ACT-Wazalendo waunga mkono utafiti Twaweza
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimekubaliana na matokeo ya utafiti
yaliyotangazwa jana na Taasisi ya Twaweza. Utafiti huo ulihusu maoni ya
wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Katika matokeo hayo taasisi hiyo ilimtaja mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli kuwa chaguo la Watanzania wengi kwa kupata asilimia 65.
Utafiti huo pia umeonesha kwamba, mgombea urais wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na anayeungwa mkonono na Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa alipata kura 25.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Mwenyekiti wa
Kamati ya Uchaguzi na Kampeni Taifa wa ACT, Nixon Tugara ametaja
changamoto hizo kuwa ni afya imetajwa kwa asilimia 59, Maji, asilimia 46
na elimu 44.
“Katika afya ACT Wazalendo tumeainisha waziwazi kwamba kutengeneza
mfumo imara na endelevu wa upatikanaji wa maji hasa vijijini ni njia
muhimu katuka kuimarisha afya za wananchi. Kwa maana hiyo hiyo utafiti
huo umeonesha kuwa chama chetu na ilani yetu ilizingatia vya kutosha
mahitahi ya jamii ya sasa na muda ujao katika nchi yetu,” amesema
Tugara.
Tugara ameongeza kuwa, licha ya kuzingatia mahitaji ya wananchi
lakini pia chama kinajivunia kupata asilimia zaidi ya moja kutajwa na
wananchi katika utafiti huo na kwamba, “ACT inashika nafasi ya nne
ukiacha CCM na vyama vitatu vinavyounda Ukawa.”
Amedai kuwa, ACT kinajivunia kuwa Twaweza imekiri kwamba wakati
utafiti huo unafavyika chama hicho kilikuwa bado hakijazindua kampeni
zake wale kumtangaza rais wao hivyo ilikuwa na nafasi ya kufanya vizuri
zaidi katika utafiti huo.
“Kutokana na kufanya vizuri sana katika uzinduzi wetu na kampeni hizi
zinazoendelea nchi nzima tunaamini kuwa endepo utafiti huu ungefanyika
tena hata leo ACT tungefanya vizuri zaidi kwa kuwa chama chetu kinapedwa
na watu wengi zaidi,” amesema Tugara.
Akizungumzia maendeleo ya chama hicho amesema, tangu walipozindua
kampeni 30 Agosti mwaka huu, wagombea wengi wamekuwa wakitumia pesa zao
binafsi kutokana na uhaba wa fedha ndani ya chama.
Tugara amesema, kwa sasa chama hicho kinakabiliwa na uhaba wa fedha
za kuendeshea kampeni zake hivyo inapelekea kuchelewa kuwafikia wananchi
katika baadhi ya maeneo.
“Tunatoa wito kwa Watanzania wote popote walipo kwa utashi wao waweze
kuguswa na kuchangia kampeni zetu kwa kiasi chochote walichonacho.
Tunaomba mchango ili tuendeleze mapambano ya kuijenga Tanzania kwenye
misingi yake” amesema Tugara.
habari chanzo na mwanahalisi online
Post a Comment: