Thursday, 1 October 2015



Naam As-salamu alaykum waungwana,karibuni tena, tupate kilichojili leo kwenye kijiwe cha mtaa wetu wa siasa,kama mada inavyowasilishwa kwenu na mwanahekaya mkuu.
Basi leo siku ilikua nzuri kwa watani hawa wa jadi hapa kitaani,na walianza vyema sana kwa kila mmoja kuiwamba ngozi yake kwa mafuta aghalabu mno kuyapata hapa mtaani.
Baada ya kila upande kuonesha umaridadi wa jinsi alivyoiwamba ngozi ya ngoma atakayoipiga kwa msimu wa 2015/20 ndipo wachangiaji walipoanza toa yao katika kuboresha mashindano.kwa sasa nitaeleza mchango wa mmoja wa wachangiaji ambaye yeye aliuliza “yuko wapi mzee kifimbo cheza?”
Binafsi namkumbuka mzee huyu ambaye alikua mkali sana kwa waharibifu/wachafuzi wa lugha waliongozwa na madenge, lodi lofa , watoto mapacha na wengineo.hivyo swali lake liliamsha sikio langu na kutega vizuri kwanini kauliza hivyo.
Ndipo nilipomsikia akianza kulalama,hawa wajamaa zetu hawana adabu kabisa siku ile jangwani mkuu wao alituita sisi malofa wao wakachekelea,haikutosha wakaenda karatu wakatufananisha na mnyama nyumbu asiyeona.yote hayo sisi tumekaa kimya sasa wanamuita mtu aliye hai marehemu.hivi kweli hawa wanaijua vyema lugha ya Kiswahili !? lakini yuko wapi Yule mwalimu wa kudhibiti lugha chafu kama hizi za mafisiemu !?
Basi ukimtizama mchangiaji jinsi alivyokua anaongea kwa hisia hakika lazima aguse hisia za mtima wako,na katika kuchombeza hili mwenzetu mmoja akaongezea "eeh jamani !!" hivi huyu bwana sijui ana adabu gani !? maana baada ya kututusi sisi majirani haikutosha sasa ameanza kuwatusi  ndugu zake na kuwaita kunguni.kweli ndugu yako unamuita na kunguni !?,na kama ndugu yako ni kunguni hakika unamaanisha nawe ni wajamii hiyo,je tukuache uendelee kunyonya damu zetu !? la hasha hapana.
Taharuki kubwa ilitupata ghafla pale mwenzetu Mwinyimpeku aliposema mzizi ule wa muarobaini mchungu tuliozoea kutuadhibu kwa zaidi ya miaka 50 pasipo kukatika,dawa yake ni kuumwagia chumvi nyeupe kwenye shina.
Aliposema hayo naaam namimi huyooo nikamaliza funda langu la tangawizi na andazi nililoshika kisha kunyenyuka taratibu kuja kuwajuza hekaya za leo,huku moyoni nikijisemea tena “kumbe dawa ya muarobaini mchungu ni chumvi nyeupe”

Post a Comment: