Rungwe: Umaskini wa Tanzania ni akili finyu za watawala
MGOMBEA Urais wa Chama cha Ukombozi ( Chaumma), Hashim Rungwe (kulia) akiwa na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete
Mbali na hilo amesema kama watawala wasingekuwa na akili zilizodumaa ni wazi kwamba kila mtanzania angekuwa na maisha bora na elimu ya kutosha.
Rungwe aliyasema hayo jana mchana wakati akihutubia wananchi katika uwanja wa Majani ya Chai mjini hapa.
Kutokana na hali hiyo amewataka watanzania kutoichagua tena CCM kwani
chama hicho ndicho shetani mkubwa wa kukosekana kwa maendeleo na
kusababisha umasikini kwa watanzania licha ya kuwa nchi imezungukwa na
rasilimali kila kona.
Rungwe alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara katika kunadi sera ya kuomba kura ili achaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano.
Amesema iwapo atachaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 ataunda baraza la mawaziri dogo lisilozidi watu 20.
“Nitahakikisha naunda baraza dogo la mawaziri lisilozidi watu 20 ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,” amesema Rungwe.
Amesema kuwa ataziunganisha wizara ambazo majukumu yake yanafanana ili kupata baraza hilo dogo la mawaziri.
“Kwa mfano wizara ya Uchukuzi na ile ya Mawasiliano nitaziunganisha
na kufanya wizara moja, wizara nyingine ni ile ya kilimo nitaiunganisha
na mifugo kuwa wizara moja, zipo nyingi tu zinaweza kuwa wizara moja,”
amesema.
Amesema katika baraza hilo atavishirikisha vyama vyote ambavyo vilisimamaisha wagombea urais ili kuunda umoja.
“Katiba haina kifungu ambacho kinakataza kuchanganya watu kutoka vyama vingine vya siasa,” amesema Rungwe.
Akizungumzia kuhusu suala la Katiba, Rungwe alisema iwapo atapata
ridhaa ya wananchi kuiongoza nchi atatengeneza Katiba ya wananchi.
Amesema katiba ya wananchi hiyo itachukua baadhi maoni ya Tume ya
Marekebisho ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mstaafu Joseph
Warioba.
Alifafanua kuwa msimamo wa chama chake ni muundo wa serikali tatu ambao utakuwa na serikali ya Muungano, Zanzibar na Tanganyika.
“Kutakuwa pia na mabaraza mawili la Tanganyika na Zanzibar halafu na Bunge la Muungano litakalojadili masuala ya Tanzania.
Mbunge wa Zanzibar hawezi kujadili utendaji na bajeti ya wizara ya
kilimo wakati kule Zanzibar pia ipo wizara kama hiyo,” amesema.
Kwa upande wa tatizo la ajira, amesema atahakikisha anaanzisha
viwanda 20 mkoani hapa ili vijana na watu wasio na ajira waweze
kunufaika.
“Nikichaguliwa nitahakikisha kuwa najenga viwanda 20 hapa Dodoma,” amesema mgombea huyo.
Pia amesema akipata urais atahakikisha anapambana na tatizo la
ufisadi ambalo lipo nchini na kuwafanya wananchi wasifaidi vyema
raslimali za Taifa.
Kwa upande wake Mgombea ubunge wa Dodoma Mjini kwa tiketi ya Chaumma,
Kayombo Kabutare amesema atahakikisha anamaliza mgogoro wa kisheria
kati ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu ya Mji wa Dodoma (CDA) na
wananchi ambao umewafanya wananchi wakose haki ya kumiliki ardhi yao.
Amesema endapo atachaguliwa atahakikisha ardhi inarejeshwa katika manispaa ili kuwapa haki ya umiliki kwa wananchi
HABARI CHANZO : MWANAHALISI ONLINE
Post a Comment: