watanzania waliofariki na kutambuliwa ni Bi. Mwanaisha Hassan Juma,
Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla. Mtu mwingine aliyefariki
ni Raia wa Kenya anayeishi nchini ambaye ametambulika kwa jina la Bi.
Fatuma Mohammed Jama.
Ubalozi
unaendelea na jitihada za kupata jina la Mtanzania mwingine aliyefariki
kwenye tukio hilo. Aidha, Serikali ya Saudia imetangaza kuwa itatoa
taarifa kamili ikiwemo idadi ya watu waliofariki na majeruhi na nchi
wanazotoka mara itakapokamilika.
Pia
Ubalozi wetu kwa kushirikiana na Taasisi zinazoshughulikia masuala ya
Hijja za Tanzania ikiwemo BAKWATA pamoja na Mamlaka za Serikali ya Saudi
Arabia unaendelea kufuatilia kwa karibu ili kujua endapo kuna vifo na
majeruhi wengine kutoka Tanzania.
Hivyo basi, Wananchi wanaombwa kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
25 Septemba, 2015
Post a Comment: